Prime
Mpangaji auza nyumba ya Serikali

Nyumba ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) inayodaiwa kuuzwa na mpangaji kinyemela
Muktasari:
- Shirika la Taifa la Nyumba baada ya kubaini mpangaji wake ameuza nyumba aliyokuwa amepangishwa, lilifungua kesi Mahakama Kuu likiomba litangazwe kuwa mmiliki halali wa nyumba hiyo, lakini Mahakama iliitupilia mbali na sasa shauri lipo Mahakama ya Rufani.
Dar es Salaam. Huu ni ujasiri wa aina yake baada ya mpangaji wa Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), Raksha Gadhvi kudaiwa kuuza nyumba aliyokuwa amepangishwa jijini Dar es Salaam na sasa Serikali inapambana mahakamani kuirejesha.
NHC ilifungua kesi Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi kupinga uuzwaji wa nyumba hiyo na mahakama hiyo ikaitupilia mbali kesi hiyo kwa sababu ya muda uliokuwa umepangwa kuisikiliza, ulimalizika kabla haijaisha, uamuzi ambao ni kama unaotoa haki ya umiliki kwa muuzaji na mnunuzi.
Kutokana na uamuzi huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ameingilia na kukimbilia Mahakama ya Rufani, katika jitihada za kuinusuru nyumba hiyo na kuirejesha katika umiliki wa NHC.
AG alifungua shauri la maombi dhidi ya mpangaji aliyeuza nyumba hiyo (Gadhvi), mnunuzi, Jehangir Aziz na NHC, akiomba kuongezewa muda wa kufungua shauri la mapitio, dhidi ya uamuzi huo wa Mahakama Kuu.
Katika shauri hilo la maombi namba 147/01 la mwaka 2022, AG alieleza kuwa uamuzi wa kufuta kesi hiyo ya msingi uligubikwa na kasoro huku akibainisha sababu mbili.
Sababu ya kwanza, AG alieleza kuwa kesi hiyo ya msingi ilifutwa bila kumuunganisha yeye, AG kama mdaawa muhimu, licha ya Mahakama Kuu kutambua marekebisho ya sheria ya mashauri dhidi ya Serikali.
Sababu ya pili, AG alidai kuwa kesi hiyo ilifutwa bila kumpa yeye fursa ya kusikilizwa.
AG katika jitihada hizo amefanikiwa kwa hatua ya kwanza kuishawishi mahakama hiyo, ambayo imeridhia maombi yake ya kumwongezea muda wa kufungua shauri la mapitio nje ya muda, ili kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu.
Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Lilian Mashaka aliyesikiliza maombi hayo, imemtaka AG kufungua shauri hilo ndani ya siku 60 tangu siku ya uamuzi wake.
Jaji Mashaka amesema ni msimamo wa kisheria kuwa kasoro katika uamuzi wa mahakama unaopingwa, ni moja ya vigezo vinavyojenga sababu stahiki ya kuongeza muda wa kufungua shauri la mapitio, marejeo au kukata rufaa.
Hivyo Jaji Mashaka alisema kuwa haki ya kusikilizwa ni kanuni ya msingi ya asili, ambayo inapaswa kuzingatiwa muda wote.
Katika kusisitiza hoja hiyo, Jaji Mashaka amerejea uamuzi wa kesi kadhaa zilizoamuriwa na mahakama hiyo, zilizobainisha kuwa kasoro za kisheria katika uamuzi unaobishaniwa ni sababu tosha ya kuridhia maombi ya nyongeza ya muda.
“Kwa kuongozwa na dondoo hizo, nimeridhika kwamba kasoro zinazodaiwa katika uamuzi unaokusudiwa kupingwa zinaibua sababu nzuri inayohitaji nyongeza ya muda, kumpa mwombaji fursa ya kufungua shauri la mapitio kuzielezea,” anasema Jaji Mashaka katika uamuzi huo.
“Hivyo ninatoa nyongeza ya muda. Mwombaji anapaswa kufungua shauri linalokusudiwa la mapitio ndani ya siku 60 kutoka siku ya kutolewa kwa uamuzi huu.”
Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, Serikali iliwakilishwa na mawakili wa Serikali George Kalenda na Rehema Mtulya, na wajibu wa maombi wa kwanza, Gadhvi na wa pili, Aziz waliwakilishwa na wakili wa kujitegemea, Ali Hamza.
Kufuatia maombi ya mawakili wa Serikali, mahakama iliridhia kuendelea na usikilizaji wa shauri hilo bila kuwepo mjibu maombi wa tatu, NHC.
Umiliki wa nyumba na kesi ya msingi
Wakili Kalenda aliieleza Mahakama kuwa nyumba hiyo yenye hati namba 1821 iliyoko kitalu 1169/199, katika mtaa wa Jamhuri, wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, imekuwa ikimilikiwa na Serikali tangu mwaka 1971.
Alieleza kuwa umiliki wa nyumba hiyo ulitangazwa katika Gazeti la Serikali na Serikali iliikabidhi kwa NHC, ambalo ni shirika la umma lililoanzishwa chini ya Sheria ya Shirika la Nyumba, Sura 295 na NHC iliipangisha kwa wapangaji kadhaa akiwemo mjibu maombi wa kwanza, Gadhvi.
Kwa mujibu wa wakili Kalenda, NHC ilipata taarifa za kuuzwa kwa nyumba hiyo baada ya kuona kuona taarifa ya kubadilisha umiliki kupitia tangazo la gazetini wakati mnunuzi wa nyumba hiyo, Aziz alipoomba hati miliki mpya.
Hivyo NHC iliweka pingamizi kwa Msajili wa Hati kwa kumwandikia barua kumweleza kuwa nyumba hiyo inamilikiwa na Serikali, pia ikafungua kesi ya ardhi Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, dhidi ya muuzaji/mpangaji wake huyo, Gadhvi na Aziz ambaye ni mnunuzi.
Katika kesi hiyo ya ardhi namba 104/2018, NHC ilikuwa ikipinga uuzwaji wa nyumba hiyo, huku ikiomba itangazwe kuwa ndiye mmiliki halali wa nyumba hiyo.
Hata hivyo, mahakama hiyo katika uamuzi uliotolewa na Jaji Salma Maghimbi Juni 3, 2021 iliifuta kesi hiyo kutokana na kuchelewa kusikilizwa baada ya muda uliokuwa umepangwa kuisikiliza kuisha.
Baadaye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kupitia kwa Wakili Mkuu wa Serikali (SG), alipokea hati ya wito katika shauri la maombi namba 3/2022, ili aeleze kwa nini pingamizi lililowekwa katika masjala ya Ardhi kwa manufaa ya NHC katika shauri la ardhi namba 104/2018 kuhusu nyumba hiyo, lisiondolewe.
Baada ya uchunguzi wa kina kuhusiana na hati hiyo ya wito, ndipo AG alibaini kuwepo kwa amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi iliyotupilia mbali kesi hiyo lililokuwa limefunguliwa na NHC, kutokana na kuisha kwa muda uliokuwa umepangwa kulisikiliza.
Alidai kuwa amri hiyo ya kuifuta kesi hiyo ya NHC kulimaanisha kuwapa haki Gadhvi na Aziz ya umiliki wa nyumba hiyo bila uthibitisho na kumnyima mwombaji fursa ya haki ya kusikilizwa ili kuthibitisha haki yake ya umiliki wa jengo hilo.
Hivyo AG alibaini kuwa amri hiyo ya Mahakama ilikuwa imegubikwa na kasoro ambazo zinaweza kutatuliwa kwa njia ya shauri la maombi ya mapitio.
Kwa kuwa muda wa kufungua shauri hilo la mapitio ulikuwa umeshapita, ndipo AG alilazimika kufungua shauri la maombi ya kuongezewa muda wa kufungua shauri la mapitio nje ya muda dhidi ya Ghadhvi, Aziz na NHC.
Akijibu hoja hizo, wakili wa wadaiwa, Hamza aliiomba mahakama ilitupilie mbali shauri hilo akidai kuwa kesi ya msingi iliyofunguliwa na NHC si aina ya kesi ambayo inaangukia kwenye sheria ya mashauri dhidi ya Serikali, bali ilikuwa ni kesi baina ya NHC yenyewe na wajibu maombi wa kwanza na wa pili.
Kuhusu hoja za AG kutokusilizwa, wakili Hamza alidai kuwa katika kesi ya msingi, AG aliwakilishwa kupitia Wakili wa Serikali aliyeiwakilisha NHC.
Hivyo alipinga madai ya AG kuwa kesi hiyo ilifutwa bila yeye kuunganishwa, akidai kuwa AG alikuwa anafahamu kesi hiyo muda wote na hivyo hapakuwa na kasoro katika uamuzi wa Mahakama Kuu kuifuta.