Mtoto wa miezi minane aokotwa akiwa amefariki

Moja wa askari Polisi Mtwara ambaye jina lake halikufahamika akiuchukua mwili wa mtoto mchanga uliokuwa umetupwa jalalani. Picha na Florence Sanawa
Muktasari:
- Mwili wa mtoto mchanga wa kiume anayekadiriwa kuwa na miezi minane amekutwa akiwa ametelekezwa jalalani huku akiwa amefariki.
Mtwara, Jeshi la Polisi mkoa wa Mtwara linafanya uchunguzi wa tukio la mwili wa mtoto mchanga wa kiume kutelekezwa jalalani na mtu asiyejulikana, katika Mtaa wa Kiyangu A Manispaa ya Mtwara Mikindani ukiwa hauna nguo.
Kaimu Kamanda Polisi Mkoa Mtwara, ACP Mtaki Kurwijila amesema kuwa mnamo Januari 16, 2024 majira ya saa 4 asubuhi katika jalala liliopo katika Mtaa wa Kiyangu A Wilaya ya Mtwara, ulikutwa mwili wa mtoto mchanga wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi minane ukiwa umetelekezwa.
Amesema kuwa mwili huo uligunduliwa na mtupa taka ambapo tayari mtoto huyo alikuwa amefariki. “Mwili umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, Ligula kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
ACP Kurwijila amesema kuwa tukio hilo limegunduliwa baada ya wabeba takataka kubaini na kisha kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa mtaa wa kiyangu A, Yusuph Abdul ambaye alitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.
Aidha uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kufanyika ili kubaini muhusika wa tukio hilo ili afikishwe mbele ya sheria.
“Ni vema jamii ikajua kuwa unapokutana na changamoto zozote zile za maisha washirikishwe ndugu, jamaa na marafiki ili kupata utatuzi. Hatua hii itasaidia kukomesha vitendo vya kikatili vya kutupa watoto wachanga vinavyosababisha kugharimu maisha ya watoto” amesema ACP Kurwijila.
Naye, David George (mtupa takataka aliyekiona kichanga hicho) amesema kuwa alifika eneo hilo ambalo hufanyia kazi na kubaini uwepo wa kichanga hicho, ambacho kilitupwa jalalani hapo bila nguo.
“Mimi huwa nafanya usafi katika eneo hili asubuhi nilipofika niliona kiumbe nikasema mbona ni kama mtoto, nilipofika karibu niliona ni mtu kwa kuwa aliachwa wazi wala hakufunikwa na kitu. Niliogopa nikaamua kutoa taarifa kwa mwenyekiiti wa mtaa ili kupata msaada zaidi” amesema George.
Zaituni Aus mkazi wa Kiyangu A amesema kuwa tukio hilo ni baya na pia linaonyesha wazi kuwa aliyetenda amedhamiria ndio maana hakumsitiri huyo mtoto.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa mtaa huo, Yusuph Namanolo amesema kuwa alipokea simu kutoka kwa watu wanaotunza jalala hilo, ambapo walieleleza namna walivyomuona kiume huyo na kumjulisha.
“Nilipofika nilisikitika sana naona hata hofu ya Mungu imepotea inakuwaje mtoto anatupwa tena jalalani, hili jambo sio sawa mjue inauma sana kwa nini mtu atelekeze kitoto kama hicho ambacho bado hakijajua kitu bila kuogopa” amesema Namanolo.