Miradi ya Sh9.36 bilioni imekamilika, lakini haitumiki
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere
Dar es Salaam. Wakati wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wakiendelea kukabiliwa na changamoto za huduma za afya, elimu na utawala, imebainika kuwa miradi yenye thamani ya Sh9.36 bilioni tayari imekamilika lakini haijaanza kutumika.
Ukaguzi wa mwaka wa fedha 2024/25 wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliyoiwasilisha Ijumaa ya Aprili 10, 2026 bungeni imeonyesha hali hiyo katika mamlaka saba za serikali za mitaa.
Ripoti hiyo imefafanua kuwa Kanuni ya 7(1) ya Kanuni za Fedha za Umma (Usimamizi wa Mali za Umma), 2024 inamtaka ofisa masuuli kuhakikisha kuwa mali za umma zinatumika ipasavyo kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
Imeongeza kuwa endapo mali yoyote ya umma itabaki bila kutumika kikamilifu au itatumika chini ya kiwango kwa kipindi cha miezi sita au zaidi, ofisa masuuli anatakiwa kutoa taarifa kwa katibu mkuu kwa hatua zaidi.
“Katika mwaka wa fedha 2024/25, nilitathmini hali ya utekelezaji wa miradi iliyokamilika na kubaini kuwa miradi 14 katika mamlaka ya serikali za mitaa saba, katika sekta za utawala, afya na elimu, yenye thamani ya Sh9.36 bilioni ilikuwa imekamilika, lakini haikuanza kutumika au ilikuwa inatumika chini ya kiwango kilichotarajiwa,” imeeleza ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kutotumika kwa miradi hiyo kunatokana zaidi na ukosefu wa miundombinu saidizi na maandalizi duni ya uendeshaji baada ya kukamilika kwa miradi.
“Changamoto kuu zilizobainika ni pamoja na ukosefu wa huduma muhimu kama maji na gesi ya maabara, kukosekana kwa vifaa na samani stahiki, pamoja na upungufu wa watumishi wenye taaluma maalumu.”
“Taarifa za kina zinaonekana katika kutumika chini ya kiwango kwa miundombinu iliyokamilika inaashiria athari kubwa katika sekta za elimu na afya, ikiwemo kuchelewa kwa utoaji wa huduma, kutokidhi mahitaji ya jamii, pamoja na kuharibika kwa mali kutokana na kutotumika kwa muda mrefu,” imeeleza ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa mapungufu hayo yanaweza kuongeza gharama za matengenezo na kuongeza hatari ya miundombinu hiyo kupitwa na wakati kabla ya kutumika kikamilifu.
Hivyo inapendekeza Tamisemi ihakikishe miundombinu iliyokamilika inatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa, kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii lengwa.
Pia, Tamisemi ishirikiane na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), kwa kutenga na kusambaza watumishi na wataalamu wa kutosha kulingana na muundo wa ajira wa mamlaka husika za serikali za mitaa.