Prime
Mkapa aliiongoza Tanzania akiwa na ‘presha sifuri’
Muktasari:
- Julai 24, 2020, Tanzania ilimpoteza Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa; kilikuwa kifo cha ghafla, maana aliumwa kwa muda mfupi, kisha safari yake ya duniani ikagota ukingoni.
Dar es Salaam. Rais wa Tatu wa Marekani, Thomas Jefferson aliwahi kusema: “Hakuna ambaye ataondoka kwenye madaraka ya urais, akiwa na sifa ileile aliyoingia nayo.”
Jefferson, mwishoni mwa urais wake, alimwandikia barua gavana wa zamani wa Carolina Kusini, Edward Rutledge kumweleza hisia zake kwamba urais wenyewe unaharibu hadhi ya kiongozi.
Alisema wadhifa huo huibua chuki kali za kisiasa na Rais kukatishwa tamaa na umma, ni jambo la lazima kutokea.
Alimweleza Rutledge kuwa, bila kujali jinsi kiongozi alivyoongoza, shinikizo lisilo na mwisho la nafasi hiyo hupunguza sifa nzuri aliyokuwa nayo kabla ya kuingia madarakani.
Madhumuni ya barua hiyo, yalikuwa kuonesha uzoefu wake binafsi kipindi anachaguliwa kuwa Rais wa Marekani, baada ya kukaa madarakani na namna umma ulivyokuwa unamtafsiri kabla ya urais.
Zama za kuelekea uhuru wa Marekani Julai 4, 1776, Jefferson aliheshimiwa na umma kwa kuwa mwandishi wa “Azimio la Uhuru.”
Baada ya uhuru, Jefferson alitafsiriwa kama zawadi kubwa ya taifa kwa kuongoza jopo la uandishi wa Katiba ya Marekani iliyoanza kutumika Machi 4, 1789.
Jinsi Marekani ilivyojengwa kitaasisi wakati taifa hilo likiwa changa, sifa nyingi zinamwelekea Jefferson.
Hata hivyo, Jefferson akiwa Rais wa Marekani kwa mihula miwili, 1801–1809, alipitia changamoto kubwa za kisiasa. Alikosolewa vikali na kupingwa.
Aliambiwa aliharibu uchumi hasa kutokana sheria ya kuzuia bidhaa za nje kuingia Marekani (Embargo Act, ya mwaka 1807).
Kutokana na hali hiyo, Jefferson alimwandikia Rutledge kumweleza kuwa rais akishaingia madarakani, hatabaki na heshima aliyokuwa nayo kabla.
Rutledge alikuwa mmoja wa waasisi wa Marekani alikuwa mmoja wa wanajopo 56 waliosaini Azimio la Uhuru.
Tuuelekee muktadha
Julai 24, 2020, Tanzania ilimpoteza Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa. Kilikuwa kifo cha ghafla, maana aliumwa kwa muda mfupi, kisha safari yake ya duniani ikagota ukingoni. Lilikuwa pigo kwa Taifa.
Tanzania ilivuka salama kwa miaka 10, chini ya uongozi wa Mkapa. Angalau hili pekee lingetosha kuumiza moyo kwa msiba huo mkubwa.
Kurejea maneno ya Jefferson kwamba urais huharibu hadhi ya kiongozi. Bila kumpinga, ukweli ni kuwa inaweza kuwa na matokeo ya aina tofauti. Siasa za hovyo zinaweza kumfanya kiongozi mzuri atapakae tope.
Mbaya akaonekana mzuri. Ni siasa na wanasiasa. Uwe mwema na mwenye dhamira njema kiasi gani, wachafuzi wakikuwahi, utazomewa hadi na familia yako.
“Urais humdhihirisha kiongozi,” alisema Michelle Obama mke wa Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama. Kiongozi mbovu aliyepambwa na kutumainiwa na wengi, baada ya kukalia kiti, anaweza kufanya madudu yanayoweza kumdhihirisha jinsi alivyo.
Yule asiyeaminiwa au hata kudhaniwa, akafanya kazi iliyotukuka. Urais ni nafasi. Inategemea mwenye kuupata anautumiaje. Jumlisha siasa zinazomzunguka.
Mkapa ni mmoja wa wale marais ambao hawakutumainiwa na wengi. Miaka 31 iliyopita, Mkapa hakuwa jina lililokuwa na matarajio makubwa kwamba angekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alikuwa waziri mwandamizi. Alisheheni sifa lukuki za kiuongozi na kiutendaji, hakuwa maarufu. Mtindo wake wa maisha ulisababisha.
Mkapa, mtendaji zaidi. Mwanasiasa bila makuu ya kisiasa. Hakuwa mtu wa makundi. Alichomoza, akashinda tiketi ya CCM. Waliokuwa na majina makubwa hawakufurukuta.
Akawa mgombea urais wa CCM, badala ya kikundi fulani cha wana-CCM. Nguvu yake ya ushawishi dhidi ya wagombea wa vyama vya upinzani haikuwa kubwa. Ushindi wake ulikuwa wa CCM zaidi kuliko wake binafsi.
Hii ilisababisha urais wake usiwe na msongo wa presha za wanakikundi, ambao wangejiona wao ndiyo walimwezesha kushinda kiti. Hakudaiwa nao.
Watu hawakuwa na matarajio makubwa juu yake, hiyo ilisababaisha afanye kazi yake kwa utulivu akitii maono na kutekeleza Ilani ya chama chake cha mapinduzi.
Presha sifuri
Hakika, kama angekuwa maarufu sana wakati anaingia madarakani, maana yake matarajio yangekuwa makubwa, hiyo ingepandisha presha ya urais wake.
Wafanyabiashara wangeweka fedha ashinde, wanasiasa wenzake wangembeba juu kumpeleka Ikulu, urais wake ungekuwa katikati ya shinikizo kubwa.
Katika kitabu chake, “My Life, My Purpose,” “Maisha Yangu, Kusudi Langu,” Mkapa ameeleza jinsi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alivyomwona mwenye uthubutu mkubwa kwa namna alivyowaweka nje ya Baraza la Mawaziri, wanasiasa waandamizi waliokuwa wabunge, Cleopa Msuya na John Malecela. Ndiyo, Mkapa alikuwa na presha sifuri, kwa hyo hata wasaidizi wake aliwateua bila shinikizo.
Ni kwa sababu urais wake haukuwa na presha, ndiyo maana alijikita kuwatumikia Watanzania na kufanya mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya miundombinu, bila kuvutwa shati.
Aliikuta nchi haina fedha. Haijiwezi. Haikopesheki. Akaja na utambulisho wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Ukafuata utambulisho wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Mkapa akatangaza kuwa ulikuwa wakati wa Watanzania kufunga mikanda.
Waliokuwepo wakaona maisha yalikuwa magumu. Wakaligeuza jina lake. Ukosefu wa fedha ukaitwa ‘ukapa.’Mtu akiwa hana fedha, anasema ‘nina ukapa.’
Kwa kuwa hakuwa kwenye shinikizo, hakuogopa. Alianzisha hotuba za kila mwezi akawa anahutubia Taifa kuwaeleza hali halisi. Kwa ugumu. Na kwa neema. Alijitambua alikuwa mtumishi. Mabosi wake ni Watanzania. Hivyo, aliwapa mrejesho wa kila kitu, pindi ulipofika mwisho wa mwezi.
Miaka miwili ya urais wake, Tanzania ikaanza kufaidi matunda ya maono na uwekezaji wake mkubwa. Nchi ikasamehewa madeni. Taasisi za kifedha za IMF na Benki ya Dunia, zikaiingiza Tanzania kwenye mpango wa kuzisaidia nchi maskini zinazoelemewa na mzigo wa madeni.
Unafuu wa misamaha ya madeni, ukasaidia nchi ipate ahueni.
Ghafla, Mkapa alianza kuzindua barabara na madaraja. Taifa likaanza kuunganishwa kwa lami. Alianzisha Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (Mkukuta).
Oktoba 2004, Serikali ya Tanzania iliingia makubaliano na Serikali ya Norway kuhusu kufanya mapitio ya biashara na rasilimali za watu wa chini ili kuzifanya ziwe rasmi. Mapitio hayo ndiyo yaliyozaa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (Mkurabita).
Kuhusu Mkumkuta, Rais Mkapa alikaa na baraza lake Hoteli ya Ngurdoto, mtaalam kutoka Peru, Jens Clausen akawapiga msasa mawaziri kuhusu njia na mbinu sahihi za kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa mazingira ya Kitanzania.
Clausen pia ndiye alikuwa kiongozi wa timu ya wataalamu waliofanya mapitio ya rasilimali na biashara za Watanzania kisha kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuzirasimisha.
Rais Mkapa alikuwa na maono makubwa kuhusu kuikwamua elimu nchini. Alianzisha Mpango ya Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Elimu ya Sekondari (MMES).
Kila kilichofanyika wakati wa urais wake, Mkapa alikitetea. Aliwatetea mawaziri wake. Alikuwa kiongozi jasiri, mwenye kujiamini. Hiyo ni kwa sababu alijua wajibu wake ulikuwa kuwatumikia Watanzania. Si aina fulani ya watu wenye masilahi.
Ni miaka sita imepita tangu Mkapa alipofariki dunia. Kumbukumbu ambayo inapaswa kubaki kwenye vichwa vya Watanzania, ni namna rais wao alivyotekeleza majukumu yake bila kandokando. Hukusikia wakati akiwa rais, akisifiwa yeye binafsi. Alijua yeye ni mtumishi, na alilitumikia taifa.
Kuna wakati, Rais madarakani akiwa Dk John Magufuli, Mkapa alikosoa mtindo wa kusema, “Serikali ya Magufuli,” alitaka isemwe, “Serikali ya CCM,” kwa sababu ndicho chama kilichokabidhiwa dhamana ya uongozi na Watanzania. Mkapa hakuwa muumini wa sifa binafsi, ndiyo maana alitenda mengi kwa uthubutu mkubwa, tena bila presha.
Kiongozi akipenda sana kusifiwa binafsi, watu huona fursa, kwa hiyo huanza kumjaza sifa za uongo na kweli ili kumteka.
Naye huona wanaomsifia wanastahili malipo ya fadhila. Mwisho, hujikuta katikati ya presha ya kulipa fadhila. Wanaomsifu ni wengi, je alimpe nani na amwache yupi?
Miaka sita tangu kifo cha Mkapa, itoshe kumkumbuka kama binadamu mwenye mawazo huru na muwazi. Hakusita kuzungumza kwenye majukwaa ya kimataifa na kukosoa mitindo ya viongozi wengine Afrika.
Ndani ya kitabu chake, “My Life, My Purpose,” Mkapa alieleza mambo mengi ambayo hakuyapenda, yaliyofanywa na mrithi wake, Jakaya Kikwete.
Mathalan, aliunda Wizara ya Ushirika alipokuwa madarakani. Kama alivyoandika kwenye kitabu chake, wizara hiyo aliianzisha baada ya utafiti na ilikuwa na manufaa makubwa kwa nchi.
Kikwete hakuiendeleza. Mkapa alieleza wazi jinsi ambavyo hakupendezwa na uamuzi huo.
Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Costa Mahalu, alishitakiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya ofisi. Kwa vile Mkapa alikuwa ndiye Rais wakati Mahalu alipokuwa balozi, alikwenda mahakamani kutoa ushahidi. Hiki ni kipimo kingine kuwa hakuwa na presha na maisha yake ya urais hata baada ya kutoka madarakani. Angekuwa na hofu, asingekwenda mahakamani.
Mkapa kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ni kielelezo kwamba aliheshimu mifumo ya kitaasisi. Alitambua kwamba yeye hakuwa mkubwa mbele ya Mahakama. Vinginevyo, angechagua kukaa nyumbani na kupiga simu ili kushawishi na kuingilia uhuru wa mahakama. Mkapa alikuwa muumini wa utawala wa sheria.
Mkapa akiwa kaburini kwa miaka sita iliyotimia, inakumbusha kuhusu binadamu na ubinadamu. Ndani ya kitabu chake, amekiri makosa kipindi cha utawala wake, kama mauaji ya kisiasa, Zanzibar, Januari 26 na 27, 2001, vilevile ukwapuaji wa fedha Benki Kuu kwenye akaunti ya madeni ya nje, Epa, Sh133 bilioni, nyakati za mwisho za utawala wake.
Alikubali makosa ya namna ubinafsishaji ulivyofanyika, kisha akatetea uamuzi wenyewe kwamba ulikuwa sahihi.
Mkapa alitambua hakuwa malaika, alikuwa binadamu, ambaye alijitahidi kutenda mema, ndiyo maana pale alipogundua alikosea alikiri, halafu alitetea alipojiona alikuwa sahihi.
Endelea kupumzika Mzee Benjamin William Mkapa. Tanzania ni bora leo kwa sababu ya namna ulivyojitoa kulihudumia Taifa katika ngazi mbalimbali, mpaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uliiongoza nchi bila presha. Ukaondoka ofisini na heshima kubwa kuliko uliyoingia nayo, kinyume na alivyosema Jefferson kuwa urais hushusha hadhi ya mtu.