Mradi wa maji wamvutia kiongozi wa mbio za Mwenge

Muktasari:
Mradi huo ambao ulikuwa kivutio kwa kiongozi huyo akidai taarifa zake zimeonyesha uwazi kwenye utekelezaji wake unatekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wamazingira Vijijini (Ruwasa) ambao utawanufaisha wananchi 3,105.
Buchosa. Wakazi wa Kijiji cha Kasela Kata ya Nyakarilo Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema wataondokana na adha ya maji baada ya mradi wa Sh190 milioni kuwekwa jiwe la msingi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdalla Shaibu Kaim.
Mradi huo ambao ulikuwa kivutio kwa kiongozi huyo akidai taarifa zake zimeonyesha uwazi kwenye utekelezaji wake unatekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wamazingira Vijijini (Ruwasa) ambao utawanufaisha wananchi 3,105.
Akitoa taarifa kwa Kaim leo Ijumaa Julai 16, 2023, Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Sengerema, George Massawe amesema mradi huo umeanza kutekelezwa mwishoni mwa 2022.
Akktaja manufaa ya mradi huo, Massawe amesema utaimarisha uchumi wa jamii kwa kuondoa muda wa kutafuta maji safi na salama ambao watautumia katika shuguli za uzalishaji, kumtuwa mama ndoo kichwani kwa kumuondolea adha ya kutembela umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.
“Pia utachochea ukuaji wa miji hasa baada ya kuwepo huduma ya maji, kuchochea shughuli za kimaendeleo katika sekta ya umwagiliaji wa mashamba, kuchochea na kuimarisha hali ya usalama katika eneo husika, “amesema
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosa, Benson Mihayo akaahidi kusimamia vema miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye halmashauri hiyo.
Baada ya kusikiliza taarifa hiyo, Kaim akamtaka Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga kuendelea kuisimamia vema wilaya hiyo ili wananchi wapate maendeleo.
Naye, Ngaga amesema ushirikiano na uwajibikaji wa wananchi na watumishi wa Halmashauri ya Buchosa ndiyo umefanikisha ufanisi wa miradi nane iliyokaguliwa, kuwekwa jiwe la msingi na kuzinduliwa.