Miswada sheria za uchaguzi haijajibu kiu ya Watanzania

Muktasari:
- Miswada iliyopelekwa bungeni ni pamoja na wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023, muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023.
Dar es Salaam. Baadhi ya wadau wa siasa wamesema miswada ya Sheria za Uchaguzi na Vyama vya siasa iliyopelekwa bungeni wiki iliyopita, bado haijajibu kiu ya Watanzania ya kuwa na Tume huru ya uchaguzi na mazingira sawa ya uchaguzi.
Wametoa maoni hayo leo Novemba 15 walipokuwa wakichangia Mwananchi Space ulioandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) ukibebwa na mada isemayo ‘Nini maoni yako juu ya miswada ya sheria za uchaguzi iliyopo bungeni.’
Akichangia mada hiyo, mdau wa Siasa Begga Richard Watanzania wanataka kuona tume huru ya uchaguzi, ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano hatakuwa akiuteua viongozi na watendaji wa tume hiyo.
“Nilitarajia kuona muswada ukisema tume inaajiri watu wake ambao ni huru wenye uwezo wa kusimamia uchaguzi bila kupata maelekezo sehemu nyingine,” amesema.
Kwa upande wake Nolasco Kaitira amefananisha usawa unaotakiwa katika mazingira ya uchaguzi na mchezo wa mpira wa miguu ambayo mwamuzi anapaswa kutofungamana na upande wowote.
“Ni kama vile Simba na Yanga wakiwa uwanjani halafu mwamuzi akatoka upande mmoja wa timu inaondoa usawa ya watu kuhisi kuwa kitakachopatikana itakuwa halali.
“Inawezekana CCM huwa wanashinda uchaguzi lakini mazingira yaliyopo ni kwamba tunacheza na timu ambayo wana mwamuzi, hivyo inakuwa ni ngumu sana kuamini hata zile rafu zinazotokea uwanjani kuwa zinafanyika katika hali ya usawa,” amsema.
Hata hivyo, ameshukuru kwa kutolewa fursa ya kufanyika marekebisho maana mwanzoni kulikuwa hakuna nafasi ya wananchi kupeleka mapendekezo.
“Kwa maoni yangu naona mkurugenzi wa tume ya uchaguzi apatikane kwa uwazi, vigezo viwekwe na watu wote waweze kuomba kazi atakayeshina afanyiwe mahojiano na baada ya hapo ndiyo apelekwe kwa rais kupata baraka.
“Pia tume isitokane na chama wala serikali moja kwa moja hii itafanya wasiende kulinda kura za bosi wao wakiwa watumishi wa serikali au ushindi wa chama chao kama ni watu wa chama tawala napendekeza tume wawe watu huru,” amesema.
Awali akichokoza mada hiyo, mhariri wa siasa wa gazeti la Mwananchi, Peter Elias amesema tangu awali maoni ya wadau yalilenga kupata mazingira ya haki katika uchaguzi.
Amesema miongoni mwa mambo yaliyopendekezwa kwenye mswada huo ni pamoja na wajumbe wa tume kuomba kazi, na jambo la pili ni wagombea kupewa haki sawa kwenye vyombo vya habari hasa vya umma.
“Kitu ambacho hatujakiona kwenye mswada huu ni wakurugenzi kuendelea kuwa wasimamimizi wa uchaguzi, Tume iwe na wasimamizi wake wenyewe watakaofanya kazi kuamzia majimboni na kwenye vituo vya uchaguzi jambo linalopiunguza Imani kwa vyama vya siasa,”amesema
Amesema kwa maoni yake anaona kuna hatua inayopigwa ingawa hatujafika pale tunapopataka, ikiwemo baadhi ya mambo yanayopendekezwa na wadau kutozingatiwa.