Mufindi watakiwa kutumia mabaki ya mbao kutengeneza samani

Muktasari:
- Balozi Pindi Chana amesema mabaki ambayo kiwanda hicho kinatumia ni kutokana na vipimo maalumu ambavyo ni vipande vidogo vidogo vinavyotumiwa baada ya kuboreshwa kwa ajili ya kutengeneza malighafi zinazoitwa MDF.
Mufindi. Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana amewataka wananchi wa wilaya ya Mufindi mkoani Iringa watumie mabaki yanayotokana na uchakataji wa mazao ya misitu kutengeneza bidhaa nyingine za samani kwa kutumia mabaki hayo.
Balozi Chana ameyasema hayo leo Septemba 17, 2022 wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani hapa na kutembelea kiwanda cha samani na kujionea bidhaa zilizotengenezwa kwa kutumia mabaki hayo.
Amesema mabaki ambayo kiwanda hicho kinatumia ni kutokana na vipimo maalumu ambavyo ni vipande vidogo vidogo vinavyotumiwa baada ya kuboreshwa kwa ajili ya kutengeneza malighafi zinazoitwa MDF.
“Hizi ni malighafi za kisasa ambazo zinatengeneza vitanda, makabati na samani mbalimbali za ndani, haya ndiyo maelekezo ambayo Rais wetu, Samia Suluhu Hassan alikuwa anatuagiza kama wizara hususani kwenye sekta ya misitu, kutengeneza na kusafirisha kwa kutumia malighafi za ndani,” amesema Dk Chana
Kuwa upande wake, mkuu wa wilaya ya Mufindi, Saad Mtambule amesema asilimia 30 hadi 35 ya miti ambayo imekomaa na ina umri wa miaka 18 zilikiwa zinatumika kuzalisha mbao huku asilia 60 hadi 65 zilikuwa zinapotea kwa sababu hazikuweza kuzalisha kitu chochote.
“Tunashukuru Rais Samia kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri kwenye Sekta mbalimbali ikiwemo misitu, hivyo kiwanda hiki kinatengeneza bidhaa kwa kutumia mabanzi na kuziongea thamani kuliko hata mbao ambazo zinazozishwa,” amesema Mtambule.
Mhifadhi mkuu wa shamba la miti la Serikali la Sao Hill, Lucas Sabida amesema kiwanda hicho ni fursa nzuri kwa wananchi wanaozunguka katika shamba hilo kutokana na shughuli mbalimbali ambazo wanazifanya, mabaki mengi huwa yanabaki katika mashamba hayo.
“Kuna rasilimali nyingi ambazo bado hazijafanyiwa kazi kwa ajili ya kutumia matumizi kama haya ya viwandani. Vipande vingi vya miti vimekuwa vikiachwa mashambani kwa sehemu kubwa na ndio imekuwa chanzo cha moto wakati wa kusafisha mashamba haya, hivyo kiwanda hiki ni fursa kwa wananchi kupeleka mabaki hayo,” amesema Sabida.
Mhifadhi huyo amesema baada ya kuona bidhaa zinazotengenezwa katika kiwanda hicho wamegundua kuwa malighafi nyingi walikuwa wanaziacha kwenye mashamba yao ambayo yangetumika kuzalisha bidhaa za MDF.
Sabida amewasisitiza wananchi Wilayani hapa kuendelea kutembelea kiwanda hicho na kuona umuhimu wake ili wasiweze kuacha Malighafi hizo katika Mashamba yao na badala yake wampeleke kwenye kiwanda hicho.
Mfanyakazi wa kiwanda hicho, Edward Wong amesema kuwa kwa sasa soko lao kubwa lipo nchi ya kenya kuliko hapa Nchini lakini wanafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wakiwa na madalali kila maeneo ili kuweza kutangaza bidhaa hizo.
“Tunazalisha bidhaa za MDF ambazo husafirishwa nje ya nchi ambayo ni kenya ndio asilimia kubwa tunauza huko kwa sababu soko la ndani bado ni dogo ukilinganisha na kenya ila kwa sasa tumeanza kuweka madalili katika mikoa ya Arusha,Mwanza pamoja na maeneo mengine kwa ajili ya kutafuta soko,” amesema Wong.
Hata hivyo, viwanda hicho kimeweza kuajiri wafanyakazi 230 ambao wanafanya kazi Katika kiwanda hicho huku uzalishaji wa Bidhaa hizo ukiwa elfu 5,000 kwa siku.