Mirathi inavyowaingiza ndugu katika vita ya mali Arumeru

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amri Mkalipa akizindua kampeni ya msaada wa kisheria ya 'Samia Legal Aid ' katika Wilaya ya Arumeru katika kata ya Malula
Muktasari:
- Kampeni ya Samia Legal Aid imeanza kutoa msaada wa kisheria ili kupunguza migogoro hiyo. Wakili Fauzia Akonay asisitiza umuhimu wa wosia na cheti cha kifo katika mirathi.
Arusha. Migogoro mingi ya ardhi katika Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, imebainika kuhusisha ndugu wanaogombania mali za urithi, huku masuala ya usawa wa kijinsia yakipuuzwa.
Tatizo hilo limechangiwa na wengi wao kushindwa kuanzisha mchakato wa mirathi baada ya kufiwa, hali inayosababisha kupoteza haki zao za urithi.
Ili kupunguza migogoro hii, wazazi na walezi wanahimizwa kuandika wosia wa urithi mapema wakiwa hai. Hatua hii itawezesha ugawaji wa mali kufanyika kwa haki, kusaidia wanufaika kupata haki zao kwa urahisi, na kuzuia migogoro ya baadaye.
Hayo yamebainika katika uzinduzi wa siku 10 za msaada wa kisheria kwa wananchi, inayotekelezwa na wataalamu wa masuala ya kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria chini ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Rais Samia, inayojulikana kama Samia Legal Aid Campaign, iliyoanza leo, Jumatatu, Machi 31, 2025.
Akizindua kampeni hiyo, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amri Mkalipa, amesema tatizo kubwa katika wilaya yake ni migogoro mingi ya ardhi, hasa za mirathi, huku ndugu wakiwa wahusika wakuu.
"Migogoro mingi unakuta ndugu ndiyo wanagombania mirathi. Mfano, kaka na dada zake wanagombania mali za marehemu wazazi wao, au wakati mwingine ni watoto wanagombana na wajomba na mashangazi, kisa mali za kaka au baba yao. Migogoro kama hiyo ndiyo maana hata usuluhishi wake unakuwa mgumu," amesema Mkalipa.
Ametumia nafasi hiyo kuishukuru timu hiyo ya msaada wa kisheria kwa kufika katika wilaya yake kusaidia suala hilo, kwani wengi, pamoja na kwenda mahakamani na kushinda kesi, bado migogoro haiishi.
"Nyie mmekuja kama wakombozi sasa. Tumieni busara zenu kuwahimiza wananchi kufanya utatuzi kwa njia mbadala, lakini pia waridhike na uamuzi wanaopewa na vyombo vyetu vya haki na watekeleze kwa amani. Hapo tatizo tutakuwa tumemaliza," amesema.
Naye wakili mwandamizi katika kampeni hiyo, Fauzia Akonay, amesema migogoro hiyo inatokana na wengi kutokuzingatia umuhimu wa kuanzisha mchakato wa ukusanyaji na ugawaji wa mirathi hadi wanapoanza kugombana, ndipo wanakimbilia mahakamani.
"Tena wanawake na watoto wengi wamekuwa waathirika wa migogoro hii, kwani anapofariki baba wa nyumba, mke au watoto wanajisahau kufungua mirathi na kufanya mgawanyo wa mali, hasa wakiona hakuna mgogoro. Hadi anaibuka ndugu huko au mtu baki anaanza kelele, ndipo wanashtuka usingizini.
"Hatari kubwa ya kushindwa kuanzisha mchakato wa mirathi haraka baada ya muhusika kufa inaweza kusababisha wanufaika kupoteza mali, itakapopita muda mrefu, kutegemeana na ushahidi utakaotolewa na mashahidi watakaokuwepo kipindi hicho," amesema.
Pia amesema kuwa katika kuanzisha mchakato wa mirathi, cheti cha kifo ni muhimu, hivyo amewataka ndugu wa karibu au mwenza wa marehemu kuhakikisha wanakuwa nacho na kukitunza kama nyaraka muhimu katika mchakato wa upatikanaji wa mirathi.
Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria, Esther Msambazi, kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, amesema kampeni hiyo, iliyoanza Machi 28, 2025, katika kata mbalimbali mkoani Arusha, inatarajiwa kuhitimishwa Aprili 6, 2025.
Amesema kampeni hiyo itatoa huduma za kisheria katika wilaya zote sita za Mkoa wa Arusha.
"Kampeni hii ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, iliyolenga kuongeza wigo wa upatikanaji wa haki kwa wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za huduma za kisheria, ikiwamo kulipa mawakili kuwasimamia katika mashauri yao," amesema.
Amesema kuwa kupitia kampeni hiyo, ambayo inatolewa bure, mpaka sasa imefanikiwa kuwafikia zaidi ya wananchi milioni moja katika mikoa 23 nchini.
Ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wa Arumeru kutumia muda wao kwenda katika viwanja vya Malula, vilivyoko Kata ya Malula, Wilaya ya Arumeru, kuwasilisha kero zao mbalimbali, lakini pia kupata elimu ya kisheria kwa ajili ya uelewa wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza.
Machi 17, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan, akizindua Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, toleo la mwaka 2023, jijini Dodoma, alisema ardhi ni suala linalogusa kila mtu na amani ya nchi, hivyo kupungua kwa migogoro ni kuendeleza amani hiyo. Aliwataka watumishi wa ardhi kufanya kazi kwa kutanguliza utu mbele ili kuwezesha utekelezaji wa sera hiyo.
Alisema miaka 30 ya sera hiyo imeonyesha ulazima wa kuifanyia maboresho ili kuendana na uhalisia wa sasa. Lengo la jumla la sera hiyo iliyoboreshwa ni kuhakikisha kunakuwa na mfumo madhubuti na usawa wa kijinsia katika umiliki, upatikanaji na usimamizi wa matumizi ya ardhi kwa maendeleo endelevu.
Alitaja mambo yaliyomo katika sera hiyo kuwa ni kuimarisha udhamini na ulipaji wa fidia, kuimarisha uwekezaji katika uendelezaji wa ardhi, kuongeza kasi ya usajili wa ardhi, uimarishaji wa mipaka ya Tanzania na nchi jirani, usimamizi kwenye soko la ardhi nchini, na kuimarisha utatuzi wa migogoro.