Mirungi yadaiwa kuponza askari polisi wawili Same

Moshi/Same. Askari wawili wa Jeshi la Polisi wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro, wanashikiliwa mahabusu ya polisi wilayani humo, kwa zaidi ya wiki moja sasa kwa tuhuma za kwenda kinyume na mwenendo mwema wa Jeshi hilo.
Vyanzo mbalimbali kutoka wilayani Same na ndani ya jeshi hilo, zilidai askari hao walikamata basi lililokuwa na mirungi, likiisafirisha kwenda jijini Dar es Salaam na kuliachia kwa makubaliano ya kutumiwa fedha.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa (pichani) alipoulizwa na gazeti hili jana alikiri kushikiliwa kwa askari hao kwa madai ya utovu wa nidhamu kama ilivyo utaratibu wao wa jeshi, bila kuweka wazi utovu walioufanya.
“Ni kweli tunawashikilia kwa utovu wa nidhamu. Kawaida askari akienda kinyume na utaratibu na kanuni za Jeshi la Polisi, tuna mashitaka yetu ya kijeshi,”alisema RPC Maigwa bila kufafanua walikamatwa lini na kwa kosa gani.
Mkoa wa Kilimanjaro ni moja ya mikoa inayotikiswa kwa biashara haramu ya dawa za kulevya aina ya mirungi, ambayo sehemu kubwa inaingizwa kutokea Kenya ambako biashara hiyo ni halali.
Taarifa kutoka vyanzo vyetu wilayani Same, ambalo ni eneo linalolima zao hilo, zinadai wiki mbili zilizopita askari hao wawili wakiwa na askari wenzao, walipekua basi linalofanya safari kati ya Moshi-Dar es Salaam na kukuta shehena hiyo ya mirungi, lakini hawakuwashtua askari wenzao waliokuwa wakikagua mabasi mengine.
Badala yake, taarifa hizo zinadai walichukua namba ya kondakta na dereva na kuliachia basi hilo kwa makubaliano kuwa baada ya kufikisha mzigo kwa mteja jijini Dar es Salaam, wangewatumia ‘fungu’ lao, lakini hata hivyo inadaiwa haikuwa hivyo.
Baada ya kuona hawajatumiwa fungu lao, inadaiwa walianza kumsumbua kwa simu kondakta wa basi hilo hadi akaamua kuwazimia simu, ndipo wakaanza kumsumbua dereva wakitaka watumiwe fungu lao.
Hata hivyo, vyanzo vilidai dereva naye hakutoa ushirikiano na ndipo walipotafuta namba ya simu ya mmiliki wa mabasi hayo, ambaye alikataa kufahamu jambo hilo na ndipo walipoanza kumpa vitisho kuwa wasipopata fedha, wangemkomoa kwa kukamata mabasi yake.
“Kuona hivyo huyo mmiliki tunaambiwa aliamua kupanda juu (makao makuu ya Polisi) ambapo aliwasilisha lalamiko lake na kuwasilisha sauti alizowarekodi pamoja na SMS (ujumbe mfupi) walizokuwa wakimtisha,”kilidai chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa kigogo mmoja wa makao makuu, baada ya kupokea ushahidi huo, aliwasiliana na viongozi wa jeshi hilo mkoa wa Kilimanjaro na kuwaagiza kuwakamata askari hao na kuwafungulia mashitaka ya kijeshi.