Mwanafunzi adaiwa kubakwa, kulawitiwa, kuuawa na kutobolewa macho

Baadhi ya wakazi wa Kata ya Galapo wilayani Babati mkoani Manyara, wakiwa kwenye tukio la mwanafunzi wa shule ya msingi Ayatsea kijiji cha Gidemar aliyeuawa baada ya kubakwa, kulawitiwa na kutobolewa macho.
Muktasari:
- Msichana huyo mwenye umri wa miaka 13 aliyekuwa anasoma darasa la sita Shule ya Msingi Ayatsea Kijiji cha Gidemar kata ya Galapo wilayani Babati mkoani Manyara anadaiwa kubakwa kwenye shamba la mbaazi na kisha kuuawa kabla ya kutobolewa macho.
Babati. Mwanafunzi wa darasa la sita mwenye umri wa miaka 13 katika Shule ya Msingi Ayatsea, iliyopo kijiji cha Gedamar, Kata ya Galapo wilayani Babati mkoani Manyara, amefariki dunia baada ya kufanyiwa ukatili unaodaiwa kuhusisha kubakwa, kulawitiwa na kutobolewa macho.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Mei 5, 2025, mkazi mmoja wa Kata ya Galapo, Ezron amesema msichana huyo hakuonekana nyumbani kwao tangu Aprili 29, 2025 baada ya kutoka shuleni.
Ngaida amesema wazazi, wananchi, walimu na wanafunzi wenzake walishiriki kumtafuta, Mei Mosi waliukuta mwili wake umeharibika kwenye shamba la mbaazi.
"Hata hivyo uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa mwili huo ulivunjwa shingo na kutobolewa macho na sehemu za siri kwa kutumia kitu chenye ncha kali," amedai Ngaida.
Mwananchi imezungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani aliyethibitisha kutokea kwa tukio hilo na amesema tayari wanamshikilia mtu mmoja anayedaiwa kuhusika na tukio hilo.
Kamanda Makarani amemtaja mtuhumiwa huyo wanayemshikilia kuwa ni Elias Daniel (26) mkazi wa Wilaya ya Babati.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na wakikamilisha, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Naye mama wa binti huyo aliomba asitajwe jina, ameiambia Mwananchi kuwa kwa sasa hana cha kuzungumza, anamuachia Mungu.
“Sina cha kusema, tukio hili limenichanganya mimi na familia nzima, akili yangu imechanganyikiwa,” amesema mama huyo huku akibubujikwa na machozi.
Mwalimu wa ushauri nasihi wa Shule ya Msingi Ayatsea, Endael Mbwambo akizungumzia tukio hilo, amesema limewaumiza sana walimu na wanafunzi wote.
Amesema siku ya tukio, mwanafunzi huyo alihudhuria vipindi vya masomo hadi saa 10:20 jioni waliporuhusiwa kwenda nyumbani.
“Tulipokea taarifa kutoka kwa wazazi kuwa mtoto wao hakuwa amerudi nyumbani, hivyo walimu tukajiunga katika jitihada za kumtafuta. Hatimaye, mwili wake ulipatikana mashambani akiwa amefariki dunia kwa kufanyiwa ukatili wa kusikitisha,” amesema Mbwambo.
Mwanafunzi mwenzake, Elizabeth John amesema marehemu alikuwa mpole, mwenye upendo na alikuwa anashirikiana vizuri na wenzake katika masomo na michezo.
“Siku ya tukio tuliagana naye vizuri. Hatuelewi kwa nini mtu afanye ukatili wa namna hii. Tunaomba sheria ichukue mkondo wake,” amesema Elizabeth.
Mkazi mwingine wa Babati, Samwel Dahaye amesema matukio kama hayo yanachafua taswira ya mkoa huo na kuongeza kuwa jamii inapaswa kuomba msaada wa Mungu, pia kuongeza jitihada za kuwalinda watoto na matukio mbaya dhidi yao.
Kwa upande wake, Katibu wa Hamasa wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Simanjiro, Matei Damas ameeleza kusikitishwa kwake na ongezeko la matukio ya ukatili, akihimiza jamii kujitafakari na kumrudia Mungu.
“Hivi ndugu zangu, mfahamu kuwa Mungu aliangamiza Sodoma na Gomora kwa maovu kama haya? Tunapaswa kutubu na kujitathmini kama jamii,” amesema Damas.