Mvua Siha zaleta msiba, mwili wa mwanamke wapatikana

Muktasari:
- Mwanamke huyo pamoja na mwenzake wanadaiwa kupotea November 22, 2023 wakidaiwa kuchukuliwa na maji ya Mto Biriri, wakati wakitokea Soko la Makiwaru kununua mahitaji ya nyumbani.
Siha. Wananchi wa Kata Songu Kijiji cha Ndumbaru, wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro wamefanikiwa kupata moja ya miili ya wanawake wawili wanaosadikiwa kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazonyesha wilayani hapa.
Wanawake hao Eliakesia Akyoo (61) na Eliakesia Elisante (55) wanadaiwa kupotea November 22, 2023 kwa madai ya kusombwa na maji ya Mto Biriri, wakati wakitokea Soko la Makiwaru kununua mahitaji ya nyumbani.
Mkuu wa Wilaya ya Siha, Christopher Timbuka amethibisha kutokea kwa jambo hilo na mmoja wa wanawake hao amepatika na wanaendelea kumtafuta mwingine.
Aidha, DC Timbuka amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ikiwamo kuchimba mitaro hasa kwenye nyumba zilizozingirwa na maji ili kuyapa njia ya kupita.
Akizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Issaya Mkilindi amesema kuwa wanaendelea na shughuli ya kumtafuta mama huto wakipita pembezoni mwa mto huo na maeneo mengine.
“Siku ya Jumatano, wanawake hao walikwenda Soko la Makiwaru kwa ajili ya kupata mahitaji, lakini wakati wanarejea makwao, hatujui nini kimewapata lakini tunahisi kutokana na mvua kuendelea kunyesha, walikuta mto umefurika maji hivyo kusabisha kubebwa na maji,” amesema na kuongeza;
“Mmoja wa wakina mama hao ilikuwa afanye ubarikio wa mtoto wake jana Novemba 24,2023. Tunaendelea kumtafuta,”amesema Mkilindi.