Hivi ndivyo Tanzania inavyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi
Mhandisi wa Viwanda Ofisi ya Makamu wa Rais, Julius Enock
Muktasari:
- Umekuwa ukisikia mabadiliko ya tabianchi yanaitwa janga, ukubwa wa athari zake, unaakisi hilo.
Dar es Salaam. Pengine tunasikia tu kwamba mabadiliko ya tabianchi ni janga na isieleweke kwanini yanaitwa hivyo, lakini ukubwa wa athari zake unaakisi hilo.
Hivi unafahamu kwamba mabadiliko ya tabianchi yanasababisha hasara ya Sh3 trilioni hadi Sh5 trilioni kwa mwaka?
Hasara hiyo ni sawa na asilimia 40 ya bajeti ya Serikali kwa mwaka kwa mujibu wa Mhadhisi Viwanda, Ofisi ya Makamu wa Rais, Julius Enock.
Hayo yamebainishwa leo, Alhamisi ya Juni 1, 2023 na Mhandisi Enock alipotoa mada katika Jukwaa la Fikra, akimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jaffo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Enock, mabadiliko ya tabianchi pia yanaathiri sekta mbalimbali ikiwemo kilimo kinachotegemewa na sehemu kubwa ya Watanzania.
Athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya kilimo, Mhandisi Enock amesema hugharimu Serikali Sh1.3 trilioni kwa mwaka.
Gharama hizo zinatokana na kile alichokifafanua ni mafuriko, ukame na kuongezeka kwa magonjwa ya mazao.
"Ni janga kubwa kwenye sekta hii ambayo uchumi wetu unaitegemea," amesema.
Si kilimo pekee, mabadiliko ya tabianchi huathiri sekta ya afya pia, inaelezwa na Mhandisi Enock.
Katika sekta hiyo, amesema mabadiliko hayo husababisha kuinuka kwa magonjwa ambayo kiasili hayakuwepo.
Hata hivyo, amesema Tanzania ni nchi ya 26 Iliyo katika hatari ya kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.
Hali hiyo inatokana na kile alichoeleza kuwa, sehemu kubwa ya sekta za uchumi nchini zinafungamana na mazingira.