Prime
Mtumishi wa ndani alivyomuua tajiri yake, kuubaka mwili wake

Elizabeth Shayo ambaye ameuawa kwa kukatwa mapanga na mfanyakazi wake.
Muktasari:
- Mshtakiwa asema alikuwa anamdai mshahara tajiri yake, alipomwambia hana akapatwa hasira amkata panga
Moshi. “Nilimfuata chumbani kwake na kumkata panga la kichwani alipodondoka nikamkata lingine chini ya mdomo. Ilipofika usiku saa nane nilimtoa nikamburuza mpaka huko Korongoni. Kabla ya kumtoa nilimbaka na kumburuza hadi porini.”
Hayo ni maneno ya John Mashaka Sigani au Castori aliyekuwa mtumishi wa ndani wa Elizabeth Shayo (63) yaliyomo katika maelezo ya onyo ya kukiri kosa aliyoyaandika polisi.
Katika maelezo hayo, alielezea mwanzo mwisho namna alivyomuua tajiri yake huyo.
Ni kutokana na maelezo yake hayo pamoja na ushahidi mwingine wa mashahidi wa upande wa mashitaka, Jaji Safina Semfukwe wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi, amemhukumu mshitakiwa huyo kunyongwa hadi kufa kwa mauaji hayo.
Mauaji hayo yalitokea Septemba 10, 2021 lakini mwili wa Elizabeth mkazi wa Himo Darajani Wilaya ya Moshi, ulipatikana Septemba 14 pembeni ya Mto Ghona ukiwa umevuliwa nguo za chini kwa maana ya sketi na chupi alizokuwa amevaa.
Muuaji huyo alikamatwa akiwa ndani ya basi la Kampuni ya Shabiby akitoroka kuelekea kwao mkoani Dodoma na alikamatwa baada ya Jeshi la Polisi kupokea taarifa fiche kuwa John alionekana amepanda basi hilo asubuhi ya siku hiyo.
Tukio hilo la mauaji liliibua sintofahamu kubwa kati ya familia na polisi wa mji wa Himo kwa namna walivyokuwa wakipeleleza, hadi Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI), ikatuma timu kuchunguza tukio hilo.
Walichokisema mashahidi
Shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri, Dk Sudi Mohamed wa Kituo cha Afya Himo, ameeleza namna alivyoufanyia uchunguzi mwili wa marehemu jirani na Mto Ghona na kwamba mwili ulishaanza kuoza na tayari ulianza kuliwa na funza.
Kulingana na shahidi huyo, mwili huo ulikuwa na mikwaruzo kwenye kiuno na ulikuwa na jeraha mdomoni, kwenye kidevu na kichwani na sababu za kifo chake ni kutokwa kwa damu nyingi kutokana na majeraha hayo.
Shahidi wa pili, Modesta Limoyi, mkazi wa KDC Mjini Moshi ameelezea namna alivyopigiwa simu na Lilian Benard akimjulisha kuwa mama yake alikuwa haonekani na Septemba 14, 2021 mwili ulipopatikana alikwenda kushuhudia.
Kwa upande wake, shahidi wa tatu, Dismas Kessy ambaye alikuwa akiishi na marehemu ambaye ni shangazi yake, aliporudi usiku wa Septemba 10, 2021 saa 2:00 usiku na kumuulizia shangazi yake, John alimjibu ameenda kununua dawa.
Shahidi huyo aliamua kufuatilia na kwenda katika hospitali ambayo shangazi yake alikuwa anapenda kwenda kutibiwa lakini hakumpata na siku iliyofuata alienda Hospitali ya Faraja hakumpata hadi mwili wake ulipopatikana Septemba 14,2021.
Mbali na shahidi huyo, shahidi wa nne, Koplo Neema alielezea namna alivyochunguza mauaji hayo; yeye na shahidi wa sita, Koplo Joseph Temba ndio walioandika maelezo ya mshitakiwa yakiwamo ya kukiri kufanya mauaji.
Katika utetezi wake, mshitakiwa amesema Septemba 10,2021 saa 12 jioni alirejea nyumbani kutoka machungani na kumkuta tajiri yake anafunga geti; alimweleza kuwa anakwenda Himo kununua dawa lakini hakurejea.
Sigani ameieleza Mahakama kuwa yeye ndiye aliyetoa ripoti polisi ya kutoweka kwa tajiri yake na alitoa taarifa hiyo Septemba 12, 2021 na wakati wa kutoa taarifa hiyo, alikwenda polisi na watoto wawili wa marehemu.
Amejitetea kuwa Septemba 14,2021 saa 12:00 asubuhi alimjulisha shahidi wa tatu, Dismas Kessy kuwa anataka kurejea kwao Dodoma na alimuuliza kama alikuwa na nauli na akajibu kuwa hakuwa na nauli ndipo Dismas alimpa fedha Sh40,000.
Amesema alisafiri na basi la Shabiby na walipofika Babati, kondakta alimfuata na kumuuliza kama alikuwa amepandia basi eneo la Himo na akamjibu ndio na kondakta akamuuliza ametenda kosa gani na kujibu hajafanya kosa lolote.
Kondakta na dereva wakamwambia wamepewa maagizo na polisi wamkabidhi kituo cha polisi chochote cha jirani; walimkabidhi Kituo cha Polisi Chemba na huko hakuwahi kutoa maelezo yoyote isipokuwa Moshi alipolazimishwa kusaini karatasi ambazo alikuwa hafahamu zimeandikwa nini.
Maelezo ya ungamo yalivyokuwa
Katika sehemu ya maelezo yake yake aliyoyaandika Kituo cha Chemba mkoani Dodoma alipokamatiwa wakati akitoroka, Sigani anaeleza kuwa aliamua kumuua tajiri yake huyo kwa kuwa alikuwa akimdai mshahara wa mwezi mmoja.
“Nilikuwa namdai mshahara wangu wa mwezi mmoja na aliponiambia hana nikashikwa na hasira nikaenda kukata majani, alivyokuja kunisaidia nikamkata panga kichwani na kwenye mdomo na kumuua papo hapo,”anaeleza.
Alipouulizwa kama alimuulia Korongoni kwa nini chumba cha marehemu kilikuwa na damu alijibu: “Baada ya kumuua kanga yake ilikuwa na damu sana nikaichukua na kwenda nayo chumbani kwake.Nilivyooona wataiona nikaenda kutupa chooni.”
Hata hivyo, Sigani alivyoulizwa kama wakati anatekeleza mauaji hayo alishirikiana na mtu mwingine alibadili hadithi na kueleza kuwa siku ya tukio, tajiri yake alimwambia hana pesa, akaacha mkoba wa pesa chumbani na kwenda kuoga.
“Nikaingia chumbani kwake na kupekua na kukuta hicho kipochi na kuchukua. Nikiwa natoka nikakutana naye akaniuliza nimebeba nini nikamjibu sio kitu. Akanifuata na kuichukua na kuniuliza kwanini ninamuibia,”ameeleza Sigani.
“Akaniambia nisubiri hapo anipeleke kituoni. Ndipo nilipoenda chumbani kwangu na kuchukua panga nikamfuata chumbani kwake na kumkata panga la kichwani. Alipodondoka nikamkata lingine la chini ya mdomo,” amesimulia Sigani.
“Alipokufa nilimfungia chumbani kwake na kila aliyekuja kuulizia nilimjibu ameenda Himo na ilipofika usiku wa saa nane nilimtoa kwa kumburuza mpaka huko korongoni na kumfunika na majani kabla ya kumtoa nilimbaka.”
Hukumu ya Jaji Simfukwe
Katika hukumu yake aliyoitoa jana Machi 20, 2024, Jaji Simfukwe amesema kutokana na maelezo hayo ya ungamo na matendo yake mara baada ya mauaji hayo, amefikia hitimisho alitenda kosa hilo.
Jaji Simfukwe amesema ni msimamo wa sheria kuwa matendo ya mtuhumiwa baada ya tukio, yanaweza kutoa ashirio la hatia aliyonayo juu tendo alilofanya.
Kuhusu maelezo yake kama aliyatoa kwa hiyari ama la na kama aliteswa na polisi kituo cha kati mjini Moshi, Jaji amesema kumbukumbu zinaonyesha maelezo hayo yalichukuliwa na shahidi wa sita, koplo Joseph Temba huko Chemba, Dodoma.
“Mshitakiwa wa kwanza hakuwahi kusema kama aliteswa Dodoma alipoandika maelezo yake ya kukiri kosa, badala yake analalamikia maelezo yaliyoandikwa na shahidi wa nne, Koplo Neema na sio yaliyoandikwa na shahidi wa 6 koplo Joseph”
“Mahakama hii inaridhika kuwa maelezo haya ya kukiri kosa yalitolewa kwa hiyari. Kama yangekuwa yametolewa bila hiyari yake, maudhui yangeweza kuwa tofauti”
“Kwa mfano yasingetoa picha mbili tofauti za eneo la mauaji. Moja kwamba ilikuwa kwenye korongo na nyingine kwenye chumba cha kulala cha marehemu. Hadithi ingekuwa imekwenda moja kwa moja (straight)”ameeleza Jaji Simfukwe.
Kuhusu uwepo wa nia ovu, Jaji Simfukwe amesema kitendo cha mshitakiwa kuelezea hadithi zinazokinzana katika maelezo yake ya kukiri kosa, kunaonyesha nia yake ovu na hiyo haiondoi ukweli kuwa alimuua marehemu Elizabeth.
“Kilichomo katika maelezo yake ni ushahidi bora unaomuingiza katika kosa hili. Mbali na hilo, lakini mshitakiwa aliwapotosha shahidi wa tatu na watu wengine kuwa marehemu amekwenda Himo kununua dawa akijua alishamuua,” amesema Jaji Simfukwe.
Katika kuhitimisha hukumu yake, Jaji Simfukwe amemwachia huru mshitakiwa wa pili, Steven Mmbando akisema ushahidi uliotolewa dhidi yake haujaweza kuthibitisha shitaka hilo juu yake na haukuwa na chochote.