Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pikipiki kutumika kufuatilia maeneo yenye matishio kiafya

Naibu Balozi na Mkuu wa Maendeleo na Ushirikiano wa Ireland, Mags Gaynor (kulia) na Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzania, Dk Charles Sagoe-Moser (kushoto) wakikabidhi mfano wa ufunguo wa pikipiki kwa Mratibu wa Ufuatiliaji wa Magonjwa na Usimamizi wa Dharura za Afya kutoka Tamisemi, Gerald Manasseh (katikati).

Muktasari:

  • Shirika la Afya Duniani (WHO) na ubalozi wa Ireland, umekabidhi pikipiki 12 kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa ajili ya kutumika kufuatilia maeneo yenye matishio kiafya.

Dodoma. Maofisa 12 wa vituo vya ufuatiliaji wa magonjwa kwenye Mfumo wa Ufuatiliaji na Majibu ya Magonjwa (IDSR) wamepatiwa pikipiki.

Hatua hiyo inalenga kuwawezesha kulinda jamii zinazoishi katika maeneo ambayo magari hayawezi kufika dhidi ya matishio ya kiafya.

Mfumo wa IDSR unahusisha usimamizi wa taarifa kwa kutambua, kutoa taarifa, kupanga vipaumbele na kuthibitisha iwapo tukio ni la kweli au la, na kulifuta endapo halina ukweli.

Shirika la Afya Duniani (WHO) na ubalozi wa Ireland, umekabidhi pikipiki hizo kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Agosti 17, 2024 jijini Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Tamisemi (anayeshughulikia afya), Mratibu wa Ufuatiliaji wa Magonjwa na Usimamizi wa Dharura za Afya kutoka ofisi hiyo, Gerald Manasseh amesema pikipiki hizo ni muhimu kwa kulinda watu dhidi ya matishio ya kiafya.

"Pikipiki hizi 12 zitaboresha programu ya Taifa ya ufuatiliaji wa magonjwa, na kutuwezesha kuthibitisha na kujibu matishio ya kiafya kwa ufanisi zaidi," amesema Manasseh.

Ameishukuru WHO kwa kuwezesha upatikanaji wa pikipiki hizo kutoka ubalozi wa Ireland.

Amesema pikipiki hizo ni za muhimu katika ufuatiliaji wa majanga mbalimbali ya kiafya kama vile Uviko-19 na milipuko ya kipindupindu.

Manasseh amesema pikipiki hizo zitasambazwa katika mikoa saba yenye hatari kubwa ya milipuko ya magonjwa.

Amesema kwa Mkoa wa Dodoma, pikipiki hizo zitapelekwa kwenye wilaya za Mpwapwa na Chemba, wakati mkoani Mwanza zitapelekwa Wilaya ya Ilemela.

Amesema wizara zingine zitakazopata mgawo ni za Nkasi na Sumbawanga zilizoko mkoani Rukwa, ambako ugonjwa wa kipindupindu umekuwa ukijirudia mara kwa mara.

Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam itapatiwa pikipiki kwa ajili ya dharura.

Amesema zitapelekwa pia katika wilaya za Rorya na Butiama mkoani Mara na Mkoa wa Tanga.

Naibu Balozi na Mkuu wa Maendeleo na Ushirikiano kutoka Ubalozi wa Ireland, Mags Gaynor ameipongeza Serikali katika ufuatiliaji na kujenga mfumo endelevu wa afya.

Amesema mabadiliko ya tabianchi na milipuko ya magonjwa huleta mshtuko, hivyo ni muhimu kuendelea na ufuatiliaji ili kuwa tayari ipasavyo.

“Kuna umuhimu wa taarifa za mapema, hasa kutoka kwa jamii,” amesema Gaynor.

Mwakilishi wa WHO Tanzania, Dk Charles Sagoe-Moses amesema kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji ni jambo muhimu katika usimamizi wa dharura za afya kwa ufanisi.

Dk Sagoe-Moses amesema Tanzania imejizatiti kuhakikisha kuwa, ufuatiliaji ni kipaumbele.

"Ningependa pia kuishukuru Wizara ya Afya kwa kutekeleza mpango huu wa kuwafikia watu wote katika jamii na suluhisho za afya," amesema.