Meli iliyopinduka bandarini Mwanza bado ipo majini, uchunguzi ukiendelea

Mwonekano wa meli ya Mv Clarias ikiwa imepinduka katika Bandari ya Mwanza Kaskazini. Meli hiyo inayotoa huduma kati ya mwalo wa Kirumba na kisiwa cha Goziba wilayani Muleba mkoani Kagera, ina uwezo wa kubeba abiria 290 na tani 10 za mizigo. Picha na Mgongo Kaitira
Muktasari:
- Meli ya Mv Clarias inadaiwa kupinduka majini ikiwa imeegeshwa katika Bandari ya Mwanza Kaskazini jijini Mwanza saa 10 alfajiri ya kuamkia Jumapili Mei 19, mwaka huu, huku taarifa za awali zikidai kuwa hakuna mtu ama mizigo iliyozama katika meli hiyo.
Mwanza. Zikiwa zimepita siku 10 tangu meli ya Mv Clarias ipinduke ikiwa imeegeshwa katika bandari ya Mwanza Kaskazini jijini hapa, meli hiyo bado haijanasuliwa yote kutoka majini.
Hata hivyo, jitihada za unasuaji wa meli hiyo inayofanya safari zake kati ya Mwanza na Kisiwa cha Goziba wilayani Muleba mkoani Kagera kwa ajili ya kuipandisha kwenye cherezo ili kufanyiwa uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha tukio hilo zinaendelea. Meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 290 na tani 10 za mizigo.
Akizungumza leo Jumanne, Mei 28, 2024, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL) Eric Hamissi ameishauri Serikali kuunda kamati huru yenye jukumu la kusimamia shughuli za uokoaji na unasuaji pindi meli zinapopata changamoto majini.
“Nadhani ifike muda tuwe na standing committee (kamati huru) ambayo inaweza kukutana quarterly (kila baada ya miezi mitatu) kuangalia tathmini na mikakati ya kuimarisha usalama katika maziwa makuu. Kila siku yanaibuka mengine, tunapopata ajali ndiyo tunashtuka.”
“Hiyo kamati inaweza ika-identify (kubainisha) maeneo ambayo tunaweza tukapata equipements (vifaa) inapotokea la kutokea, hatupendi ajali lakini yawezekana zikatokea, ndege ilivyoanguka ya Precision Air imetufundisha kitu, Mv Bukoba miaka 28 iliyopita imetufundisha jambo, hata hii (Mv Clarias) imetufundisha jambo,” amesema Hamissi.
Kwa mujibu wa Hamissi, kamati hiyo ikianzishwa itasaidia kutambua maeneo vilipo vifaa maalum vya uokozi wa abiria na unasuaji wa meli inapozama, ili kuimarisha usalama wa abiria na vyombo vinavyotoa huduma ndani ya Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.
“Niwahakikishie wananchi kwamba usafiri kwa njia ya maji uko salama kabisa, ni mara chache ajali kutokea majini hata inapotokea tunaichambua na kubainisha hatua za kuchukua ili isitokee tena,” amesema Hamissi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli nchini (Tasac), Mohamed Salum, uchunguzi wa tukio la meli hiyo kupinduka majini ikiwa bandarini unaendelea huku akidokeza kuwa ikibainika kuna uzembe uliochangia, wahusika hawatofumbiwa macho.
Mbali na hatua hizo, Saluma amewataka wadau wa usafirishaji majini kuzingatia miongozo na kanuni za usafirishaji wa abiria na mizigo ikiwemo kuandaa muongozo wa usalama ndani ya meli na kuajiri mabaharia waliothibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Mabaharia inayosimamiwa na wataalamu wa Tasac.
“Tukio lililotokea hapa limetufundisha kwamba tuna haja ya kuwekeza kwenye masuala ya uokozi wa vyombo, lakini kimataifa kuna Mkataba wa Kimataifa wa Salvage na mara nyingi huwa haifanyi Serikali, inahamasisha wawekezaji binafsi. Kwa hiyo tunalichukua kwa ajili ya kuishauri Serikali,” amesema Salum.
Kwa upande wake, Mkazi wa Nela jijini Mwanza, Ananilea Mushi ameeleza kitendo cha meli hiyo kunasa majini zaidi ya siku tano bila kunasuliwa kuwa ni aibu kwa nchi, huku akiiomba Serikali kuwekeza fedha za kutosha kwenye vifaa vya uokozi na unasuaji wa meli.
“Nimekuwa nasikia kuna kituo cha uokozi kinajengwa cha Afrika Mashariki, lakini hicho hakitoshi, tunahitaji kuona kuna kituo maalum ambacho tunajua kabisa hata meli ikizama majini sehemu yoyote inakuwa rahisi kufika kwa wakati na kunusuru maisha ya abiria na meli yenyewe,” amesema Ananilea.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mkombozi Fishing and Marine Transport Limited, Ibrahim Kitano ameishauri Tasac kuwafutia leseni mabaharia wa meli ya Mv Clarias, endapo uchunguzi huo utaonyesha kuwa walifanya uzembe uliosababisha meli hiyo kuzama.
Mv Butiama yaanza safari
Awali, ilielezwa kwamba tukio la Mv Clarias kupinduka lilisababisha meli ya Mv Butiama inayofanya safari zake kati ya bandari ya Mwanza Kaskazini kwenda Ukerewe kushindwa kuendelea na safari zake kwani eneo ambalo Mv Butiama ilikuwa ikigeuzia ndipo Mv Clarias ilipopindukia.
Hata hivyo, Ofisa Uhusiano wa MSCL, Abdulrahman Salim ameieleza Mwananchi Digital kuwa safari za Mv Butiama zimerejea tangu juzi Jumapili Mei 26, mwaka huu ambapo abiria na mizigo walianza kusafiri kutoka Mwanza kuelekea kisiwa cha Ukerewe.