Tanzania yaiita Urusi kuwekeza kwenye gesi, uzalishaji simu janja na teknolojia

Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC), Dk Godwill Wanga akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara kutoka nchini Urusi.
Muktasari:
- Tanzania huagiza bidhaa kutoka Urusi za wastani wa dola bilioni 2.26 (Sh5.93 trilioni) kwa mwaka, zikiwemo ngano, kemikali na mashine, wakati mauzo ya Tanzania kwenda Urusi yanasimama kwenye dola milioni 5.8 pekee.
Dar es Salaam. Serikali imewataka wawekezaji kutoka Urusi kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo nchini, hususan katika maeneo ya kimkakati kama gesi asilia, uzalishaji wa simu janja, na teknolojia ya kidijitali.
Hatua hiyo inalenga kukuza uchumi wa viwanda na kuimarisha urari wa biashara kati ya Tanzania na Urusi.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Urusi kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk Godwill Wanga amesema Tanzania inaendelea kutafuta kwa dhati washirika wa kimataifa ili kuimarisha uwezo wake wa kiuchumi.
“Tanzania ina utajiri mkubwa wa gesi asilia ambao bado haujatumiwa ipasavyo. Tunataka kushirikiana na kampuni za Urusi zenye uzoefu ili kukuza sekta hii kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na uchakataji wa viwandani,” amesema Dk Wanga.
Licha ya kuwepo kwa zaidi ya viwanda 80,000 vilivyosajiliwa nchini ni 57 pekee vinavyotumia gesi asilia kama chanzo cha nishati na matumizi ya kiwandani.
Aidha, ni magari takriban 5,000 tu yanayotumia gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG), huku kaya zilizounganishwa na gesi ya kupikia kwa njia ya mabomba zikiwa ni 1,500 pekee.
“Urusi ina kampuni kubwa za nishati zenye uzoefu na mafanikio tunayohitaji. Tuko tayari kwa ushirikiano utakaoleta mafanikio ya pamoja,” ameongeza.
Dk Wanga pia amesisitiza umuhimu wa kuanzisha viwanda vya kuunganisha simu za mkononi nchini, hasa wakati huu ambapo Tanzania imeanza safari ya mabadiliko ya kidijitali ya miaka kumi.
Amesema Serikali inatoa vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kwa wawekezaji watakaowekeza katika uzalishaji wa vifaa vya kidijitali.
“Kutokana na ongezeko la mahitaji ya vifaa vya kidijitali, kuanzisha kiwanda cha kuunganisha simu ni jambo la kimkakati. Tuko tayari kuwasaidia wawekezaji katika eneo hili,” amesema.
Amebainisha kuwa mazingira ya uwekezaji yameboreshwa kutokana na uthabiti wa viashiria vya uchumi, mageuzi ya kisheria kupitia Mpango wa Mageuzi ya Udhibiti (Blueprint) pamoja na sera za kifedha zinazoeleweka.
“Mfumuko wa bei, kodi na viwango vya riba vimebaki kuwa thabiti na serikali imejizatiti kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanabaki kuwa ya kueleweka na ya kuvutia,” ameongeza Dk Wanga.
Licha ya uhusiano wa kidiplomasia wa zaidi ya miaka hamsini, biashara kati ya Tanzania na Urusi bado ni ndogo.
Uagizaji wa bidhaa kutoka Urusi umefikia wastani wa dola bilioni 2.26 (Sh5.93 trilioni) kwa mwaka, zikiwemo ngano, kemikali, mashine, na maji ya chupa, wakati mauzo ya Tanzania kwenda Urusi yanasimama kwenye dola milioni 5.8 pekee.
“Tunahitaji kuongeza kiwango cha biashara kati ya nchi hizi. Kuna fursa nyingi bado hazijagunduliwa, na Tanzania imejizatiti kuzichunguza na kuzitumia,” amesema.
Sekta nyingine zilizotajwa kuwa na fursa kwa wawekezaji wa Urusi ni pamoja na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, uchakataji wa viwandani na utalii.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Urusi nchini Tanzania, Nikita Rassokhih amependekeza Siku ya Urusi iwe sehemu ya kudumu katika Maonesho ya Sabasaba, akisisitiza umuhimu wake katika kuimarisha majadiliano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili.
“Maadhimisho haya yanawakutanisha wafanyabiashara wa mataifa haya mawili. Urusi iko tayari pia kuunga mkono Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050,” amesema.
Kwa upande wake Lulu Mkude kutoka TanTrade ameeleza kuwa taasisi hiyo itaendelea kuunga mkono ushirikiano wa kimataifa na juhudi za kuvutia wawekezaji.