Mmoja adaiwa kufariki dunia kwa kipindupindu Kilindi

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Hashim Mgandilwa
Muktasari:
- Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi alipotafutwa kuzungumzia ugonjwa huo, amesema hana mamlaka ya kuzungumzia suala hilo
Kilindi. Mkuu wa Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Hashim Mgandilwa amesema mtu mmoja amepoteza maisha kwa ugonjwa wa kipindupindu huku wengine 16 wakiambukizwa ugonjwa huo wilayani mwake.
Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Mariam Mgwere alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia ugonjwa huo, amesema hana mamlaka ya kuzungumzia suala hilo, badala yake akaelekeza atafutwe Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO), ambaye pia alisema hawezi kulizungumzia pia, labda ofisi ya mkuu wa mkoa.
Mgandilwa amebainisha hayo leo Jumanne Septemba 10, 2024 wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye mazishi ya mtu huyo aliyefariki dunia kwa ugonjwa huo wilayani Kilindi.
Amedai kuwa kati ya walioambukizwa, 16 wamepatiwa huduma ya matibabu na kupona na kuruhusiwa kurejea kwenye familia zao huku mmoja akiendelea na matibabu katika moja ya vituo maalumu ambavyo vipo wilayani humo.
“Alikuwepo mtu mmoja, alikuwa na ugonjwa wa kutapika na kuharisha, yeye kwa mtazamo wake alihisi amerogwa, hivyo alianza kutafuta matibabu kwa waganga wa kienyeji. Alitoka Kijiji cha Kwamwande akaenda Kilwa na baadaye Lulago katika kutafuta tiba, lakini alifariki dunia,” amesema Mgandilwa.
Mgandilwa amesema wagonjwa hao ni kutoka kata saba wilayani humo.
Amesema hadi sasa zimepita siku 15 tangu kutokea mlipuko wa ugonjwa huo ulioanza Agosti 24, 2024, lakini elimu imeendelea kutolewa ngazi ya jamii ili kuwajengea uelewa wananchi wa kutambua dalili za kipindupindu na hatua za kuchukua ili kutopata madhara.
Mkazi wa Songe Mjini, Wilaya ya Kilindi, Madanga Lusewa ameieleza Mwananchi kuwa jamii ya eneo hilo ilikuwa na hofu kuhusu mlipuko wa ugonjwa huo lakini baada ya Serikali ya wilaya kutoa elimu ya jinsi ya kukabiliana nao wameanza kuchukua tahadhari stahiki.
Kwa upande wa maeneo yenye mikusanyiko, Lusewa amesema wameagizwa kuweka ndoo ya maji ya kunawa mikono, jambo ambalo limetekelezwa na wafanyabiashara na wananchi.
“Naomba elimu iendelee kutolewa kwa wananchi ili wagonjwa wengine wasiongezeke, lakini mkuu wetu wa wilaya, Mgandilwa na viongozi wenzake wamepambana sana na maambukizi hayakuongezeka,” amesema Lusewa.