Mvua ya upepo yaezua nyumba, kujeruhi watoto wawili Katavi

Muktasari:
Mvua iliyoambatana na upepo mkali imeezua nyumba 31 na kubomoa kuta zake katika Kijiji cha Tukoma, Kata ya Itenka Halmashauri ya Nsimbo huku baadhi ya familia zikikosa makazi.
Katavi. Mvua iliyoambatana na upepo mkali imeezua nyumba 31 na kubomoa kuta zake katika Kijiji cha Tukoma, Kata ya Itenka Halmashauri ya Nsimbo huku baadhi ya familia zikikosa makazi.
Akitoa taarifa mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Mpanda, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Itenka, Yegela Samike amesema mvua hiyo imenyesha Novemba 9, 2022 saa 12:45 jioni.
Samike amesema pamoja na nyumba kuezuliwa na kubomoka, watoto wawili walijeruhiwa baada ya kupondwa na tofali na hali zao zinaendelea vizuri.
"Tulipita kwenye kaya 24 tumebaini nyumba 31 zimeezuliwa na baadhi zimebomoka lakini kuku na bata idadi yake haijafahamika wamefunikwa na vifusi," amesema Yegela.
Kwa upande wao waathiriwa wa tukio hilo Agnes John na Daudi Pius wameiomba serikali kuwasaidia wapate sehemu ya kujisitiri wakati wakirebisha nyumba zao.
"Nina watoto wanne nimeachwa nje naomba serikali inisaidie nitaishi wapi na fedha ya kurekebisha sina nihurumieni," wamema waathiriwa.
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuph akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama ametoa pole kwa waathirika na kuahidi kuwa serikali akiwasihi kubadili mfumo wa ujenzi wa nyumba zao.
"Tutafanya tathmini kubaini athari zilizosababishwa na tukio hilo ili kuona namna ya kusaidia lakini boresheni makazi yenu," amesema Jamila.
Tukio hili ni la kwanza kutokea tangu mvua msimu wa kilimo 2022/2023 uzinduliwe mkoani Katavi.