Misungwi wafunga maduka wakilalamikia ushuru

Sehemu ya wafanyabiashara waliogoma wilayani Misungwi, Mwanza
Muktasari:
Wakizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Machi 22, 2024 wafanyabiashara hao wamesema mbali na kukusanywa kiholela., pia wanadai wanatozwa kiwango kikubwa nje na utaratibu wa leseni zao.
Mwanza. Baadhi ya wafanyabiashara wilayani Misungwi mkoani Mwanza wamesitisha huduma za maduka yao kwa kile wanacholalamikia ushuru wa huduma unakusanywa pasipo utaratibu maalumu.
Wakizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Machi 22, 2024 wafanyabiashara hao wamesema mbali na kukusanywa kiholela., pia wanadai wanatozwa kiwango kikubwa nje na utaratibu wa leseni zao.
"Tumeingiliwa na suala la service levy, leseni unalipia Sh100, 000 unaambiwa ushuru wa huduma ni Sh200, 000 tunashindwa kuelewa huu ushuru unakuwaje.
“Kwa kweli hatuelewi huko nyuma tulielewa ushuru huo huwa unalipia asilimia 0.03 ya leseni ya biashara, lakini leo hii tunashindwa kuelewa," amesema Ibrahim Manyasi, mkazi na mfanyabiashara katika soko la Misungwi.
Akiunga hoja hiyo, Jeni Batholomeo, mfanyabiashara wa duka la nguo Misungwi amesema wanashindwa kuelewa utaratibu wa ukusanyaji wa ushuru huo, hali inayosababisha wengi wao kukamatwa pindi wanaposhindwa kulipa kutokana na gharama yake kuwa kubwa zaidi ya leseni yake.
"Hii imekuwa ni uonevu halafu wanasubiria wakati wa sikukuu ndo wanakuja kufungia watu biashara wakitegemea sisi familia zetu tunalisha nini?
“Tunaomba mkurugenzi aliangalie hili suala hata kama sio yeye basi mkuu wa Mkoa wa Mwanza atusaidie maana sisi wafanyabiashara wa Misungwi tunanyanyasika," amesema Jeni.
Akizungumzaia malalamiko hayo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Deogratius David amesema wamekubaliana kuendeleza mgomo huo mpaka Jumatatu Machi 25, 2024 pindi wakikutana na uongozi wa wilaya na kutatua changamoto hiyo.
"Sisi tuna changamoto ya ushuru wa huduma kiwango kinachotozwa ni kinyume cha utaratibu.
“Hapa kuna wafanyabiashara wakubwa na wadogo sasa mfanyabiashara mdogo anatozwa tozo kubwa ambayo ni kinyume cha utaratibu. Unakuta biashara ni ndogo lakini anaambiwa alipe Sh200,000," amesema David.
Akizungumza na wafanyabiashara hao Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi, Abdi Makange amewaomba wafanyabiashara hao kufungua maduka yao, huku akiahidi kuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo atakutana nao Jumatatu Machi 25, 2024 kwa ajili ya kusikia kilio chao.
"Kuanzia sasa nimesitisha hilo fungueni maduka yenu, halmashauri tutakuwa na kikao na Mkurugenzi baaada ya kurudi tupeane elimu na tuone namna gani ya ukusanyaji wa hiyo Service levy.
“Lazima tukubaliane suala la kulipa kodi ni lazima ila kwa utaratibu bila kumuonea mtu, kumnyanyasa au kutumia mabavu," amesema Makange.
Mbali na kauli hiyo kutolewa bado wafanyabiashara hao wameendelea na mgomo wao na kufanya maandamano wakihamasisha wafanyabiashara wengine kugoma.
Hata hivyo, maandamano hayo yalikomeshwa mara baada ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, Yesaya Sudi kuzungumza nao juu ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amosi Makalla kuridhia kukutana nao kesho Jumamosi.
"Kero hapa zipo tatu ya kwanza ushuru wa service levy, ya pili elimu haijatolewa na la tatu mmesema kauli na ubabe hayo mambo matatu yapo kwa kila mmoja, ndio maana mimi nikasema Serikali yenu ni sikivu na huyo mnayesema sio mwisho ndio maana Mkuu wa Mkoa akasema waambie nimepokea na nitakuja kesho," amesema.