Msukuma ataka wapotoshaji mkataba bandari washunghulikiwe

Mbunge wa Geita Vijiji Joseph Msukuma
Muktasari:
- Sakata la makubaliano ya ushirikiano baina ya Serikali za Tanzania na Dubai katika uendeshaji wa bandari, limemuibua Mbunge wa Geita Vijiji Josephu Musukuma (CCM) ambaye ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua wanaopotosha kuhusu mkataba huo.
Dodoma. Sakata la makubaliano ya ushirikiano baina ya Serikali za Tanzania na Dubai katika uendeshaji wa bandari, limemuibua Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ ambaye ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua wanaopotosha kuhusu mkataba huo.
Mkataba huo wa mashirikiano wenye ibara 31 ulisainiwa Oktoba 25 mwaka jana na serikali hizo mbili kwa lengo la uendelezaji, uboreshaji na uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 9, 2023, jijini hapa Mbunge huyo amesema anajua imetengenezwa propaganda ili kukwamisha jambo hilo hivyo vyombo vya ulinzi na usalama vinatakiwa kuwachukulia hatua kali wanaofanya hivyo.
“Watanzania tunahitaji kuwa na akili za kufikiria na Watanzania wenzangu wa kawaida ndio tunamiliki uchumi wa Tanzania, uchumi wa Tanzania haumilikiwi na watu wenye degree wanaotusumbua mitandaoni,” amesema na kuongeza;
“Imetengenezwa propaganda, mimi niwashauri vyombo vya ulinzi na usalama tumekuwa wapole sana, hatuwezi kwenda kwa style hii, mtu anaamua kutengeneza uongo taharuki, hakuna hatua yoyote ambayo inachukuliwa, kweli?
Mbunge huyo amesema yeye ni mmoja ya wabunge waliosafirishwa kwenda Dubai kujifunza jinsi ambavyo bandari ya nchi hiyo inavyofanya na alienda kwa fedha za Bunge.
“Mimi naamini maneno yanayoandikwa katika mitandao sio kweli hata Rais Samia atastaafu ataishi maisha kama ya kwetu, tusikatishane tamaa; turudi nyuma, hakuna mradi mkubwa wa kimkakati tumeufanya bila ya kuwa na makelele na makelele haya yanatengenezwa,” amesena Msukuma.
Jana alhamisi Juni 8, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa ametolea ufafanuzi suala hilo akisema mkataba huo ni wa miezi 12 na baada ya hapo kutakuwa na mikataba ya utekelezaji.
Kwa upande mwingine, Spika wa Bunge Dk Tulia Akson jana Juni 8 2023, amesema suala hilo litawasilishwa bungeni Juni 10, 2023 kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na wabunge.