Mpango ahimiza wazazi Njombe kupeleka watoto shule

Muktasari:
Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amewataka wazazi mkoani Njombe kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule ili kuwaanda katika kujenga maisha yao na taifa kwa ujumla.
Njombe. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amewataka wazazi mkoani Njombe kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule ili kuwaanda katika kujenga maisha yao na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Idofi kilichopo Halmashauri ya Mji wa Makàmbako, mkoani Njombe.
Amesema kila mzazi mkoani Njombe anatakiwa kuhakikisha anafuatilia maendeleo ya mtoto wake shuleni ili kujua mwenendo wake katika masomo.
"Msiwaache tu wakanaenda shule na kurudi, amefanya nini, mzazi hujui ndugu zangu hapana mnanisikia wananjombe," amesema Dk. Mpango.
Amesema wanafunzi wanaoacha shule mkoani Njombe siyo kwa asilimia kubwa lakini bado inatakiwa mtoto anapoanza shule wahakikishe anamaliza masomo yake ikiwezekana mpaka chuo kikuu.
Amesema kwenye elimu ya sekondari hali siyo nzuri kwani karibu asilimia 11 ya wanafunzi hawamalizi shule idadi ambayo ni kubwa na wazazi hawapaswi kukubaliana nalo.
Amesema watoto wa kike wanatakiwa kupewa kipaumbele katika kusoma ili miaka ijayo Rais mwanamke aweze kutoka mkoani Njombe.
Aidha Mpango amewataka wananchi mkoani humo kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa ukimwi kwakuwa hali ya maambukizi ni mbaya.
Amesema serikali kupitia wizara ya afya imefanya jitihada ili kupambana na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi hivyo kila mwananchi anatakiwa kujikinga.
Mkazi wa kijiji cha Idofi mjini Makàmbako mkoani Njombe Obadia Mlelwa amesema serikali imeshaweka miundo mbinu mizuri ya madarasa hivyo watahakisha watoto wao wanakwenda shule.
"Tunamshukuru makamu wa Rais kwa kutuimiza kupeleka watoto shuleni nasi tutafanya hivyo kwakuwa serikali imejenga madarasa kila sehemu ili kuhakikisha watoto wanakwenda shuleni" amesema Mlelwa.