Mkurugenzi Jatu afikisha siku 382 rumande, ataka upelelezi ukamilike

Mkurugenzi wa Jatu, Peter Gasaya
Muktasari:
Anakabiliwa na mashtaka mawili, likiwemo la kujipatia Sh5.1bilioni kwa njia ya udanganyifu, kwa madai kuwa fedha hizo ataziwekeza kwenye kilimo ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya JATU PLC, Peter Gasaya (33) ameiomba Serikali ifanye jitihada za haraka ili kukamilisha upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili.
Kufikia leo, Januari 15, 2024, Gasaya, anatimiza siku 382 rumande, kutokana upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Gasaya anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia Sh5.1bilioni kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha kiasi hicho cha fedha, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya JATU, kwa madai kuwa fedha hizo atazipeleka kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.
Mshtakiwa huyo amewasilisha ombi hilo, kupitia wakili wake, Wabeya Kung'e, leo Januari 15, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amiri Msumi, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
"Mheshimiwa hakimu, tunaomba Serikali ifanye jitihada za haraka kukamilisha upelelezi wa kesi hii kwa sababu mteja wangu anaendelea kusota rumande kwa muda mrefu" amedai Wakili Kung'e
Wakili Kung'e, ametoa maelezo hayo muda mfupi baada ya wakili wa Serikali, Eva Kassa kuieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea, hivyo wanaomba tarehe kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, upande wa mashtaka umedai kuwa umepokea ombi hilo na unaendelea kulifanyia kazi.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Msumi aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 29, 2024 itakapotajwa.
Kesi hiyo imesikilizwa kwa njia ya video, huku mshtakiwa akiwa rumande.
Aidha katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa, kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5,139,865,733 kutoka Saccos ya JATU.
Mshtakiwa anadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya JATU kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa sio kweli.
Shtaka la pili ni kutakatisha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es salaam.
Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa JATU SACCOS, alijihusisha na muamala wa Sh5,139,865,733 kutoka katika akaunti ya JATU SACCOS iliyopo benki ya MNB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya JATU PLC iliyopo katika benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.