Kesi ya watumishi 16 Dar kutoa taarifa Mahakama Kuu

Muktasari:
- Upande wa Jamhuri umedai shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa wanaendelea na tararibu za kuwasilisha taarifa Mahakama Kuu.
Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi inayowakabili watumishi 16 wakiwemo wahasibu wa Jiji la Dar es Salaam wamedai kuwa wanaendelea na tararibu za kuwasilisha taarifa Mahakama Kuu.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 143 likiwemo la kuisababishia hasara Jiji hilo zaidi ya Sh8.9 bilioni.
Wakili wa Serikali, Aroun Titus alidai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Pamela Mazengo alidai shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa wanaendelea na tararibu za kuwasilisha taarifa katika Mahakama Kuu.
"Naiomba mahakama hii iahirishe shauri hili Kwa kuwa tukaendelea na tararibu za kuwasilisha taarifa mahakama kuu," amesema Titus.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Oktoba 23, 2023 kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Tulusubya Kamalamo, James Bangi ambao ni wahazini Mohamed Khars, Abdallah Mlwale na Deogratias Lutatuza na Alinanuswe Mwakasumbe ni wahasibu pamoja naJudica Ngowo ambaye ni karani wa fedha.
Wengine ni Febronia Nagwa, Glory Eugen, Said Bakari, Josephine Sandewa, Dorica Gwihala, Jesca Lugonzibwa, Patrick Chibwana ambao ni wahasibu, Patrick Chubwana Ofisa Afya , Ally Baruan meneja na Khalid Nyakamande ofisa mtendaji wa mtaa.
Katika kesi msingi inadaiwa kuwa Julai Mosi, 2019 na Juni 30, 2021 jijini Dar es Salaam washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu, utakatishaji wa fedha na kujipatia kiasi cha Sh8.9 bilioni mali ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam..