Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mshtakiwa adai hayupo tayari kusikiliza kesi yake, Mahakama yamgomea

Mshtakiwa Pascal Dunia anayekabiliwa na shtaka la kusafirisha meno mawili ya tembo yenye thamani ya Sh 34milion, akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Dunia anakabiliwa na shitaka moja la kusafirisha vipande viwili vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh34 milioni, bila kuwa na kibali.

Dar es Salaam. Wakati washtakiwa wengi ambao hawana dhamana, wakiomba usiku na mchana kesi zao zisikilizwe haraka na kutolewa uamuzi, hilo ni  kwa mshtakiwa  Pascal Daima (39).

Daima, mkazi wa Kongowe anayekabiliwa na shitaka la kusafirisha vipande viwili vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh34 milioni, ametoa mpya mahakamani baada ya kudai kuwa hayupo tayari kusikiliza ushahidi bila kutoa sababu.

 Mshtakiwa huyo ametoa maelezo hayo, leo Jumatatu, Januari 20, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini hapa, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashitaka.

Ametoa maelezo hayo, muda mfupi baada ya wakili wa Serikali, Erick Kamala kuieleza mahakama hiyo kuwa, kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa na upande wa mashitaka unao mashahidi wawili.

Kamala baada ya kueleza hayo, mshtakiwa alinyoosha mkono na alipewa nafasi ya kuongea, alidai kuwa hayupo tayari kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka.

Alipoulizwa na Hakimu Mwankuga sababu ya kutokuwa tayari ni ipi? Hakutoa sababu.

Pili, mshtakiwa huyo amedai kuwa hajapewa maelezo ya mashahidi na mlalamikaji ili ayapitie ndipo kesi hiyo ianze kusikilizwa.

Hakimu Mwankuga amemueleza kuwa maelezo ya mashahidi hawezi kupewa bali anatakiwa kusikiliza ushahidi mahakamani hapo.

Kuhusu maelezo ya mlalamikaji, hakimu Mwankuga ameelekeza mshtakiwa apewe maelezo ya mlalamikaji ili ayapitie kwa dakika 30.

Baada ya maelekezo hayo, mshtakiwa alipewa nakala ya maelezo ya mlalamikaji ambayo yalikuwa na kurasa nne na kwenda nayo mahabusu kuyasoma.

Hata hivyo, baada ya dakika 30 kuisha, mshtakiwa huyo alipandishwa Mahakama kwa mara ya pili, kisha hakimu Mwankuga amemueleza mshtakiwa kuwa Mahakama ipo tayari kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka.

Mwankuga baada ya kutoa maelekezo hayo, mshtakiwa alinyoosha mkono tena na alipopewa nafasi alidai kuwa amesoma nyaraka hiyo lakini mwanga ulikuwa mdogo kule mahabusu, hivyo hayuko tayari kuendelea.

"Mheshimiwa hakimu, nimeisoma hiyo nyaraka ila mwanga ulikuwa mdogo kule mahabusu, hivyo sipo tayari kuendelea," amedai Daima.

Mshtakiwa ameendelea kudai kuwa ndugu zake wanakuja mahakamani hapo kwa ajili ya kumtafutia wakili, hivyo hayupo tayari kuendelea kwa leo.

Hakimu Mwankuga baada ya kusikiliza maelezo ya mshtakiwa amedai sababu alizotoa mshtakiwa hiyo hazina msingi kisheria na kwamba kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara.

"Mshtakiwa Dunia, kesi hii itaendelea leo na usikilizwaji kwa sababu hujatoa sababu za kisheria ambazo zingenifanya niahirishe kesi hii, lakini pia upande wa mashitaka umeleta mashahidi wawili hapa, hivyo tunaendelea na usikilizwaji" amesema Hakimu Mwankuga.

Hakimu baada ya kutoa maelezo hayo, upande wa mashtaka ulimuita shahidi na kuanza kutoa ushahidi.

Shahidi huyo, Ofisa Wanyamapori Augustino Kawala(37) kutoka Kikosi cha Kupambana na Ujangili Kanda ya Mashariki na Pwani, amedai kuwa alifanya tathimini ya meno hayo.

Akiongozwa kutoa ushahidi na wakili Makala, shahidi huyo mwenye uzoefu wa miaka 10 katika kikosi hicho, amedai kuwa Agosti 9, 2021 aliitwa na kiongozi wa kazi aende kituo cha Polisi Oysterbay kufanya utambuzi na tathimini ya vitu vilivyokamatwa ambayo vinadhaniwa ni nyara za Serikali.

"Nilipewa boksi rangi ya kaki ambalo kwa nje lina nembo ya K- Vant ambalo ndani yake kulikuwa na mfuko wa salfeti uliokuwa na vipande viwili vya meno ya tembo vyenye kilo 15.18" amedai Shahidi.

Ameendelea kueleza kuwa baada ya kufanyia utambuzi aligundua kuwa yale ni meno ya tembo.

"Utambuzi huu ulikuwa ni kuangalia maumbile kwa macho na kila nyara ina maumbile ya kipekee" amedai.

Ameendelea kufafanua kuwa meno ya tembo yakikatwa katika vipande zaidi ya viwili huwa kunakuwa na mistari midogo kwa ndani na huo ndio upekee uliopo.

Ameendelea kudai kuwa baada ya utambuzi huo aligundua tembo aliyeuawa  ni mmoja na thamani ya tembo mmoja ni Dola za Marekani 15,000,  ambapo kwa siku hiyo, dola moja ilikuwa ni Sh2287.85 , sawa na Sh34, 317,722.

"Nilipima uzito kwa kila kipande na meno ya tembo, ambapo kimoja kilikuwa na uzito wa kilo 7.320 na kingine kilo 7.875 na kupata jumla ya kilo 15.18" amedai shahidi. Kisha niliandaa fomu ya tathimini ya wanyamapori na kuijaza na kisha kumkabidhi mtunza vielelezo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho itakapoendelea.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, Agosti 6, 2021 katika eneo la Tandale Mhuluge , lililopo wilaya ya Kinondoni, ambapo siku hiyo alikutwa akisafirisha vipande viwili vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh34 milioni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.