Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpina ataka mafisadi wanyongwe

Muktasari:

  • Waziri wa zamani wa mifugo na uvuvi, Luhaga Mpina ameishauri Serikali na wabunge kutunga sheria ya kuwashughulikia watu wanaobainika kufanya ubadhirifu wa fedha za umma wanyongwe ili kutoa funzo kwa wengine.

Mbogwe. Mbunge wa Kisesa (CCM) Mkoa wa Simiyu, Luhaga Mpina ameiomba Serikali kupitia wabunge kuridhia na kupitisha sheria itakayotoa adhabu kali ikiwemo ya kunyongwa kwa watu watakaobainika kufanya ubadhilifu wa mali za umma.

Waziri huyo wa zamani wa mifugo na uvuvi ametoa kauli hiyo akiunga mkono hoja ya Mbunge wa Mbogwe (CCM) Mkoa wa Geita, Nicodemas Maganga aliyoitoa bungeni akiwataka wabunge kumuunga mkono kutungwa kwa sheria ya kunyongwa kwa wezi, mafisadi, wala rushwa na wabadhirifu wa fedha za umma.

Mpina ameyabainisha haya leo Alhamisi Machi 6, 2025 kwenye mkutano wa hadhara wa jimbo la Mbogwe, uliofanyika kata ya Nyakafuru halmashauri ya Mbogwe akisisitiza matumizi mabaya ya kodi za wananchi ni kuwakosesha haki ya kupata huduma bora za kijamii kutokana na kodi zao.

Amesema kutokana na mafisadi hao wachache, vifo vya wajawazito na watoto bado vipo, vifo vya wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma, elimu mbovu kwa kukosa miundombinu bora ya kufundishia na kujifunzia, huku baadhi wakigawana na kutafuna fedha hizo bila shaka.

“Ninaamini Bunge lijalo la bajeti hii itakuwa moja ya hoja itakayojadiliwa, Rais wetu aliunda tume ya maboresho ya kodi na mimi mchango wangu niliandika kitabu chenye kurasa 235 ili kuweka sawa masuala ya kodi, ripoti yangu ilibaini upotevu wa fedha zaidi ya Sh42 trilioni kila mwaka,” amedai Mpina.

Mpina amesisitiza kutungwa kwa sheria kali itakayowadhibiti wahujumu uchumi hao na kama wakinyongwa watu wawili au watatu watakaobaki wataziogopa mali za umma na hawatozichezea tena na wananchi watapata mahitaji muhimu, ikiwemo vifaa tiba na dawa kwenye vituo vya afya vijijini.

 “Fedha za umma zikitumiwa vibaya, wewe utaenda hospitali, hautamkuta mganga, hautakuta dawa na ni wangapi wamekufa kwa kukosa huduma hizo muhimu, watoto wetu wangapi waliokufa kwa kukosa damu kwa sababu fedha zinaliwa na mafisadi,” amedai Mpina akihoji.

Kadhalika amesema ni vyema wawakilishi wa wananchi wakaepuka kuwa machawa wa viongozi wakubwa na kushindwa kuzisemea changamoto za wapigakura wanyonge na wa hali ya chini, kwani wabunge wengi wamegeuka machawa na kusahau majukumu yao.

Awali, mbunge mwenyeji Maganga amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh74 bilioni za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hasa kwenye sekta ya afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara na kila mwanafunzi anasoma kwenye mazingira mazuri.

Amesema hakuna mwekezaji kwenye sekta ya madini atakayekwenda kuwekeza kwa wachimbaji wadogo kinyemela kulinganisha na wilaya nyingine walivyovamia badala yake atahakikisha wananchi hao wa kipato cha chini, wanachimba na kunufaika wao na familia zao.

“Leo tumebadilisha sheria za wachimbaji wadogo, na katika wilaya ambazo bado hazijapata wawekezaji wakubwa ni Mbogwe, mimi nimekataa tujipange kwanza tuchimbe wenyewe ili tufaidike na sio kuwanufaisha wageni,” amesema Maganga.

Mkazi wa Nyakafuru, Daudi Mashishanga amesema matarajio yao kwa viongozi wanaowachagua ni kuwasemea kwenye ngazi za juu na kushirikiana nao kuwaletea maendeleo ikiwemo umeme, maji na barabara nzuri.