Mpina na mawaziri bado ngoma mbichi

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji (kushoto), Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (kulia) pamoja na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (katikati).
Muktasari:
- Mvutano wa hoja baina ya Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina na mawaziri umeendelea kuibuka bungeni na sasa mawaziri watatu wamelazimika kumjibu kutokana na kile alichokichangia kwenye mchango wake wa bajeti ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2024/25.
Dodoma. Sakata la Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina na mawaziri bado mbichi, baada ya leo mawaziri watatu kuishambulia hoja yake aliyoitoa wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2024/25.
Mawaziri hao ni Hussein Bashe (Kilimo), Profesa Kitila Mkumbo (Mipango na Uwekezaji) na Dk Ashatu Kijaji wa Viwanda na Biashara.
Hii si mara ya kwanza kwa Mpina kuibua mvutano bungeni na kuwafanya mawaziri kadhaa kusimama kujibu hoja zake wakiwemo.
Mawaziri waliowahi kumjibu ni pamoja na Dk Mwigulu Nchemba (Fedha), January Makamba (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Abdallh Ulega (Mifugo na Uvuvi).
Mei 10, 2024, akichangia mjadala wa Wizara ya Maji kwa mwaka 2024/25, aliwatuhumu mawaziri kuwa wanampikia majungu kwa kushindwa kujibu maswali ama hoja anazizitoa bungeni.
Alisema watendaji hao wa Serikali wameshindwa kujibu hoja zake na badala yake wamekuwa wakidai ana jambo lake, huku yeye akidai hana jambo lolote na jambo lake ni moja tu Watanzania wapate maendeleo.
Mjadala wa leo
Leo Jumatano Mei 22, 2024, Mpina tena akichangia bajeti ya Wizara ya Viwanda na biashara kwa mwaka 2024/25 iliyowasilishwa na Dk Kijaji, amesema waziri huyo katika hotuba yake ya bajeti ameonyesha mauzo ya bidhaa nje ya nchi katika masoko ya Afrika Mashariki, nchi za Kusini mwa Afrika, AGOA pamoja na nchi za bara la Asia yamepungua katika mwaka 2023.
Mpina amesema waziri huyo alieleza mauzo hayo yamepungua kwa Sh2.851 trilioni mwaka 2023, lakini Waziri Bashe alipopeleka taarifa yake bungeni alisema kuwa mauzo hayo yameongezeka na kufikia Sh2.86 trilioni.
“Nini kiini chanzo cha mgongano wa taarifa kwa mawaziri hawa wawili katika kipindi hicho kimoja,” amehoji Mpina, aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Aidha, amesema Serikali imekuwa ikipeleka misamaha ya kodi katika Bunge hilo lengo likiwa ni kuchochea, ajira, uwekezaji na mauzo nje lakini kuwasaidia Watanzania kupata bei nzuri ya mazao.
Amesema wamefanya misamaha mwaka jana na miaka mingine lakini wabunge hawajaweza kupata tathimini ya misamaha kuwa imeleta tija gani, limenufaisha watu gani na imevutia wawekezaji wangapi.
Ametahadharisha eneo hilo lisipotumika vizuri na wabunge kupata mrejesho linaweza kuwa eneo la biashara kama biashara nyingine ambazo zinafanywa na baadhi ya watumishi, watu binafsi na baadhi ya mawaziri.
Mpina amesema Tanzania iko nyuma kwenye ukusanyaji wa kodi na kuwa inakusanya kwa asilimia 12.5 ya pato la Taifa ikilinganishwa na nchi za Kenya na Rwanda ambazo zinaanzia asilimia 15 hadi asilimia 16.
Mpina amesema ukusanyaji wa mapato madogo ukilinganisha na nchi nyingine, unasababishwa na changamoto ya misamaha ya kodi na vitu vingine.
Ametoa mfano waliwahi kutoa msamaha kwa uunganishaji wa magari, lakini ukweli ni kwamba magari hayo yanakuja nchini yakiwa yameunganishwa na kinachofanyika ni kushika spana tu.
“Unawaondolea kodi halafu unakwenda kutoza kodi ya muunganishaji pikipiki, wa baiskeli, wa bajaji huyu mwenye trela hapana. Rekebisha hii hazina usawa na hatutendi haki kwa watu wetu. Lakini mwishowe tumevutia uwekezaji gani kwa kuunganisha hayo magari,”amesema.
Amehoji pia ni kampuni gani za wawekezaji zilizopata msamaha na kuleta tija nchini.
Pia amehoji ni tija gani imepatikana katika mfumo wa utoaji vyeti kwa bidhaa zinazoingia nchini (PVoC) kwa kuwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilikuwa halijajiandaa na matokeo yake nchi imekuwa ni jalala la bidhaa feki.
“Hakuna mifumo mizuri ya udhibiti bidhaa, feki zimetambaa kila sehemu hadi pikipiki feki,”amesema Mpina.
Kuhusu mbolea, amesema mbolea ya ruzuku imefikia asilimia 25 ya wakulima tu nchini.
Mawaziri wamjibu
Akimjibu Mpina, Profesa Kitila amewataka wabunge kusoma takwimu kwa ujumla wake, mwaka 2000 mauzo ya bidhaa nje ya nchi yalikuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 935 lakini mwaka jana mauzo ya bidhaa nje ya nchi yamefikia Dola za Mrekani bilioni 8.2.
“Sasa hayo mauzo yaliyoshuka yameshuka wapi? Na katika mauzo haya bidhaa za kilimo zinachukua nafasi kubwa sana na unavyotoa takwimu utoe vizuri kidogo na kama inakuwa changamoto watakusaidia ili utoe takwimu vizuri,” amesema.
Kwa upande wake, Bashe amesema mfumo wa ruzuku ya mbolea, wakulima hutumia mbolea tofauti tofauti kulingana na mazao wanayootesha.
Amesema asilimia 25 ya wakulima anawaona wamenufaika ni wakulima wa mazao ya chakula.
Amesema utumiaji wa wakulima wa mbolea kwa takwimu za miaka mitatu umetoka wastani wa tani 350 na kuwa hadi Juni mwaka huu watafika tani 900.
“Lengo letu ni kufika tani milioni moja ya mbolea ili kwa hekta moja tuweze kufika kilo 50 kwa wakulima wa mahindi, mpunga na mazao ya chakula na ndio lengo la Serikali,”amesema.
Kwa upande wa mauzo ya nje, Dk Kijaji amechagua takwimu za masoko matano tu ambapo masoko manne yameanguka lakini kwa kusema hivyo sio kama kwamba masoko yote Tanzania yameanguka.
Akihitimisha hoja yake, Dk Kijaji amesema takwimu zilizotolewa na Bashe ni za mazao ya kilimo na haziwezi kufanana na takwimu anazozitoa yeye kama Waziri wa Biashara.
“Kwa hiyo hili nimuombe sana Mheshimiwa Mpina usiwe unalenga sana katika kutafuta makosa utaishia kuonekana makosa kwako wewe mwenyewe. Nikuombe sana kaka yangu ni vyema ukaangalia yale mema yanayofanywa na Serikali yetu ya awamu ya sita ili tuweze kumsaidia katika huduma zake anazozifanya kwenye utumishi wa umma,”amesema.