Uchunguzi kesi ya kusafirisha mifupa, kucha za simba bado

Muktasari:
- Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 12, ikiwemo kuongoza genge la uhalifu, kughushi, kukutwa na mifupa ya simba, meno ya tembo, na nyara nyingine, zote zenye jumla ya thamani ya Sh3.3 bilioni.
Dar es Salaam. Serikali imesema bado inaendelea na uchunguzi katika kesi ya kusafirisha nyara za Serikali, ikiwemo mifupa 1,107 ya simba zenye jumla ya thamani ya Sh3.3bilioni, inayowakabili washtakiwa 12 wakiwemo waliokuwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA).
Wakili wa Serikali, Titus Aaron ameieleza hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatatu Agosti 26, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Mele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, Wakili Aaron alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea, hivyo kuomba tarehe nyingi kwa ajili ya kutajwa.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mwankuga ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 25, 2024 itakapotajwa. Washtakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba Mahakama Kuu.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 28/2023 ni Abdulah Hamad (58) mfanyabiashara na mkazi wa Ubungo Maziwa, Kampuni ya AB Marine Products Ltd iliyopo Ubungo Maziwa.
Wengine ni Meneja Mkazi wa Kampuni ya Airline Ltd, Roseline Achachi Wandera(43) mkazi wa Mikocheni, Kennedy Mwambeta na Noel Kasaro (41) Mratibu wa Mizigo na mkazi wa Tabata.
Walinzi wawili wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Tito Mwabe (34) na Erasto Makinda(46); Wakala wa mizigo Theresia Lukanga(40) na Abubakari Pazi(32) Wakala wa mizigo kutoka kampuni ya Smart Ocean.
Pia yupo Haipeng Guo (34) mfanyabiashara na raia wa China, Yassir Husein (50), mfanyabiashara na mkazi wa Arusha pamoja na Peter Kikweka(50) mfanyabiashara na mkazi wa Ukonga Mombasa.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 12. Mashtaka mawili ni ya kuongoza genge uhalifu, mashtaka matatu ni ya kughushi, mashtaka manne ya kukutwa meno ya tembo, shtaka moja kujihusisha na nyara za Serikali na shtaka lingine ni kukutwa na mifupa ya simba kinyume cha sheria.
Miongoni mwa mashtaka hayo, ni shtaka la kwanza na la pili ambalo ni kuongoza genge la uhalifu linalowakabili washtakiwa wote, ambapo inadaiwa kati ya Januari mosi 2019 na Mei 27, 2023 katika Uwanja wa Ndege wa Pemba uliopo mji wa Cabo Delgado Province, uliopo nchini Msumbiji, walipanga genge la uhalifu kwa kupokea, kuuza na kusafirisha vipande 166, zenye thamani ya Dola 1,410,000 za Mareani (Sh3.2 bilioni) mali ya Serikali, bila kuwa na kibali.
Washtakiwa pia, wanakabiliwa na shtaka la kukutwa na mifupa ya simba, ambapo kati ya Januari mosi 2019 na Mei 27, 2023 katika Uwanja wa Ndege wa Pemba uliopo mji wa Cabo Delgado Province, uliopo nchini Msumbiji, isivyo halali walikutwa na mifupa 1107 ya simba yenye thamani ya Sh61 milioni, kinyume cha sheria.
Pia wanadaiwa kujihusisha na kupatikana na nyara za Serikali ambazo ni meno ya tembo vipande 166 vyenye uzito wa kilo 236.82, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Januari mosi, 2019 na Mei 27, 2023.
Vilevile, wanadaiwa kupatikana na meno 20 ya simba na kucha 65 za simba zikiwa na thamani ya Sh57 milioni na kusafirisha samaki aina ya kaa bila kuwa na vibali.