Muswada wa bima ya afya kwa wote kutua Bungeni kesho

Muktasari:
- Baada ya kukwama mara mbili kujadiliwa katika Bunge la Tanzania, Muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote unatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili kesho Bungeni, ambapo Serikali kupitia Wizara ya Afya itaainisha yale marekebisho ambayo wabunge waliyahitaji.
Dar es Salaam. Muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote, unatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili kesho katika Bunge la Tanzania.
Serikali kupitia Wizara ya Afya inatarajiwa kuusoma tena baada ya kukwama Februari mwaka huu kwa hoja iliyotolewa na Bunge ya kutokuwepo kwa chanzo endelevu cha fedha kutekeleza mpango huo.
Akizungumza leo Jumanne, Oktoba 31, 2023 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Afya, Englibert Kayombo amesema muswada huo ni ndoto ya Serikali ya miaka mingi.
Amesema Serikali ya awamu ya sita imeboresha huduma za afya kuanzia ngazi ya Taifa hadi ya msingi kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya karibu zaidi na maeneo yao.
“Serikali kupitia Wizara ya Afya, wadau wa sekta na wataalam wengine tayari wamefanyia kazi hoja zote zilizoibuliwa na Bunge pamoja na wadau, hata hivyo semina zimefanyika kwa makundi mbalimbali ndani ya jamii kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa wote.
“Tulipokea maoni yao na kuyafanyia kazi wananchi kesho watege macho na masikio yao Bungeni kujua nini ambacho Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu atawasilisha,” amesema
Amesema kupitishwa kwa muswada huo kutawezesha kila Mtanzania kuwa ndani ya mfumo wa bima ya afya hatua itakayoboresha zaidi upatikanaji wa huduma za matibabu bila kuwa na kikwazo cha fedha.
“Serikali yetu ni sikivu na imefanyia kazi hoja zote zilizoibuliwa na Wabunge ambao ndio wawakilishi wa wananchi hivyo yaliyomo ndani ya muswada huo yamelenga kuwasaidia wananchi kupata huduma bora za afya bila ya kikwazo cha fedha,” amesema Kayombo.
Kuhusu gharama za vifurushi, Kayombo amesema kuwa mara baada ya Muswada huo kupita na kuwa sheria, kanuni zitatungwa ili kuratibu suala ya gharama za vifurushi na kusema kuwa uchambuzi utafanyika ili vifurushi viwe vya gharama nafuu na kila mwananchi aweze kuwa na bima ya afya.
Ameongeza kuwa kwa upande wa Serikali imeshakamilisha maandalizi ya kutoa huduma kwa wananchi kupitia mfumo wa bima ya afya kwa wote ambapo imeboresha ubora wa huduma katika vituo vyake vya kutolea huduma ikiwemo upatikanaji wa dawa, ununuzi na usimikaji wa vifaa na vifaa tiba na ajira za watumishi.
“Kwa sasa nchi yetu iko mbali sana katika utoaji wa huduma, tuna vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa, huduma nyingi za kibingwa zinapatikana hapa hapa nchini lakini pia huduma za afya zimesogezwa sana kwa wananchi hivyo kama nchi tupo tayari kutekeleza hili, nia na uwezo wa kufanya hivyo tunao,” amesema Kayombo.