Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwanafunzi alivyookolewa kuozeshwa na ng'ombe 15

Muktasari:

  • Operesheni ya kuvunja ndoa hiyo ilifanyika baada ya kubainika kuwa mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 19, ambaye amechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano, alikuwa ameozeshwa.

Maswa. Wakati Tanzania ikiendelea kupambana na tatizo la ndoa za utotoni, mamlaka wilayani Maswa mkoani Simiyu zimefanikiwa kumuokoa mwanafunzi aliyekuwa amechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano baada ya kuozeshwa kwa mahari ya ng’ombe 15, hatua iliyozuia ndoto zake za kuendelea na elimu.

Kwa mujibu wa Utafiti wa Afya na Viashiria vya Demografia Tanzania (TDHS 2022), asilimia 22 ya wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 24 walikuwa wameolewa au kuishi kwenye ndoa kabla ya kutimiza miaka 18, hali inayoonyesha kuwa licha ya juhudi za Serikali na wadau, ndoa za utotoni bado ni changamoto katika baadhi ya maeneo nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vincent Naano, amesema operesheni ya kuvunja ndoa hiyo ilifanyika baada ya kubainika kuwa mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 19, ambaye amechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari Nyalanja wilayani Meatu, alifungishwa ndoa ya kimila Julai 19, 2026 katika Kijiji cha Mwamashindike, Kata ya Budekwa.

Akizungumza Julai 23, 2026, Dk Naano amesema Jeshi la Polisi limewakamata wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo, akiwemo aliyekuwa akimuoa mwanafunzi huyo, Mahene Kulwa, baba mzazi wa binti huyo, Shilinde Ntegwa, dada yake Felister Kulwa pamoja na washenga waliodaiwa kushiriki kufanikisha ndoa hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano akifungua kongamano la vijana katika wilaya hiyo. Picha na Samwel Mwanga

Amesema uchunguzi umebaini mwanafunzi huyo aliolewa baada ya makubaliano ya mahari ya ng’ombe 15, licha ya kuwa tayari alikuwa amechaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari.

Akizungumza mbele ya viongozi wa Serikali, Mahene amesema kabla ya kufunga ndoa alimuuliza mwanafunzi huyo kuhusu masomo yake na akaambiwa hana uhakika wa kuendelea na Kidato cha Tano.

"Aliniambia amemaliza shule na hana uhakika kama atafaulu na kuendelea na masomo. Nikawashirikisha wazazi wangu, wakazungumza na baba yake, wakakubaliana mahari ya ng’ombe 15 ndipo tukafunga ndoa ya kimila," amesema.

Amesema siku ya harusi mwanafunzi huyo hakuwa katika hali nzuri kiafya, hivyo dada yake, Felister Kulwa, alivaa mavazi ya harusi na kukaa nafasi ya bibi harusi ili kuficha utambulisho wake.

Kwa upande wake, baba wa mwanafunzi huyo, Shilinde Ntegwa, amekiri kumuozesha mtoto wake akidai alielezwa kuwa hataki kuendelea na masomo.

"Nilimuuliza kuhusu shule, akasema hataki kuendelea na masomo. Lakini sasa ni lazima aende shule," amesema.

Hata hivyo, baada ya kuhojiwa na Mkuu wa Wilaya, mwanafunzi huyo amesema yuko tayari kurejea shuleni na kuendelea na masomo ikiwa atapatiwa nafasi hiyo.

Dk Naano amesema Serikali itahakikisha mwanafunzi huyo anarudi shuleni ili aendelee kutimiza ndoto zake za elimu, huku akitoa onyo kwa wazazi wanaowakatisha watoto wa kike masomo kwa kisingizio cha mila na desturi.

"Inashangaza kuona walijua ni mwanafunzi, wakaamua kumweka dada yake avae mavazi ya harusi ili watu wasitambue. Tunawapongeza Jeshi la Polisi kwa kushiriki operesheni hii na kuwakamata wote waliohusika," amesema.

Amesisitiza kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya mtoto na taifa, hivyo wazazi na jamii wanapaswa kuacha vitendo vinavyowanyima watoto wa kike haki yao ya kupata elimu.