Mkaa unavyoweza kuokoa maisha ya aliyekunywa sumu

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule akizungumza na waandishi na wahariri wa vyombo vya habari wakati akifungua mafunzo yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala la Kazi (OSHA) jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Aprili 19, 2024. Picha na Pamela Chilongola
Dar es Salaam. Ikiwa mtu amekunywa sumu ya vidonge, inashauriwa njia sahihi ya kumpatia huduma ya kwanza ni kwa kumpa mkaa atafune badala ya maziwa, ili kuzuia kifo kabla ya kupelekwa hospitali kwa matibabu zaidi.
Ushauri huo umetolewa na mtaalamu wa huduma ya kwanza anayeeleza kuwa anaweza kupewa mkaa atafune au asagiwe na kisha kulamba unga wake, kwani unasaidia kufyonza sumu iliyopo mwilini.
Akizungumza leo Ijumaa Aprili 19, 2024 wakati wa mafunzo kuhusu usalama na afya mahala pa kazi kwa waandishi na wahariri wa habari, yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), mkufunzi wa huduma ya kwanza, Mutesw Meda amesema watu wengi katika jamii wana dhana kwamba mtu aliyekunywa sumu anaweza kupewa huduma ya kwanza kwa kupewa maziwa.
“Hii dhana haifanyi kazi kwa aina zote za sumu. Mtu aliyekunywa vidonge vingi anaweza kupatiwa huduma ya kwanza kwa kupewa mkaa atafune au asagiwe na apewe unga wake.
Hata hivyo, amesema mtu aliyekunywa sumu za asidi ama tindikali, anaweza kupewa maji mengi au maziwa ambayo ni bora zaidi.
Kuhusu mtu aliyekunywa mafuta ya petroli au mafuta ya taa, anashauri asipewe kitu chochote, badala yake awekwe sehemu yenye hewa na kisha awahishwe hospitali.
“Mtu aliyekunywa petroli au mafuta ya taa, akipewa maji, yatasababisha apate shida kwenye mfumo wa upumuaji… Pia ili kuepuka changamoto hii tunashauri watu waepuke kuweka kemikali zenye sumu kwenye chupa za maji,” amesema.
Pia amesema tiba ya kutafuna mkaa inaweza kumsaidia mtu aliyekunywa pombe kupita kiasi, kwani inasaidia kwa muda mfupi kukata ulevi.
Aliyegongwa na nyoka
Mkufunzi huyo amesema kwa mtu aliyegongwa na nyoka, haipaswi kumfunga kamba eneo la juu ya jeraha, kumchanja au kumfunga mawe, kwani njia hizo hazimsaidii, bali mgonjwa asafishwe jeraha kwa maji safi na sabuni, kisha apelekwe hospitali.
“Hizi dhana zipo sana kwenye jamii, lakini hazisaidii chochote…. Mtu aliyegongwa na nyoka akishapewa huduma ya kwanza, kama amegongwa mkononi uelekezwe chini, kama mguuni ni vizuri akabebwa,” amesema Meda.
Pia amesema mtu aliyeng’atwa na tandu au nge ambao sumu yao haitofautiani sana na ya nyoka, anatakiwa kupatiwa huduma ya kwanza kwa kusafishwa jeraha, kisha kumwagia ‘vinegar’ kwenye jeraha na kukanda jeraha kwa kutumia barafu iliyofungwa kwenye kitambaa.
Kumsaidia mwenye shinikizo la damu
Mkufunzi huyo amesema mtu mwenye changamoto ya ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, akiwa katika hali mbaya anaweza kupatiwa huduma ya kwanza kwa kupewa dawa ya Asprini ambayo inasaidia kushusha presha.
Kauli ya DC kwa OSHA
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule ameitaka OSHA kuwafuatilia wamiliki wa viwanda wasiofuata sheria ya usalama wa kazi, ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Akifungua mafunzo hayo, Mtambule amesema OSHA wanatakiwa wawe wakali kwa wamiliki wa viwanda wanaovunja sheria hiyo, ikiwemo kutiririsha maji machafu yenye kemikali ili wachukuliwe hatua.
Pia amesema wakala huo unatakiwa kuwasajili wamiliki wa viwanda kwenye mfumo ya kielektroniki, ili kuwabaini wasiofuata sheria wachukuliwe hatua.
"Wawekezaji wameongezeka katika wilaya ya Kinondoni kuna viwanda zaidi ya 150. Hii inatokana na Serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, hivyo jukumu la OSHA ni kuhakikisha usalama unazingatiwa," amesema Mtambule.
Pamoja na hayo, mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi kuhakikisha wanajikinga na magonjwa ya mlipuko, ikiwemo ya kuhara kutokana na mvua zinazoendelea.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema miaka mitatu iliyopita maeneo ya kazi yaliyosajiliwa yalikuwa zaidi ya 3,000, lakini sasa yameongezeka na kufikia zaidi ya 11,000.
Amesema hali hiyo inatokana na ukuaji wa uchumi, hivyo watu hao kulipa kodi ambayo inasaidia kutengenezwa miundombinu ikiwemo kujenga shule na hospitali.
"Maeneo ya usajili ya kazi yakiongezeka idadi ya usajili inaongezeka na uchumi unakua, hivyo tumeona kwa miaka mitatu uwekezaji umeongezeka," amesema Mwenda