Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mususa: Wananchi washirikishwe kukabili mabadiliko ya tabianchi

Mwenyekiti wa Bodi ya Mwananchi Communication Limited, Leonard Mususa

Muktasari:

  • Wadau wametaka wananchi kushirikishwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa mafanikio katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yatafikiwa iwapo Serikali itawashirikisha wananchi wote kwenye juhudi hizo.

Hayo yameelezwa leo alhamisi Juni 1, 2023 na Mwenyekiti wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Leonard Mususa alipohutubia Kongamano la Jukwaa la Fikra lililofanyika jijini hapa.

Ametolea mfano taifa la Coastarica lililofanikiwa kukabiliana na janga hilo kupitia kuwashirikisha wananchi wote.

"Serikali haiwezi kufanikiwa katika mipango bila mipango hiyo kufika hadi chini, kila mwananchi lazima awe na malengo ya kuyatimiza ili kupunguza mabadiliko ya tabianchi," amesema.

Hata hivyo, amesema mjadala huo ni muafaka kwa kuwa unafanyika kipindi ambacho ni mwaka mmoja umepita tangu dunia ifanye mkutano wa kujadili athari za mabadiliko ya tabianchi (COP27).

Katika mkutano huo, Mususa amesema maazimio mbalimbali yamefikiwa ikiwemo uanzishwaji wa mfuko wa kurejeleza athari zilizoyakumba mataifa yanayoendelea (Loss and Damage Fund).

"Maazimio yamefikiwa lakini sisi kama wananchi na wadau tuna nafasi ya kuhakikisha tunakuwa na malengo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi," ameeleza.

Kwa mujibu wa Mususa, Serikali kwa sehemu yake imefanya mambo kadhaa kufanikisha hilo, ikiwemo kuhifadhi maeneo ya misitu mita za mraba 361,000.

Mipango mingine aliyoitaja ni upandaji wa miti milioni 1.5 kila wilaya kwa kila mwaka, kadhalika kuanzisha sera ya uwekezaji katika nishati mbadala.

Mususa ametaja mpango mwingine uliofanywa na Serikali ni kuanzisha kampeni kubwa ya kupunguza matumizi ya nishati ya mkaa.

Akizungumzia jukwaa la fikra, amesema ni programu inayofanyika kwa kukutanisha wadau ikilenga kujadili mambo mbalimbali.

Kinachozungumzwa si changamoto pekee, amesema ni kusaka suluhu ya changamoto mbalimbali.

"Ingawa tunazungumza kuhusu changamoto, lakini tumejikita zaidi katika kutafuta suluhu ya matatizo mbalimbali ndiyo maana leo hii tumewakutanisha wote," ameeleza.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu amesema kazi kubwa ya kampuni hiyo ni kuhakikisha watu wanapata taarifa sahihi.

Amesema taarifa hizo zinalenga kuwaelimisha ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi.

"Magazeti ni njia tu tunayoitumia kumbe tukitumia mijadala mbalimbali tukawapa watu wasaa wa kujadili kwa pamoja tunatimiza wajibu ule ule wa kuwapa watu maarifa," amesema.

Hata hivyo, amesema ulimwengu wa sasa wa taaluma ya habari umebadilika na kuzaa kitu kinachojulikana kama uandishi wa habari wa matukio (Event Journalism) na hicho ndicho kinachofanywa na MCL.

Kinachofanyika, amesema kinalenga kuzungumza mambo yatakayosaidia kupata ufumbuzi.

Kwa sababu ni chombo cha habari, ameeleza kazi kubwa itakayofanywa ni kusambaza taarifa kupitia mitandao, magazeti na vyanzo vingine kuuhabarisha umma.