Prime
Msako ujenzi holela majengo Kariakoo waanza kung’ata
Muktasari:
- Soma hapa
Dar es Salaam. Tukio la kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu 31 na kujeruhi wengine Novemba 2024, limeendelea kusalia kwenye vichwa vya Watanzania.
Ni miongoni mwa matukio yaliacha taswira ya hofu ya usalama kwa kila mmoja anapolitaja eneo la Kariakoo.
Kwa waliojeruhiwa na kubaki na ulemavu wa kudumu, kupoteza ndugu na jamaa huku wengine wakipoteza mitaji ya biashara, tukio hili litaendelea kujenga kumbukumbu mbaya kwenye historia ya maisha yao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, Levian Anatory akikagua nyaraka katika moja ya jengo lililopo mtaa wa Kisarawe, Kata ya Gerezani Kariakoo walipokuwa wanafanya ukaguzi wa majengo eneo hilo.
Baada ya tukio hilo, hatua mbalimbali zilichukuliwa ikiwemo Serikali kuunda timu ya kucunguza ubora wa majengo eneo la Kariakoo, ambapo mambo mbalimbali yaliibuliwa ikiwemo ukiukwaji mkubwa wa sheria, utoaji wa vibali holela na uendelezaji majengo kinyemela tofauti na vibali vilivyotolewa.
Hata hivyo, matukio yanayoacha maumivu katika eneo la Kariakoo yameendelea kusikika kila kukicha huku siku za karibuni matukio ya moto kwenye majengo yamezidi kushika kasi na kusababisha athari mbalimbali.
Kutokana na matukio hayo mfululizo na vilio vya ujenzi wa majengo yasiyozingatia sheria na ubora, Halmashauri wa Jiji la Dar es Salaam, imeanza kuchukua hatua kwa kusimamisha ujenzi wa majengo mawili ya ghorofa.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kile kilichoelezwa kwamba, ujenzi huo haukufuata sheria za ujenzi. Majengo hayo yaliyopo kwenye Mtaa wa Kisarawe, Kata ya Gerezani.
Kamati hiyo ambayo imeanza operesheni maalumu ya ukaguzi wa majengo yanayojengwa bila vibali katika maeneo mbalimbali ya jijini humo imeanza Kata ya Gerezani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Majengo, Leverian Anatory amesema katika ukaguzi huo wamebaini baadhi ya wamiliki wa majengo wameendelea na ujenzi bila vibali halali.
“Tumefika kwenye ‘saiti’ zote tulizopita, hakuna hata moja ambayo tumekuta mhandisi. Na maana yake ni kwamba baada ya kukagua majengo, tumebaini wamiliki wanatoa maelekezo wenyewe bila wataalamu,” amesema Anatory.
Amesema kamati imeacha notisi za kusimamisha shughuli za ujenzi katika maeneo yote yaliyokutwa na kasoro, huku wamiliki wakitakiwa kuwasilisha nyaraka zinazohitajika kabla ya kuendelea.
“Tumeacha notisi za kusimamisha shughuli za ujenzi kwenye hizi ‘saiti’ na tunasubiri wahusika watakapokuja kuleta nyaraka tulizozitaka, zikiwemo nyaraka za ukaguzi na vibali vya ujenzi.” amesema.
Amesema pia katika baadhi ya maeneo wamebaini michoro ya majengo haijakamilika ipasavyo.
Mwenyekiti huyo, amesema katika baadhi ya majengo hawajafanikiwa kuona michoro, kwa hiyo wamejipanga kwa ajili ya kurudi tena kuangalia waliowaachia notisi za kusimamisha ujenzi kama watakuwa wamekamilisha taratibu za kisheria.
Amesema hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maelekezo hayo bila upendeleo.
Pia, amesema kamati imejipanga kuhakikisha ukaguzi unafanyika kwa ufanisi kwa kushirikiana na wataalamu wa idara mbalimbali za ujenzi na mipango miji katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Anatory amesema mkakati uliopo ni ukaguzi wa jengo kwa jengo kama ilivyofanyika leo kwa kuanza na mtaa mmoja na hawatapoa, kwani lengo ni kuhakikisha majengo yote yanayojengwa ndani ya mipaka ya halmashauri yanazingatia sheria.
“Tumeanza rasmi na tutapita kila eneo kuhakikisha kila jengo linajengwa kwa mujibu wa sheria na wote watakaobainika kukiuka sheria, basi sheria itachukua mkondo wake na hakuna atakayesamehewa,” amesema.
Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Valerian Momburi amesema majengo mengi hayajatekeleza matakwa ya usalama wa moto kama inavyotakiwa na sheria.
Kamati ya ujenzi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ikiwa katika ukaguzi wa ujenzi Mtaa wa Kisarawe, Kata ya Gerezani, Kariakoo.
“Tumekuta majengo hayana mifumo ya kinga dhidi ya moto kama vigunduzi vya moshi, paneli za udhibiti wa moto, mizunguko ya bomba la kuzimia moto na ngazi maalumu za dharura. Haya ni mambo ya msingi katika ujenzi wa majengo makubwa, lakini hayajazingatiwa,” amesema Momburi.
Hata hivyo, wamiliki wa majengo hayo hawakupatikana mara moja kuzungumzia hatua hiyo na mlinzi wa jengo mojawapo ambaye hakutaja jina lake, alipoulizwa kuhusu muhusika alisema ametoka na angerudi baada ya dakika 10 na kamati hiyo iliahidi kurudi baada ya muda huo walioelezwa.
"Siwezi kueleza chochote na muhusika alikuwepo muda si mrefu lakini ametoka kama mnaweza nendi kisha mrudi baada ya dakika 10, atakuwepo na mimi nitamueleza ujio wenu," alisema mlinzi huyo.
Hata hivyo, baada ya kuzunguka Kamati ilirudi tena katika jengo hilo lakini muhusika hakuwepo ndipo walipoamua kutoa notisi ya kusimamisha ujenzi na kumtaka muhusika kufika ofisi za jiji.
Changamoto sheria
Mtaalamu wa masuala ya ujenzi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Geraldine Kikwasi amesema changamoto kubwa inayosababisha majengo mengi nchini kuwa hatarini si ukosefu wa ukaguzi wa kushitukiza, bali ni kutofuata sheria na kanuni za ujenzi zilizowekwa tangu mwaka 2008.
“Watu wanajenga kwa kupata vibali, haiwezekani ujenzi uendelee katikati ya mji bila kuwa na vibali. Hata wale wanaopata kibali hawafuati hatua zinazopaswa kufuatwa. Manispaa inapaswa kufuatilia kila mradi ili kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa mujibu wa kanuni,” alisema Profesa Kikwasi.
Alifafanua kuwa taratibu za kupata kibali cha ujenzi ziko wazi, ikiwemo kuchukua fomu katika ofisi za manispaa, kuwasilisha michoro ya majengo, na kusubiri ukaguzi kabla ya kuanza kazi.
“Unapojaza fomu na kuanza kazi, manispaa inapaswa kuja kukagua. Hivyo, ukaguzi wa kushtukiza hauna maana kama hakuna taarifa za msingi. Tatizo si kushitukiza, bali ni kutofuata sheria,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Profesa Kikwasi, kila mradi wa ujenzi unapaswa kuwa na mkandarasi anayesimamia kazi kwa mujibu wa vibali vilivyotolewa, lakini hali halisi inaonyesha miradi mingi inatekelezwa kiholela bila wataalamu.
“Kama hakuna mkandarasi wala msimamizi aliyeidhinishwa, hilo lenyewe ni kosa. Majengo mengi yanayoporomoka ni matokeo ya watu kufanya ujenzi bila kufuata taratibu, au bila ukaguzi wa mara kwa mara,” alisema.
Profesa Kikwasi aliongeza kuwa manispaa zina jukumu la kuhakikisha zinatambua maeneo yote yenye vibali vya ujenzi na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini mapema changamoto zinazoweza kuleta madhara.
“Ukaguzi wa mara kwa mara ni muhimu. Siyo kusubiri majengo yaporomoke ndipo mnakimbilia kufanya ukaguzi wa kushitukiza. Hapo tunakuwa tumechelewa,” alisema.
Alisisitiza kuwa, utekelezaji hafifu wa sheria za ujenzi unaonyesha mapungufu katika usimamizi wa mipango miji na udhaifu wa baadhi ya watendaji katika halmashauri.
“Kibali cha ujenzi hakitolewi kiholela. Kinaambatana na tathmini ya udongo, uwezo wa jengo kubeba uzito, na usalama wa wakazi. Ukaguzi wa kushitukiza hauwezi kuwa suluhisho la mfumo dhaifu,” alisema.
Kwa mujibu wa Profesa Kikwasi, ili kukomesha migogoro na ajali za majengo kuporomoka, ni lazima manispaa zitekeleze wajibu wake ipasavyo kwa kufuatilia kila hatua ya ujenzi na kuhakikisha sheria zinaheshimiwa.
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Valerian Momburi akitoa maelekezo kwa fundi umeme aliyekuwa anaendelea na shughuli yake ya uwekaji wa nyaya huku kukiwa na maji
Kamati ya Majaliwa
Hatua ya halmashauri ni mwendelezo wa zile zilizochukuliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipounda kamati Novemba 21, 2024 kufanya uchunguzi kutokana na kuporomoka ghorofa la Mtaa wa Mchikichi na Congo.
Kamati pia, ilichunguza majengo mengine yanayoendelea kutumika katika eneo la Kariakoo na kuangalia uimara wa majengo yanayojengwa.
Majaliwa alisema kamati ingechunguza endapo uboreshaji wa majengo unaofanywa Kariakoo unazingatia sheria, kanuni na taratibu na kubainisha majengo yote yaliyo katika hatari ya kuanguka na kupendekeza hatua za kuchukua.
Hata hivyo, licha ya uwepo wa maelekezo hayo bado matukio yanayoacha maumivu katika eneo la Kariakoo yameendelea kusikika kila kukicha.
Katika miezi mitatu majengo manne ya mitaa tofauti yamekumbwa na balaa la moto huku wafanyabiashara wakilalamika kutokuwepo kwa ukaguzi kutoka mamlaka husika.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kariakoo Magharibi, Said Omary alisema changamoto zinazojitokeza katika maeneo ya Kariakoo ni kutokuwepo kwa uwajibikaji kwa viongozi wanaosimamia ujenzi ili kuhakiki kila hatua inakuwa salama.
“Nakutana na kesi nyingi za malalamiko ya wafanyabiashara kuanzia ujenzi wa majengo, masuala ya moto hadi mazingira, ninapozichukua na kuzipeleka sehemu husika, ni kama zinapuuzwa tunahitaji mamlaka iwajibike,” alisema Omary.