Muhimbili yajipanga kuwapelekea wagonjwa huduma ya dharura nyumbani

Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili (MNH)Profesa Mohamed Janabi akizungumza na Waandishi wa Habari Hospitalini hapo Dar es Salaam
Muktasari:
- Hospitali ya Taifa Muhimbili Idara ya Tiba ya Dharura kwa siku hupokea wagonjwa 150 mpaka 200, matukio ya ajali yakitajwa kuchangia wagonjwa wengi.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Profesa Mohamed Janabi amesema mwelekeo wa hospitali hiyo kupitia idara ya tiba dharura ni kutambua dharura za wagonjwa na kuwafuata kuwahudumia kulingana na matatizo waliyonayo.
"Tunachotaka, tukipigiwa simu na mgonjwa yupo Masaki tutamuuliza nini tatizo, wakituambia shida ni ujauzito tumpelekee gari ambalo akitaka kujifungua aendelee kujifungua, tukiambiwa mgonjwa ameanguka kwa mshtuko wa moyo tupeleke gari lenye vifaa vitakavyowezesha huyo mgonjwa kutibiwa, huu ndio mwelekeo wa hospitali yetu," amesema Profesa Janabi.
Profesa Janabi ametoa kauli hiyo leo Mei 27, 2024 katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Tiba Dharura iliyofanyika hospitalini hapo ikiongozwa na kauli mbiu Mabadiliko ya Tabia ya Nchi na matokeo katika huduma za dharura.
Hatua ya kuwafuata wagonjwa na kuwapa huduma kulingana na mahitaji yao, Profesa Janabi amesema ni uboreshaji wa huduma za dharura ambazo miaka 1990 katika hospitali hiyo huduma hazikuwa nzuri .
Akizungumzia matukio yanayochangia idadi kubwa ya magonjwa ya dharura hospitali hapo, Profesa Janabi ametaja ajali kushika nafasi ya kwanza huku maradhi mengine kama malaria, nimonia na maradhi ya moyo yakifuatia.
Kwa siku moja pekee, Profesa Janabi idara ya magonjwa ya dharura wanapokea wagonjwa 150 hadi 200 asilimia moja pekee ndio wakipoteza maisha.
Hii ni tofauti na hali ilivyo Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila, ambapo wagonjwa kati ya 30 hadi 35 ndio wanaopokelewa na kuhudumiwa, takwimu za jumla zikionyesha kwa mwaka jana pekee hospitali hizo mbili zilihudumia wagonjwa wa dharura 21,000
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) watu milioni 4.4 hupoteza maisha kutokana na ajali duniani hiyo sawa na asilimia ya vifo vyote vinavyotokea duniani.
Pia, Profesa Janabi amesema mara kadhaa wamekuwa wakiulizana na Jeshi la Zimamoto na Ukosoaji kama wanavifaa vya kuzima moto inapozuka kwenye ghorofa refu kwani wao kama wataalamu wa tiba yanapotokea matukio hayo wanasubiri majeruhi chini na sio kuwafuata ghorofani.
"Sisi kama kitengo cha dharura tunawasubiri chini, hivyo tutaendelea kushirikiana na taasisi zingine kuangalia namna tulivyonipanga, ni muhimu haya kuzingatia sasa hivi tusisubiri ajali," amesema Profesa Janabi.
Awali kabla ya maadhimisho hayo, Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kiliandaa tukio la dharura kwa wanafunzi wa chuo hicho kuigiza kupata ajali eneo la ufukwe wa bahari karibu na Hospitali ya Aga Khan.
Katika tukio hilo lililohusisha wanafunzi kujifanya wamepata ajali na kujitupa pembezoni mwa bahari, Idara ya Magonjwa ya Dharura Muhimbili ilijulishwa tukio hilo saa 1:50 asubuhi kuja kutoa msaada lakini walifika saa 2:23 tathmini ya wataalamu ikionyesha wamechelewa eneo la tukio.
Tathmini hiyo ya kitaalamu imetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Dharura Muhas, Dk Said Kilindimo ambaye amesema wataalamu wa dharura kutoka Muhimbili walipaswa kufika eneo la tukio dakika 10 baada ya kupata simu.
"Jaribio tulilolifanya limefanikiwa kwa asilimia 94, hizi asilimia sita ni za kuchelewa na sababu ni foleni, kwa eneo ndani ya kilomita tano kama kuna dharura inapaswa kufika ndani ya dakika 10, tuliwapigia simu saa 1:50 na kufika saa 2:23,"amesema.
Kulingana na jiografia ya Jiji la Dar es Salaam kutoka Hospitali ya Muhimbili hadi Hospitali ya Aga Khan palipotekelezwa tukio hilo la kujipima utayari ni Km 3.1.
Dk Doreen Kamoli mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo cha Muhas, amesema suala la mabadiliko ya tabianchi ni dharura ya kiafya, hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari ya kutunza na kuhifadhi mazingira.
Akilinukuu Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi kufikia 2030 vifo vitokanavyo na mabadiliko ya tabianchi yataongezeka kutoka milioni 250 duniani kufikia vifo 300.