Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mume adaiwa kuua mke, kumzika ndani ya nyumba

Madaktari na maafisa afya wilaya ya Kilosa wakivaa mavazi rasmi Kwa ajili ya kuanza kazi ya kufukua mwili wa mwanamke mmoja anayedaiwa kuuawa na mume wake kisha kufukiwa kwenye shimo chini ya kitanda nyumbani kwake. Picha Johnson James

Muktasari:

  • Mtoto wa marehemu aeleza walikuwa wakiishi maisha magumu na yaliongezeka baada ya mama yao kufariki dunia.

Kilosa. Utu umekwisha umebakia unyama. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na simulizi ya kusikitisha ya tukio la mauaji ya Beatrice Ngongolwa yanayodaiwa kufanywa na mumewe, Mohamed Salanga (37), kisha kuufukia mwili wake chini ya kitanda ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi.

Mauaji ya Beatrice (32), mkazi wa Sekutari, Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro yanadaiwa kutokea usiku wa Desemba 31 mwaka jana na mazishi yake kufanyika Januari mosi, 2024.

Leo, Machi 22, 2024, kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Kilosa ikiongozwa na mwenyekiti wake, Shaka Hamdu Shaka ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo iliongoza shughuli ya kuufukua mwili wa Beatrice na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro baada ya siri hiyo kufichuka.

Hatua hiyo ya kamati ya ulinzi na usalama ilikuja baada ya Salanga kuwaonyesha alipomzika mkewe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema wanamshikiliwa Salanga, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Kudewa kwa tuhuma za kumuua mke wake.

Alisema wamemkamata jana Machi 21, 2024 baada ya mke wake kutoonekana kwa muda mrefu, amedai mtuhumiwa alikiri kumuua mke wake na kumzika ndani ya nyumba.

Amesema baada ya taratibu kukamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.


DC aelezea tukio hilo

Akizungumzia tukio hilo, DC Shaka amesema jana Machi 21, saa 6 mchana walipokea taarifa kutoka kwa raia wema wakieleza juu ya tukio hilo.

“Watu wema walitupigia na kutueleza juu ya mama mmoja kufariki dunia kutokana na kipigo kinachodhaniwa kufanywa na mpenzi wake, kwa taarifa za awali zinaeleza tukio lilitokea Januari 1, 2024,” amesema Shaka.

Amesema wawili hao walikuwa wakiishi tarafa ya Kimamba A, Kitongoji cha Skutari wakiwa na watoto watatu akiwamo wa kike mwenye miaka 11 na wawili wa kiume wa miaka tisa na minne. Hata hivyo, watoto hao inadaiwa si wa mtuhumiwa huyo.

"Tumebaini marehemu alikuwa akiishi maisha magumu na yenye ukatili mbele ya huyu mtuhumiwa, kwani taarifa zinaeleza ukatili ulikuwa mkubwa kwa mkewe na watoto wake walifungiwa ndani muda wote bila kupata haki na fursa za msingi kama watoto.”

“Watoto hawa walikuwa hawaendi shule, tumemkagua mtoto wa kiume tumeona hana meno, tulipomuuliza akasema baba huwa anatugonga vyuma mdomoni ndiyo maana meno yametoka,” amesema Shaka.

Katika maelezo yake baada ya kushuhudia shughuli ya kuufukua mwili, Shaka amesema: “Nimemkagua mmoja wa watoto nikaona mdomo nao umechanika, nilipomuuliza akasema baba yake huyo wa kambo alimpasua baada ya kumlazimisha afanye mapenzi na wenziwe, alipokataa ndipo akampiga. Kiufupi chanzo cha haya mauaji ni ukatili ambao huyu mtuhumiwa alikuwa nao."


Simulizi ya tukio lilivyotokea

Moja ya vyanzo vya Jeshi la Polisi kilichozungumza kwa sharti la kutotajwa jina, kimesimulia maelezo yaliyotolewa na mmoja wa watoto wa marehemu aliyeeleza walikuwa wakiishi maisha magumu na yaliongezeka baada ya mama yao kufariki dunia.

“Maisha yetu hapa nyumbani yalikuwa ya tabu sana kwa kuwa baba yetu huyu wa kambo alitufungia ndani muda wote, hakutaka tutoke nje, tulipotoka tuliishia kukaa kwenye uzio wa nyumba na hatukuruhusiwa kutoka kabisa,” anamnuku mtoto huyo.

Chanzo hicho kimedai, wazazi hao walikuwa wakitoka nyumbani kwenda kwenye majukumu yao waliwaacha kwa kuwafungia ndani mpaka waliporudi, ndipo walikuwa wanawafungulia.

“Taarifa zinaeleza, mama huyo alipigwa usiku wa Desemba 31 mwaka jana, wakati anampiga aliwafungia watoto hao ndani, akaanza kumpiga mama, alimpiga akampasua kichwa kisha akamuacha.

Baada ya kumuacha walimsikia baba yao wa kambo akimwambia mama yao  "Kwa nilivyokupiga hivi utapona kweli, mwanamke huyo akajibu ‘niue lakini nilele watoto wangu’ kisha hawakusikia tena akiongea.

Inadaiwa baada ya kufariki dunia, mtuhumiwa huyo alichimba shimo chumbani na kumzika marehemu kisha akamfuata mtoto mkubwa na kumweleza asiseme kitu na iwapo atafanya hivyo angemuua.

Chanzo chetu kimeendelea kudai, baada ya mama huyo kufariki dunia watoto hao waliendelea kuishi kwa mateso na ilifikia hatua akamng’oa meno mtoto mmoja kwa kumpiga na chuma mdomoni.

Amesema mtuhumiwa huyo alikuwa akiwanyima chakula watoto hao na pindi walipokuwa wakiomba alidai walikutana na kipigo.

Anamnukuu mtoto huyo akidai, “ilifika wakati nikimkumbuka mama nalia tu, lakini sikuwa na cha kufanya badala yake nilifanya kile ambacho baba alitaka na ilifika mahali nikazoea.”


Salanga aoa mke mwingine

Baada ya kudaiwa kumuua mkewe, mtuhumiwa inaelezwa alimuoa mwaname mwingine ambaye awali waliishi kama wapenzi, anaenda nyumbani hapo na kuondoka.

“Lakini baadaye aliamua kumuoa kabisa, lakini hakutoa mwanya kwa wale watoto kukaa na mama huyo aliyemuoa. Na alipomuoa walilala chumba kilekile walichokuwa wanaishi na mke wa awali,” kinaeleza chanzo chetu.

Inadaiwa baadaye walihamia chumba kingine na chumba walichokuwa wakiishia walikigeuza jiko, juu ya kaburi yaliwekwa mafiga ya kupikia.

Taarifa zinadai, majirani walipokuwa wakimuuliza Salanga (mtuhumiwa) alipo mke wake, aliwajibu ametoroka na hata mwanamke aliyemuoa aliamini hivyo.

Kujulikana kwa taarifa hizo ni baada ya mtuhumiwa kudaiwa kuuza mabati ya huyo mke mpya ambayo aliyanunua na kuyapeleka nyumbani kwa ajili ya kujenga. Mwanamke huyo hakukubali na inaelezwa akapeleka suala hilo mahakamani.

“Baada ya kuwa ameenda mahakamani akamshtaki huyu baba yetu kuwa ameuza bati zake, baba akawa anahudhuria mahakamani kama kawaida,” anamnukuu mtoto.

Inadaiwa baada ya Salanga kwenda mahakamani, watoto walipata fursa ya kuzungumza na mama yao wa kambo na walichomweleza ni kuwa makini kutomchokoza baba yao, kwani anaweza kumfanya kama alivyomfanya mama yao.

“Unaambiwa yule mama akashtuka. Akawauliza ilikuwaje, wakamsimulia kila kitu ikiwemo alipozikwa mwanamke huyo. Nasikia huyo mwanamke akaogopa na kukimbia kutoa taarifa Polisi,” kinaeleza chanzo chetu.

Taarifa zinaeleza, baadaye alihama kijijini hapo na kwenda kuishi kijiji kingine cha Ludewa Batini takribani kilomita 20 kutoka alipokuwa akiishi awali.


Walichosema majirani

Gazeti hili lilizungumza na majirani wa Salanga ambapo Hidaya Mashaka amesema binafsi alikuwa akiwaona wapo pamoja muda wote.

“Mimi kwa kweli hawa walikuwa majirani zangu hapa na niliwaona wakipita wakienda sentani (center) na mara nyingi walipita na kunisalimia na kuondoka na ile familia hawakuwa watu wa kujichanganya sana na watu."

"Maana wao walikuwa wanakaa tu nyumbani kwao na hata watoto wao hawakutoka ndani kucheza na wenzao kwa majirani, walifungiwa tu ndani walipotoka waliishia kwenye uzio tu,” amesema na kuongeza;

“Nilikuwa nasikia wana ugomvi wa mara kwa mara mle ndani, lakini walipokuwa wakitoka nje ulikuwa huwezi kugundua kama kuna chochote kinaendelea,” amesema.

Mwashamu Hussein, rafiki wa marehemu amesema alimfahamu tangu Julai mwaka jana na waliwahi kukutana na kumwomba mwanangu awe dada yake wa hiyari na baadaye wakaenda mpaka nyumbani kwake.

Amesema alipokwenda miongoni mwa mambo aliyomuuliza  mumewe ni kwa nini ameweka uzio, hataki mambo yako yaonekane? Akajibu kwamba amefuga sungura. Sasa mara ya mwisho tulipoongea aliniambia mke wake ameondoka na amechukua Sh700,000.”

“Nikauliza shida nini, nikamwambia ahakikishe mke wake anakuja kulea watoto maana walikuwa watatu na wadogo, nilipomkazania hakunijibu na akaacha kabisa kuja nyumbani kwangu mpaka leo niliposikia kwamba kumbe alimuua mkewe na kumzika ndani,” amesema.

Mwashamu alisema enzi za uhai wake, Beatrice alimweleza walikutana na Salanga bandarini, Unguja visiwani Zanzibar na wakaamua kwenda Kilosa kuishi.

“Lakini siku za karibuni hapa nilibahatika kuwaona wale watoto wake wamedhoofika sana, nilitamani kuwauliza kwani mama hajarudi mpaka sasa, yuko wapi na hamna mawasiliano naye? Kwa hivyo wale watoto walinihuzunisha,” amesema.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sekutali, Mtaa wa Kimamba A, Elbet Haule amesema mara ya mwisho alikutana na mtuhumiwa baada ya kupokea taarifa za wawili hao kugombana.

“Hawa watu binafsi nilikuwa nawafahamu na walikuwa wakiishi kama wananchi wengine lakini walihamia hapa tangu mwaka jana na kwenye pitapita nikapokea taarifa kuna ugomvi kati yake na mkewe, nikaja mpaka hapa, (nyumbani kwa mtuhumiwa alipokuwa amepanga) nikaonana na mtuhumiwa."

"Nikamweleza akae chini na mkewe waache ugomvi wao, akajibu kwamba amenielewa, nikasisitiza mkewe akirudi nyumba anitafute nije kusuluhisha ugomvi wao, tangu wakati huo sikumuona tena huyu mtuhumiwa mpaka napata taarifa hizi,” amesema.