Mchina alivyotapeliwa na mtuhumiwa aliyejitambulisha muhtasi wa Waziri Mkuu

Muktasari:
- Shahidi huyo ametoa ushahidi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika kesi ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo na kujipatia Dola za Marekani 10,000 inayomkabili Bahati Malila na Godfrey Mtonyi (30).
Dar es Salaam. Raia wa China, Biao Lin Tang, ameieleza mahakama jinsi alivyotapeliwa Dola za Marekani 10,000, kutoka kwa Bahati Malila, baada ya kujitambulisha kuwa yeye ni katibu mhutasi wa Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa, wakati akijua ni uongo.
Kiasi hicho cha fedha ni sawa na Sh22 milioni, kwani kwa wakati huo tukio linatendeka, Dola moja likuwa Sh2,200.
Lin Tang ambaye ni Rais wa Taasisi ya Canton HongKong and Macau Fellow Townsmen Association in Tanzania, ametoa ushahidi wake, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika kesi ya kughushi nyaraka na kujipitia fedha kwa njia ya udanganyifu inayowakabili washtakiwa wawili ambao ni Bahati Malila (50) na Godfrey Mtonyi (30).
Malila maarufu kama Masele, ambaye ni mkazi wa Kijamboni na Mtonyi mkazi wa Mbezi Jogoo, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 14/2020 yenye mashtaka sita yakiwemo ya kughushi nyaraka, kuwasilisha nyaraka za uongo wakionyesha kuwa zimetolewa na waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa pamoja na kujipatia dola za Marekani 10,000 kwa njia ya udanganyifu ambazo ni sawa na zaidi ya Sh22 milioni, mali Lin Tang.
Lin Tag ambaye ni shahidi wa 10 wa upande wa mashtaka, ametoa ushahidi wake leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya upande mashtaka kuendeleza na ushahidi.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga, Lin Tang alidai mwishoni mwa Desemba 2019, taasisi yake ilipanga kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa msaada katika Jimbo la Ruangwa ambalo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassimu Majaliwa ndiye mbunge, ambapo walipanga kutoa dola za Marekani 20,000 kwa ajili ya kuwanunulia watoto wenye uhitaji vifaa mbalimbali vya shule ikiwemo madaftari, vitabu, kalamu na sare za shule.
‘Ili kufanikisha jambo hili, nilimshirikisha rafiki yangu ambaye ni raia wa Tanzania anayeitwa John Kilasile, kisha akanikutanisha na Bahati ambaye alitambulishwa kama katibu muhtasi wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,’’ amedai.
Lin Tang ambaye alikuwa anatoa ushahidi wake kwa lugha ya Kichina na kutafsiriwa na mkalimani kwenda lugha ya Kiswahili, alidai anajuana na Kilasile kwa zaidi ya miaka mitano na kwa mara ya kwanza kuonana ilikuwa Morogoro kwenye maonyesho ya Sabasaba.
Amesema tangu walivyokutana Morogoro, Lin Tang amekuwa akimuanini sana na Kilasile na kumshirikisha katika baadhi ya vitu.
“Nikiwa kama rais na mwenyekiti wa Taasisi Taasisi ya Canton HongKong and Maccaw Fellow Townsmen Association in Tanzania, niliita wanachana wote na msaidizi wangu na kufanya kikao cha kusaidia watoto hao katika Jimbo la Ruangwa,” anasema Lin Tang.
Anadai baada ya kumaliza kikao kikubwa lilichoshirikisha wanachama wa taasisi hiyo, walikutana kwa mara ya pili na kufanya kikao kidogo katika Hoteli ya Serena iliyopo Dar es Salaam kilichohusisha watu watano, akiwepo yeye, John Kilasile, Bahati Malila, msaidizi wa Jin Tang ambaye ni Guanhui Su Biaolin Tang na mwanamke mmoja ambaye hakumfahamu kwa jina japo alitambulishwa kama rafiki wa Kilasile.
“Katika kikao kile kilichofanyika Serena Hoteli, tulimueleza huyo aliyedai ni katibu wa Waziri Mkuu, kuwa tuna Dola za Kimarekani 20,000 zinazotakiwa kuelekezwa katika Jimbo la Ruangwa pamoja na vifaa vya shule ambavyo ni kalamu, madafari, nguo kwa ajili ya kusaidia watoto yatima na wale wenye mazingira magumu,” alidai Lin Tang huku akifafanua kuwa taasisi yake ni muunganiko wa wafanyabaishara kutoka Canton, HongKong na Macau wanaoishi nchini Tanzania, ambayo inajishughulisha na kutoa misaada kwa watoto yatima na wasiojiweza.
Akiendelea kutoa ushahidi wake, Lin Tang alidai kuwa Bahati alimueleza shahidi huyo kuwa hitaji la kwanza ili kazi hiyo iweze kufanyikiwa alimtaka atoe Dola za Marekani 10,000 kwanza ili apate vyeti vitatu ikiwemo cheti cha shukrani kinachoonesha wanachoenda kufanya ni chema.
“Bahati aliniambia, cheti cha kwanza kitakuwa na jina langu, cheti cha pili kitakuwa na jina la msaidizi wangu na cheti cha tatu kitakuwa na jina la taasisi yetu,” amedai shahidi huyo.
Baada ya mazungumo hayo, Januari 14, 2020 akiwa katika ofisi yake iliyopo Msasani, alitoa dola za Marekani 10,000 na kumpatia Kilasile ambapo kilasile alimpatia Bahati kwa ajili ya kuandaa vyeti hivyo.
Alidai fedha iliyobaki ambayo ni dola 10,000, alipanga kuitoa baada ya kuonana naYe Bahati ili afanye kikao cha kuonana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa ajili ya kumalizia ununuzi wa vifaa vya shule.
Alidai kuwa Bahati alimtaka kuongeza tena dola za Marekani 10,000 ili ziwe Dola 20,000 kwa ajili ya kuonana na Waziri Mkuu Majaliwa ambapo zilipita wiki mbili wakisubiri kuonana naye lakini hakukuwa na kilichoendelea ndipo Kilasile akampigia simu Bahati baada ya kuhisi kuwa kunaweza kukawa na uongo ulioendelea.
“Baada ya wiki mbili kuptia, tangu nilipotoa dola 10,000 na wakati huo nikijiandaa kwenda kuonana na Waziri Mkuu, sikupata vyeti nilivyoahidiwa wala sikuona chochote kilichokuwa kinaendelea katika ahadi yetu mimi na Bahati,” alidai shahidi huyo ambaye muda wote alikuwa amesimama na kuongeza kwa msisitizo.
“Baada ya kuwa na wasiwasi, ilibidi tutafute namna ya kukamata Bahati na kilichofanyika ni kwamba, nilimpigia simu Kilasile na kumwambia ampigie simu Bahati ili aje ofisini kwangu kuchukua hela,” amesema.
Iliendele akudaiwa kuwa Lin Tang baada ya kugundua Bahati ni muongo walienda Kituo Kikuu cha Polisi (Central ) kuripoti tukio hilo.
Hata hivyo, Bahati alitengeneza vyeti viwili vyenye rangi ya kijani ambavyo pembeni vilikuwa na mistari yenye rangi ya bendera ya taifa na kuviwasilisha ofisi za taasisi hiyo zilizopo Msasani, Wilaya ya Kinondoni.
Mbali na kuwatambua washtakiwa hao mahakamani hapo, shahidi huyo alitambua vyeti hivyo vya kughushi na kuiomba mahakama ipokee vyeti kama vielelezo kwa upande wa mashtaka.
Hata hivyo ambavyo vyeti hivyo vilipokelewa na mahakama kama kilelelezo cha upande wa mashtaka.
Shahidi huyo baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, upande wa mashtaka walidai kuwa wamefunga ushahidi, hivyo wanaomba terehe nyingine kwa ajili ya uamuzi
Hakimu Kabate aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 19, 2023 kwa ajili ya kutoa uamuzi iwapo washtakiwa hao wanakesi ya kujibu.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Januari 13, 2020 katika eneo la Msasani, Kinondoni mkoani Dar es Salaam, wakiwa na nia ovu walighushi vyeti vitatu wakionyesha ni vyeti vya kuchangia michango kwa ajili ya kutoa misaada elimu kwa watoto wenye uhitaji, vikionyesha vimetolewa Januari 13, 2020 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, wakati wakijua ni uongo.
Katika mashtaka ya kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa, inadaiwa kuwa Januari 14,2020 washtakiwa wakiwa wanafahamu na kwa nia ovu waliwasilisha nyaraka za uongo kwa Biao Lin Tang ambazo ni vyeti vya utoaji wa michango kwa ajili ya misaada vikionyesha kuwa vimetolewa na Januari 13, 2020 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, wakati wakijua ni oungo.
Katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, washtakiwa wanadaiwa, Januari 14, 2020 katika eneo la Msasani, Kinondoni, kwa lengo ovu washtakiwa walijipatia Dola za Marekani 10,000 sawa na Sh22,950,000 kutoka kwa Biao Lin Tang kwa kudai kuwa zinaenda katika jimbo la Ruangwa ambalo linasiamiwa na Mbunge Kassim Majaliwa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya shule, wakijua kwamba si kweli.