MCL yasaini MoU kukuza ‘Rising Woman’

Muktasari:
- Makubaliano hayo yamelenga katika maeneo matatu ambayo ni kupewa mafunzo, kuwalea na ushauri kwa kubadilishana fursa na kujengewa uwezo wa kiuongozi katika shughuli wanazozifanya ili kuwainua zaidi kupitia majukwaa ya kidijitali ya MCL.
Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imetiliana saini ya makubaliano ‘MoU’ na Taasisi ya Wakurugenzi Tanzania (IODT) kwa ajili ya kuendeleza Jukwaa la The Citizen Rising Woman lenye lengo la kumuinua mwanamke.
Makubaliano hayo yamelenga katika maeneo matatu ambayo ni kupewa mafunzo, kuwalea na ushauri kwa kubadilishana fursa na kujengewa uwezo wa kiuongozi katika shughuli wanazozifanya ili kuwainua zaidi kupitia majukwaa ya kidijitali ya MCL.
Hatua hiyo imekuja baada ya maombi ya wadau wengi waliokuwa wakitaka jukwaa hilo ambalo awali liliangazia wanawake viongozi katika makampuni makubwa kwa kuandika makala za mafanikio yao na namna walivyothubutu kipindi cha Februari mpaka Machi 8 pekee, kuangazia pia wanawake wa ngazi za chini waliothubutu.
Akizungumza leo Mei 30, 2023 baada ya kusaini mkataba huo Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu amesema hiyo ni mara ya pili kushirikiana na IODT kwani wamekuwa na makubaliano kwa kipindi cha miaka miwili.
Amesema kinachofanywa sasa ni mwendelezo wa Rising Woman ambayo imekuwa ikianza mwezi Februari mpaka Machi lakini kilele kikifanyika tarehe 8.
“Ile itaendelea tunachokifanya sasa ni kuiboresha kwa kuwa kulikuwa na uhitaji mkubwa, kusiwe kati ya Februari na Machi ila iwe inaendelea kwa maana ya kuwajengea uwezo hawa waliopo kwenye nafasi za uongozi lakini bado wana changamoto zingine, lakini pia kuangalia tunawaleta vipi wanawake wengine kwenye nafasi hizi,” amesema Machumu.
Amesema Rising Woman sasa itakuwa inawakusanya wale ambao wangependa kuwa katika ile jumuiya, wabadilishane fursa na wajengewe uwezo wa uongozi ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.
“Sisi kama MCL hatutabagua nani anaingia itakuwa wazi kwa yeyote anayetaka kuingia pale aweze kujiandikisha na kwamba sasa itawagusa wanawake wote si wale walio katika nafasi za maamuzi pekee bali itagusa wanawake wote, wajasiriamali na wale walio katika masomo ambao wana ndoto waseme malengo yao,” amesema.
Mkurugenzi wa IDOT, Said Kambi alisema viongozi wanazaliwa na karama lakini pia wanafaa kutengenezwa kwa kuendelezwa na ndiyo sababu ya kuja na hayo mambo matatu.
“Changamoto ni nyingi zinazowakumba wanawake, mwanamke ambaye anauza matunda ana changamoto zake hivyo kutakuwa na kufunda na kushauri kwa nasaha na kitaalamu na kiuongozi,” amesema.
“Kwa sasa tunaamini uongozi unakuja kwa kuongezewa maarifa yaani kupewa mafunzo, kuwalea na ushauri wa namna gani wafanye shughuli zao kufikia mafanikio wanayoyatamani na tunataka kuona wakikua kutoka pale walipo,” alisema Kambi na kuongeza;
“Kwa sasa tunataka kuona wanawake ambao wanauza mboga mboga wanatuambia kuhusu wao lakini wanaendelezwa kwa kupewa mafunzo na kuwalea wafikie matamanio yao hivyo IDOT tutasimamia katika kuhakikisha mambo hayo matatu yanafanikiwa,” amesema.