Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Mke, watoto wasimulia dakika za mwisho mkurugenzi Tanesco

Baadhi ya watoto wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Boniface Gissima Nyamo-Hanga,, Monica, Bitonga na Ghati wakiwa na mama yao (mke wa marehemu) Kashemeile Stanslaus

Muktasari:

  • Nyamo-Hanga pamoja na dereva wake, Muhajiri Haule walifariki dunia usiku wa kuamkia Jumapili, Aprili 13, 2025 baada ya kupata ajali ya gari katika eneo la Nyatwali, wilayani Bunda Mkoa wa Mara.

Dar/Bunda. Kashemeile Stanslaus, mke wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Boniface Gissima Nyamo-Hanga, ameelezea namna alivyoagana na mumewe kabla ya kukutwa na mauti.

Nyamo-Hanga pamoja na dereva wake, Muhajiri Haule walifariki dunia usiku wa kuamkia Jumapili, Aprili 13, 2025 baada ya kupata ajali ya gari katika eneo la Nyatwali, wilayani Bunda Mkoa wa Mara.

Mwili wake utazikwa Jumatano, Aprili 16 nyumbani kwao Bunda, huku mwili wa dereva wake ukitarajiwa kuzikwa kesho Jumanne, Mlandizi mkoani Pwani.

Mke, watoto wasimulia dakika za mwisho bosi Tanesco

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake Oysterbay, jijini Dar es Salaam leo, kulikokuwa na msiba, mke wa mkurugenzi huyo, Kashemeile amesema alipokea taarifa za kifo cha mumewe Jumapili asubuhi akiwa kanisani.

"Nilipigiwa simu, nikaambiwa kuna taarifa Gissima amefariki kwa ajali Bunda. Sikuamini, maana alikuwa Dodoma. Nikaanza kufuatilia," amesema huku akibubujikwa na machozi.

Amesema mumewe alimuaga kuwa anakwenda Dodoma kikazi na hakujua kama angeenda Bunda mpaka pale alipopata taarifa za ajali.

"Sina cha kufanya zaidi ya kumuombea Gissima. Siwezi kumuelezea, kuondoka kwake ni pigo. Alikuwa ni baba na mume mwenye heshima sana kwangu. Aliamini katika elimu, alipenda kila mtoto wake asome," amesema Kashemeile, akibainisha kwamba Gissima ameacha watoto 15.

Mtoto wake wa tano kuzaliwa, Monica Nyamo-Hanga amesema alionana mara ya mwisho na baba yake Januari, mwaka huu.

"Tuliagana, yeye alikuwa anasafiri kikazi. Mimi, siku tatu baadaye nilitakiwa kwenda chuo Malaysia, hivyo akataka tuagane kabisa," amesema Monica.

Amesema saa chache kabla ya kifo cha baba yake, walizungumza kupitia WhatsApp akiwa Malaysia, lakini hakumuambia kama alikuwa na mpango wa kusafiri kuelekea Bunda.

"Nilimtumia matokeo yangu ya semester ya kwanza. Aliyapokea kwa furaha, akaniombea kama mzazi. Kumbe ndiyo tulikuwa tukiagana. Niliamka asubuhi ndipo nikapokea simu ya mama akiniambia baba amefariki," amesema Monica.

Binti yake mwingine, Bitonga Nyamo-Hanga amesema baba yao alikuwa mchapakazi, na ukiachana na utendaji wake Tanesco, nyumbani alikuwa ni baba mwenye upendo mkubwa kwa familia yake.

"Alipenda tusome. Aliamini katika elimu. Mbali na kuwa baba, alikuwa pia mtu wa kawaida, mkarimu na alikuwa mtu wa kujishusha," amemuelezea baba yake.

Mtoto wake wa nne, Ghati Nyamo-Hanga amesema siku ambayo baba yake alipata ajali, alijaribu kumpigia simu bila mafanikio.

"Nilimpigia tu kwa lengo la kumsalimia, hakuwa hewani. Asubuhi ya Jumapili ndipo nikapigiwa simu na mtu wangu wa karibu kuniambia amesikia baba amefariki, akitaka kufahamu ukweli. Zile taarifa zilinishtua, ikabidi nianze kufuatilia na kujua ni kweli. Japo sijui Bunda alikwenda kufanya nini, lakini huenda alikwenda kusalimia mara moja kisha aendelee na kazi," amesema Ghati.

Amesema mara ya mwisho kuzungumza na baba yake ilikuwa ni kuhusu masuala ya shule, akimpongeza kwa kuhitimu shahada ya uzamili.

"Baba alikuwa anaijali sana familia. Upendo wake ni wa tofauti sana. Tutaukosa milele. Alituhimiza na kutuhamasisha kufanya vitu vitakavyotusaidia maishani. Tunaomba moyo wake uendelee kukaa nasi," amesema Ghati kwa huzuni.


Wasemavyo ndugu huko Bunda

Mwananchi pia imefika nyumbani kwa baadhi ya ndugu wa marehemu. Wakizungumza na Mwananchi nyumbani kwao Migungani, mjini Bunda, wamesema wamepoteza nguzo ya familia huku wakidai hawakuwa na taarifa juu ya ujio wake nyumbani.

Kisyeri Gissima amesema enzi za uhai wake, Nyamo-Hanga alikuwa ni mtu mwenye mapenzi na ndugu na jamaa na hakuwa mbaguzi, bali alikuwa na tabia ya kutembelea ndugu mara kwa mara.

"Tulishangaa baada ya kupata taarifa za ajali hiyo. Sisi kama familia hatukujua kama anakuja huku siku hiyo," amesema Gissima.

Kaka wa marehemu, Robert Nyamo-Hanga amesema:

"Mimi naishi Dar es Salaam. Nilipewa taarifa ya msiba na shemeji yangu jana asubuhi. Kwa kweli nilipatwa na mshtuko mkubwa na nilipoteza fahamu. Ndugu yangu amefariki ghafla mno.

“Nimeumia sana na hakutuambia kama angekuja huku nyumbani. Hatuelewi, inatuuma sana," amesema kaka yake huyo.

Robert, ambaye anasema ndiye aliyemlea Nyamo-Hanga tangu utotoni, amesema alikuwa mtu mwenye upendo wa hali ya juu na msikivu siku zote.

Nyamo-Hanga aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo Septemba 23, 2023, akichukua nafasi ya Maharage Chande. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea).

Moja ya kibarua kigumu kilichomkabili baada ya kuingia katika nafasi hiyo ilikuwa kushughulikia changamoto za muda mrefu za umeme nchini – na alifanikiwa.


Eneo la ajali

Ajali iliyokatisha uhai wa Nyamo-Hanga ilitokea eneo la Nyatwali, karibu na geti la Ndabaka la kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Chanzo cha ajali kilitajwa kuwa ni dereva wa gari alilokuwamo Nyamo-Hanga aina ya Land Cruiser, kumkwepa mwendesha baiskeli, kisha kupoteza mwelekeo na kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa mbele yao saa 1:30 usiku. Baada ya ajali hiyo, dereva wa lori pamoja na mwendesha baiskeli walikimbia.


Dereva kuzikwa kesho

Mwili wa Haule, aliyekuwa dereva wa Nyamo-Hanga, utazikwa Kibaha, mkoani Pwani kesho.

Mkurugenzi wa Tanesco Kanda ya Ziwa, Satco Nombo amesema mwili wa Haule ulisafirishwa jana kwenda mkoani Pwani kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika kesho.