Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mkanganyiko wa ushahidi ulivyomtoa jela baba aliyehukumiwa kwa kumbaka mwanaye

Muktasari:

  • Baba huyo, mkazi wa Majengo Kibaigwa, wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, alidaiwa kumbaka binti yake mwenye umri wa miaka 13, na ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo hauungi mkono shtaka, kwani akihojiwa polisi alidai kubakwa, ila wakati akitoa ushahidi mahakamani alidai kubakwa na kulawitiwa.

Arusha. Mahakama ya Rufani imemuachia huru baba aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, fidia ya Sh100,000 na viboko sita kwa kumbaka mtoto wake aliyekuwa na umri wa miaka 13.

Baba huyo, mkazi wa Majengo Kibaigwa, wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, alidaiwa kumbaka binti yake kati ya Desemba 13 hadi 16, 2021.

Hii ni rufaa yake ya pili, ambapo rufaa ya awali aliikata Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, ambayo Juni 22, 2023 ilibariki adhabu aliyopewa na kutupilia mbali rufaa yake.

Uamuzi wa Mahakama ya Rufani umetolewa Machi 28, 2025 na majaji watatu ambao ni Rehema Mkuye, Lucia Kairo na Gerson Mdemu walioketi Dodoma. Majaji hao, baada ya kupitia hoja za rufaa, walibaini shtaka hilo halikuthibitishwa bila kuacha shaka, ikiwamo kuwa na utofauti kati ya shtaka na ushahidi.

Ushahidi huo ni pamoja na ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo, ambao hauungi mkono shtaka na haukuwa wa kuaminika, kwani akihojiwa polisi alidai kubakwa, ila wakati akitoa ushahidi mahakamani alidai kubakwa na kulawitiwa.


Msingi wa rufaa

Baba huyo alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kongwa akikabiliwa na kosa la ubakaji, akidaiwa kumbaka mwanaye ambaye katika hukumu hiyo amefichwa utambulisho wake na kutambulika kama GHK.

Ilidaiwa siku ya tukio baba huyo akiwa ofisini kwake alimpigia simu GHK, aliyekuwa nyumbani akimtaka aende ofisini akamsaidie kazi.

Ilidaiwa akiwa njiani alikutana na vijana wawili katika barabara ya Mroma, baba yake akiwemo, ambaye alimnyang’anya simu na kumuamuru amfuate.

GHK alitii, walielekea nyumbani hadi kwenye chumba cha mtoto huyo, ambapo mrufani alimvua nguo na kujivua na baada ya hapo akaingiza uume wake sehemu zake za siri.

Kwa mujibu wa kumbukumbu, ilidaiwa GHK alikuwa katika mzunguko wake wa hedhi, hivyo baba yake akamlawiti, kisha akafunga mlango na kumuacha chumbani, ilidaiwa aliendelea kumfanyia kitendo hicho mara kwa mara.

Ilidaiwa tukio hilo liliripotiwa Kituo cha Polisi, kisha GHK akapelekwa Kituo cha Afya Kibaigwa, ambapo shahidi wa tano, Pius Gumbo, alimfanyia uchunguzi wa kimatibabu na kukutwa ana michumbuko sehemu za siri, na mrufani kukamatwa.

Ilidaiwa baada ya kukamatwa na kuhojiwa alikiri kutenda kosa hilo, licha ya kukiri alikana kutenda kosa hilo mahakamani, ambapo Mahakama ya Wilaya ya Kongwa ilizingatia ushahidi wa GHK na kumtia hatiani mrufani.


Rufaa ya kwanza

Katika rufaa ya kwanza, Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma ilitupilia mbali rufaa yake na kusema upande wa mashtaka ilithibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.


Rufaa ya pili

Katika Mahakama ya Rufani, baba huyo alikuwa na sababu 12, huku akiwa hana uwakilishi wa wakili na upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na mawakili wawili wa Serikali waandamizi wakiongozwa na Patricia Mkina.

Miongoni mwa sababu hizo ni Jaji alikosea kushikilia uamuzi wa Mahakama ya Wilaya wakati upande wa mashtaka ulishindwa kudhibitisha shtaka dhidi ya mrufani bila mashaka yoyote.

Mahakama mbili zilikosea kisheria kushindwa kutambua hati ya mashtaka ilikuwa na dosari, kwani ilionyesha kosa ni ubakaji, ila GHK aliiambia mahakama alibakwa na kulawitiwa.

Sababu nyingine ni Jaji alikosea kisheria kuunga mkono uamuzi wa Mahakama ya Wilaya bila kuzingatia Hakimu alimtia hatiani wakati usomaji wa maelezo ya awali ulifanyika kinyume na kifungu cha 192 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hivyo kesi na hukumu ilikuwa ubatili.

Nyingine ni mahakama mbili zilikosea sana kisheria kwa kushindwa kuzingatia kifungu cha 10(3) cha CPA, ndiyo maana ushahidi uliotolewa na mwathirika na shahidi wa tano ulipingana.


Uamuzi Majaji

Jaji Mdemu amesema kuhusu hoja ya utofauti kati ya shtaka na ushahidi, amesema maelezo ya kosa ilikuwa ni ubakaji na daktari aliyemchunguza mwathirika wa tukio hilo hakusema iwapo alimchunguza katika njia ya haja kubwa.

“Katika kipindi chote cha shauri hilo, rekodi iko kimya iwapo shtaka lilirekebishwa kwa mujibu wa kifungu cha 234 (1) cha CPA kwa jambo hilo, shtaka la ubakaji halikuthibitishwa kwa sababu upande wa mashtaka umeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuthibitisha kesi bila shaka yoyote,” amesema.

Akinukuu rufaa ya jinai namba 736 ya 2023 ya Ladislaus Baltazar Kalaba dhidi ya Jamhuri katika ukurasa wa 8 wa hukumu hiyo, Mahakama iliona kwamba:

“Tunaanza na shtaka kwa sababu ndio msingi wa kesi. Katika haki ya jinai ni wajibu kwa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wa kuunga mkono shtaka. Wakati wowote ushahidi hauendani na shtaka, hiyo ni tofauti kati ya ushahidi na shtaka na ina athari mbaya kwa upande wa mashtaka, kwani shtaka linabaki bila uthibitisho."

Jaji Mdemu amesema mbali na utofauti kati ya shtaka na ushahidi, wanadhani ushahidi wa mwathirika haukupaswa kutegemewa kwa msingi wa kutiwa hatiani kwa sababu alitoa ushahidi wa kupotoka juu ya alichoripoti polisi na kusababisha msingi wa shtaka la ubakaji na kile alichoshuhudia mahakamani kwamba alilawitiwa pia.

Amesema mahakamani shahidi huyo alidai kubakwa na kulawitiwa, ila polisi alidai kubakwa na kuwa alithibitisha zaidi kuwa alichunguzwa sehemu zake za siri na njia ya haja kubwa, taarifa ambayo ina tofauti kubwa na ya shahidi wa tano ambaye hakueleza kuhusu uchunguzi sehemu ya haja kubwa.

Jaji Mdemu amesema msimamo wao katika uchambuzi uliotangulia wa ushahidi wa upande wa mashtaka unaonekana kutikisa uaminifu wa ushahidi wa GHK na kuwa Mahakama mbili hapa chini zilipaswa kuzingatia ushahidi wake.

“Mwisho wake unatupeleka kwenye kupata kwamba upande wa mashtaka kesi haikuthibitishwa bila shaka yoyote, tunaruhusu rufaa na hukumu iliyotolewa dhidi ya mrufani kwa kosa la ubakaji inafutwa na tunaamuru aachiliwe kutoka kizuizini labda kama ameshikiliwa kwa sababu zingine halali,” amehitimisha.