Mrufani alivyoepa kitanzi kesi ya mauaji ya bodaboda
Muktasari:
- Jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa laeleza upande wa mshtaka ulishindwa kuthibitisha shtaka la mauaji pasipo kuacha shaka
Arusha. Mahakama ya Rufaa imemuachia huru, Charles Kidaha, aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya dereva wa bodaboda, Frank Joseph.
Awali, katika Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Kidaha pamoja na Kuzenza Jendesha na Joseph Mtema, walishtakiwa kwa mauaji Frank, yaliyodaiwa kufanyika Aprili 26, 2014.
Charles alitiwa hatiani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa, huku wenzake wakiachiwa huru.
Hakuridhika na hukumu pamoja na adhabu akakata rufaa ya jinai namba 246/2022 iliyosikilizwa na majaji Augustine Mwarija, Lilian Mashaka na Eliezer Feleshi. Jopo hilo lililoketi Sumbawanga lilitoa hukumu Septemba 4, 2025 na nakala kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Jaji Mashaka katika hukumu ya jopo amesema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi ya mrufani pasipo kuacha shaka, hivyo Mahakama imetengua hukumu ya Mahakama Kuu na kuamuru aachiwe mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali.
Kesi ya msingi
Wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi, ilidaiwa tukio la mauaji lilitokea Aprili 26, 2014 katika Kijiji cha Mpembe, wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Ilielezwa Frank (marehemu) alikuwa dereva wa bodaboda aliyekuwa akiegesha pikipiki jirani na Hospitali ya Wilaya ya Katavi.
Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Geofrey Mongomongo, ambaye pia ni dereva wa bodaboda alidai alimuona mtu akimsogelea Frank na kumkodi baada ya kukubaliana nauli, lakini baada ya siku hiyo Frank hakuwahi kurudi.
Alidai siku iliyofuata walipokea simu kutoka kwa kiongozi wao wa bodaboda kuwa Frank amefariki dunia.
Katika ushahidi alidai alikwenda mochwari ambako askari polisi walifungua mwili wa marehemu kwa ajili ya utambuzi akautambua kuwa ni wa Frank.
Ripoti ya uchunguzi wa mwili huo ilionesha chanzo cha kifo ni kuumia kichwa kulikosababishwa na kitu butu, hivyo damu kuvuja na kusababisha upungufu wa oksijeni kwenye ubongo.
Jioni ya Mei 21, 2014, shahidi wa tano ASP Halifan William, alipata taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasekese kuwa kuna watuhumiwa wamekamatwa.
Alieleza wakiwa wameongozana na askari polisi wengine, walikwenda eneo la tukio ambako walikuta umati na watuhumiwa watatu wakiwa wamefungiwa kwenye ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kijiji.
Alieleza ilibainika watuhumiwa walikutwa wakiwa na pikipiki iliyoripotiwa kuibwa na walikuwa wakitafuta wanunuzi.
Waliokamatwa walikuwa mrufani na watu wengine wawili, ambao wote walikana kuhusika na mauaji ya Frank. Mrufani (mshtakiwa) akikiri kukamatwa akiwa na pikipiki aina ya SANLG eneo la Kasekese.
Mrufani alieleza kuwa aliinunua kutoka kwa Hamis Maduhu kwa Sh1 milioni na alikuwa ameshalipa Sh600,000 na kiasi kilichobaki walikubaliana angelipa baadaye. Kadi ya umiliki wa pikipiki angekabidhiwa baada ya kumaliza malipo yote.
Alidai alikamatwa akiwa na Kuzenza na Joseph ambao walimkodi awapeleke Kayenza kuhudhuria sherehe ya harusi.
Mahakama ilimtia hatia mrufani (mshtakiwa) kutokana na kukutwa na pikipiki hiyo pamoja na ushahidi wa kimazingira, huku wenzake wawili wakiachiwa.
Kuhusu rufaa
Hakuridhika akakata rufaa akiwa na sababu tano na baadaye katika hati ya nyongeza alikuwa na sababu saba.
Miongoni mwa sababu hizo ni Jaji alikosea kisheria kwa kumtia hatiani kwa kuzingatia vielelezo cha kwanza hadi cha nne ambavyo havikusomwa kwa mrufani wakati shauri likisikilizwa, vilevile alikosea kwa hukumu kuegemea maelezo ambayo yalikubaliwa kimakosa katika ushahidi.
Sababu nyingine ni Jaji alikosea kisheria kumruhusu shahidi wa nne kutoa ushahidi katika kesi hiyo, huku maelezo yake yakiwa hajasomewa wala taarifa ya msingi kutolewa kwa mrufani au wakili wake, pia kesi dhidi yake haikuthibitishwa pasipo kuacha shaka.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa, mrufani aliwakilishwa na Wakili Peter Kamyalile, huku mjibu rufaa akiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Calistus Kapinga na Wakili wa Serikali, Joseph Mwakasege.
Wakili wa mrufani alieleza Mahakama ilikosea kisheria kumtia hatiani mteja wake bila kuzingatia kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi kwa mujibu wa viwango vinavyotakiwa kisheria.
Kamyalile alieleza vielelezo cha kwanza hadi cha tatu na taarifa ya shahidi wa nne hazikusomwa kwa mrufani, hivyo kukiuka kifungu cha 246 (2) na 289 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 (CPA).
Kuhusu Mahakama kuegemea kimakosa msingi wa kumtia hatiani mrufuani kutokana na kielele cha tatu (maelezo ya ziada), aliisihi Mahakama ifute kielelezo hicho kwenye rekodi, kwani hayakuorodheshwa kama moja ya vielelezo vitakavyotolewa katika kesi hiyo.
Amedai taarifa ya shahidi wa nne aliyekuwa wa nyongeza, haikutolewa kwa mrufani kwani notisi iliyotolewa na upande wa mashtaka ya kuita shahidi wa ziada haikutolewa ndani ya muda muafaka.
Alidai hukumu dhidi ya mrufani ilitokana na kudaiwa kukutwa na pikipiki ambayo haikutolewa wakati wa kesi na hakuna sababu iliyowasilishwa na upande wa mashtaka kwa kushindwa kufanya hivyo. Alidai hakuna ushahidi unaomuhusisha mrufani na mauaji hayo.
Wakili Kapinga, awali alipinga rufaa lakini baadaye aliunga mkono kwa msingi kwamba, shtaka halikuthibitishwa.
Alieleza pikipiki inayohusika na shtaka haikutolewa katika ushahidi ingawa iliorodheshwa kama kielelezo kilichokusudiwa kwa upande wa mashtaka na hakuna sababu iliyotolewa ya kutoitoa.
Wakili Kapinga alieleza upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha shtaka pasipo kuacha shaka ni nani mmiliki halali wa pikipiki.
Uamuzi wa mahakama
Jaji Mashaka katika uamuzi wa jopo amesema suala kuu la kuamua ni iwapo shtaka lilithibitishwa pasipo kuacha shaka.
Amesema kama ilivyoainishwa katika ukurasa wa 25 wa kumbukumbu ya rufaa, upande wa mashitaka ulieleza utaita mashahidi 16 wakati wa kesi na msingi wa ushahidi wa maelezo yao ulisomwa kwa washtakiwa kwa mujibu wa kifungu cha 246 (2) cha CPA.
Jaji amesema rekodi iko kimya haisemi kama inavyotakiwa na kifungu hicho ikiwa kiini cha ushahidi wa vielelezo cha kwanza hadi cha nne, vilisomwa kwa mrufani.
Amesema kama ilivyowasilishwa na wakili wa mrufani na kuungwa mkono na wakili wa Serikali, vielelezo vilistahili kufutwa kwenye rekodi, hivyo vimefutwa.
Jaji Mashaka amesema kuhusu upande wa mashtaka kuthibitisha shtaka dhidi ya mrufani bila kuacha shaka yoyote, wanakubaliana na maoni ya mawakili wote wawili kwamba upande wa mashtaka ulishindwa kuonyesha uhusiano wa moja kwa moja wa jinsi mrufani anavyohusishwa na mauaji.
“Zaidi ya hayo, upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kuwa pikipiki iliyodaiwa kuibwa (kwa bodaboda sasa marehemu) na kukutwa nayo mrufani ni moja. Zaidi ya hapo tulipoamua kufuta kielelezo cha kwanza hadi cha nne, ushahidi uliosalia unaotegemewa na upande wa mashtaka umepunguzwa na hakuna chochote kinachosalia kuunga mkono shtaka dhidi ya mrufani,” amesema.