Mwanafunzi Rucu afariki dunia akidaiwa kubakwa na watu wasiojulikana

Muktasari:
- Mwanafunzi huyo alikuwa anasoma mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu Ruco kilichopo mkoani Iringa.
Iringa. Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu Rucu mkoani Iringa, Rachel Mkubwa amefariki dunia kwa kile kilichodaiwa kubakwa hadi kufa na watu wasiojulikana.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Desemba 12 katika Mtaa wa Mhimba B, Kata ya Makorongoni Manispaa ya Iringa.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Diwani wa Kata hiyo, Thadeus John amethibitisha kutokea kwa kifo hicho huku akisema mpaka sasa wanasubiri taarifa rasmi za Jeshi la Polisi kuhusiana na tukio hilo.
Diwani huyo amesema wiki iliyopita katika eneo hilo mwili wa kijana mmoja nao uliokotwa mtaroni akiwa amefariki dunia, huku amefungwa kamba.
“Hali hii imeanza kuibua hofu kwa wakazi wa mtaa huu na kifo cha huyu mwanafunzi, tunaishi na wanafunzi wengi mtaani sasa mambo kama haya yakianza kuibuka, yanazua hofu kubwa,” amesema diwani John.
Amesema taarifa alizopata kutoka kwa mwanafunzi mwenzake aliyekuwa karibu naye enzi za uhai wake, inaeleza kabla ya kukutwa na umauti, waliachana saa mbili usiku na kila mmoja akaenda kwake kulala.
“Lakini mwenzake anasema alishtuka usiku wa manane na kukuta laptop na simu mbili hazipo akahisi huenda ni rafiki yake (marehemu) amechukua vifaa hivyo, akaenda kumgongea akakuta mlango uko wazi na amelala kifudifudi akiwa uchi ameshakufa, akamuita jirani yake wakamsitili,” amesimulia diwani huyo.
Amesema kutokana na mauaji hayo, kesho Ijumaa ameandaa mkutano wa ajenda moja ya kujadili hali ya ulinzi kwenye mitaa ya kata hiyo.
Mwenyekiti wa Mtaa Kaguo ambao ni jirani na tukio lilipotokea, Alibin Sungura amesema baada ya kumalizika kwa uchaguzi, kwa sasa wanaanza rasmi majukumu na kipaumbele cha kwanza ni kuimarisha vikundi vya ulinzi na usalama.
"Tukio hili ni kama la tatu, tulikuwa na jukumu la uchaguzi sasa tunarejea rasmi kazini na zaidi ni kuimarisha makundi ya ulinzi na usalama katika mtaa huu," amesema Sungura.