Mtoto aliyekatwa koromeo wilayani Njombe afariki dunia

Muktasari:
Meshack Myonga (4), aliyenusurika kuuawa baada ya kutekwa na kukatwa koromeo wilayani Njombe amefariki dunia leo mchana Jumamosi Februari 9, 2019 katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya
Njombe. Meshack Myonga (4), aliyenusurika kuuawa baada ya kutekwa na kukatwa koromeo wilayani Njombe amefariki dunia leo mchana Jumamosi Februari 9, 2019 katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
Desemba 23, 2018 mtoto huyo alitekwa na mtu asiyejulikana akiwa nyumbani kwa wazazi wake mtaa wa Mji Mwema wilayani Njombe, kisha kupelekwa msituni na kukatwa koromeo kabla ya kuokolewa na kijana mmoja.
Baada ya kuokolewa alipelekwa Hospitali ya Mkoa ya Kibena-Njombe na baadaye kuhamishiwa hospitali ya rufaa Mbeya kwa matibabu zaidi.
Akizungumza na Mwananchi mama mzazi wa mtoto huyo, Rabia Mlelwa amesema, "Leo tumekwenda Hospitali na madaktari wakamchukua wakaingia chumba cha matibabu, baadae nikaitwa na kuambiwa mtoto amefariki. Hata sielewi imekuaje."
"Wakati wanaingia nae ndani hawakuniambia lolote kuhusu maendeleo yake ila waliniambia mwanangu amefariki, wamesema mtoto koromeo lake lilikuwa limekaa vibaya hivyo alikuwa mtu wa kufa muda wowote."
Amesema alipewa taarifa za kifo cha mwanaye saa nane mchana, kuelezwa koromeo lilikuwa limesinyaa.
Amebainisha kuwa jana ndio alitakiwa kurudi katika hospitali hiyo kujua maendeleo ya mwanaye baada ya kukaa wiki mbili katika hospitali hiyo ya rufaa wakipatiwa matibabu.
"Jana Mkuu wa wilaya ya Njombe (Ruth Msafiri) alitoa gari lililotuleta Mbeya, lakini leo baada ya tukio hili ametaarifiwa hivyo ameamuru gari hilo lirudi tena kwa ajili ya kutuchukua hivyo kesho asubuhi ndiyo tutaanza safari kurudi kijijini Ngalangwa (Njombe)," amesema.