Prime
Mvutano upungufu wa dizeli, petroli

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mamlaka ya Huduma za Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kuzionya kampuni zinazohodhi mafuta kuacha, Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (Taomac), kimedai hakuna kampuni iliyohodhi nishati hiyo.
Wakati Taomac wakikanusha madai hayo, Taasisi ya Wafanyabiashara wa Mafuta ya Rejareja Tanzania (Tapsoa), imesema hadi Ewura inajitokeza hadharani kueleza jambo hilo, kuna ukweli, huku wakitoa rai kwa wahusika kuacha kuhodhi mafuta.
Juzi, Ewura ilitoa taarifa kwa umma ikizionya kampuni hizo, ikisema ni kinyume cha sheria na kanuni zinazosimamia biashara ya petroli nchini na masharti ya leseni zao za biashara.
Hata hivyo, taasisi hiyo iliwatoa hofu wananchi baada ya kupokea taarifa ya kuchelewa kufikishwa mafuta katika baadhi ya maeneo ya pembezoni mwa nchi na miji, ikisema mafuta yapo.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Taomac, Raphael Mgaya alisema kwa mujibu wa chama chao mafuta yanayotumika mwezi huu ni pungufu, kutokana na uhaba wa dola za Marekani.
“Mei kampuni zilipunguza uagizaji wa mafuta, yale yaliyoagizwa mwezi huo ndiyo yanayotumika hivi sasa. Hali inayoonekana kwenye soko kuna sehemu mafuta hayafiki… yamepungua,” alisema Mgaya.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti dada la The Citizen, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta wa pamoja (PBPA), Erasto Mulokozi alisema hakuna uhaba wa mafuta, nishati hiyo ipo ya kutosha.
Hata hivyo, Mgaya alidai kuwa, Ewura wanatafuta kisingizio, lakini Taomac ilishatoa tahadhari mapema kuhusu hali iliyopo hivi sasa ya uhaba wa upatikanaji wa mafuta kujitokeza.
Alisema kuanzia Januari walitoa tahadhari wa Ewura na mamlaka nyingine.
“Tuliwaambia tunashindwa kupata dola ili kuagiza mzigo wa kutosha, hali itakayosababisha uhaba wa mafuta. Sasa Ewura wanatafuta mchawi, tatizo ni dola na hakuna mtu anayehodhi kusubiri bei kupanda,” alisema Mgaya.
Katibu wa Tapsoa, Augustino Mmasi alisema, “hizi taarifa za Ewura zina ukweli kwa kuwa yeye ni msimamizi wa mafuta yote yanayoingia nchini, kuanzia upokeaji hadi kuuzwa.
“Ewura ina taarifa za upokeaji wa mafuta kutoka kwenye maghala, lakini yanakokwenda ndio changamoto. Maana yake ukweli upo, Ewura haiwezi kusema jambo lisilokuwa na ukweli, naamini wapo sahihi.”
Mmasi alisema athari za suala hilo, baadhi ya maeneo yatakuwa na uhaba wa mafuta nchini, hasa sehemu za vijijini, ikiwamo Loliondo (Arusha), Kilindi (Tanga) Kateshi na Kiteto (Manyara).
Alisema kinachotakiwa ni ushirikiano wa mawasiliano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kufikisha mafuta kwenye uhaba.
“Tunatoa wito kama kuna wafanyabiashara wakubwa wamehodhi waache, maana yake wafanyabiashara wadogo hatutapata nishati hii kupeleka maeneo ya vijijini. Pia, hata wafanyabiashara wadogo waache, hasa wenye vituo vya mafuta vidogo,” alisema Mmasi.
Kwa mujibu wa Ewura, zipo kampuni za mafuta zinazosemekana kupakia mafuta kutoka kwenye maghala pasipo kuyauza na nyingine kukataa kuuza kwa wamiliki wa vituo wasio kuwa na ubia au mikataba nao.
“Ewura inapenda kuwajulisha wananchi wote kuwa, nchi ina mafuta ya kutosha katika maghala na meli zenye shehena ya mafuta kutoka nje ya nchi zinaendelea kuingia na kushusha kama kawaida chini ya uratibu wa PBPA,” inaeleza taarifa ya Ewura.
Hata hivyo, mamlaka hiyo inaendelea kufanya ukaguzi kwenye maghala na vituo vya mafuta na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wote watakaothibitika kukiuka sheria, kanuni na masharti ya leseni zao, ikiwamo kuwanyang’anya leseni kwa mujibu wa Kanuni Namba 6 ya Kanuni Ndogo za Ukokotoaji wa Bei za Mafuta GN. 57 ya mwaka 2022.