Prime
Mchengerwa: Kanuni za uchaguzi serikali za mitaa zitakuwa shirikishi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa katika mahojiano maalumu na wahariri wa gazeti la Mwananchi. Picha na Said Khamis
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakaofanyia baadaye mwaka huu utakuwa huru na haki, kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi.
Waziri huyo mwenye dhamana ya kuusimamia uchaguzi huo amesema, “uamuzi utakuwa wa wananchi, wakisema twende hivi huko ndiko tutakakokwenda na Rais ameshatoa mwongozo, hivyo Watanzania wawe na furaha, kwa sababu tunaishi katika miongozo hiyo.”
Msisitizo huo ameutoa akijenga hoja ya jinsi Tamisemi ilivyojipanga kuusimamia uchaguzi huo wakati wadau wakipaza sauti juu ya kuchelewa kutolewa kwa kanuni za kuusimamia na iwapo uamuzi wa wananchi kupitia sanduku la kura utaheshimiwa.
Katika kuhakikisha mchakato wa uchaguzi huo unakuwa huru na haki, Mchengerwa alisema Serikali itazingatia maoni ya wananchi, wadau wa vyama vya siasa yatakayotolewa katika kuboresha kanuni za uchaguzi huo u.
Machi 5, mwaka huu akimwakilisha, Rais Samia katika mkutano mkuu wa nne wa ACT-Wazalendo, Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulrahman Kinana alisema uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utakuwa huru ili wananchi wafanye uamuzi wenyewe wa viongozi wanaowataka.
“Niwahakikishie Rais Samia ameamua uchaguzi wa mwaku huu na mwaka ujao unakuwa huru na haki... wapo wenye mashaka na kauli hii, lakini wanazo sababu zinatokana na mwaka 2019 na mwaka 2020,” alisema Kinana.
Katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji mwaka 2019 wagombea wengi wa CCM walipita bila kupingwa kama ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 baada ya wagombea wa upinzani na mawakala wao kuenguliwa.
Lakini juzi, Waziri Mchengerewa akizungumza katika mahojiano maalumu na wahariri na waandishi wa Mwananchi alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salaam, alisisitiza mchakato wa mwaka huu na mwakani utakuwa tofauti kwa sababu wanatekeleza maono ya Rais Samia.
Alisema falsafa ya 4R za Rais Samia zinamaanisha mambo mengi, ikiwemo kuwaunganisha Watanzania, hivyo watendaji wa Tamisemi wanaishi na kutekeleza majukumu yao kutokana maono hayo.
Baada ya Rais Samia kushika wadhifa huo Machi 19 mwaka 2021, alikuja na falsafa ya 4R kwa lengo la kuliponya na kuliweka Taifa pamoja, akiwa na maana kuleta maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kulijenga upya na akawataka viongozi na watendaji wenzake kuishi katika misingi hiyo.
Katika mahojiano hayo, Mchengerewa alisema “Rais anapotoa maelekezo ya namna hii, jukumu letu ni kutelekeza. Rais anataka kuona uchaguzi unakuwa huru na haki, hivyo lazima tutekeleze kama mkuu wa nchi anavyohubiri.
“Huu ndio msingi wa muunganiko wa Watanzania kuwa kitu kimoja, sasa hivi tunafanya kazi katika mazingira mazuri kwa sababu tumeshapata miongozo, jukumu letu ni kuitekeleza na tutahakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki,” alisema Mchengerwa.
Alisema uchaguzi ni hatua, mchakato wa kuandaa kalenda ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji na maandalizi ya kanuni kwa ndani vimekamilika.
“Kanuni zinazoandaliwa ni za Watanzania wote na zina uratibu kama zinavyoandaliwa sheria. Ndani ya Serikali tumeshamaliza, sasa tunaendelea na taratibu za wadau na mchakato utakuwa wazi kwa sababu Rais anaamini katika demokrasia, ili kuleta mshikamano wa Taifa,” alisema.
Alisema muda si mrefu mchakato wa kanuni utashuka katika ngazi ya wadau, wananchi na vyama vya siasa katika kutoa maoni, wote watashirikishwa katika mchakato huo.
“Tutapata kanuni kila mmoja atazifurahia,” alisema Mchengerwa.
Alipoulizwa atawezaje kuleta uwanja usawa katika mchakato huo wakati yeye ni waziri anayetokana na CCM, Mchengerwa alijibu “hata majaji wanateuliwa na Rais lakini kuna baadhi ya maeneo Serikali inashindwa kesi zinazosimamiwa na majaji hao.”
“Kanuni sio za waziri bali za Watanzania, namna ya kuchukua maoni taratibu zitatuongoza katika kufanya uamuzi. Uamuzi utakuwa wa wananchi, wakisema twende hivi, huko ndiko tutakakokwenda na Rais ameshatoa mwongozo, hivyo Watanzania wawe na furaha, kwa sababu tunaishi katika miongozo hiyo,” alisisitiza.
Ninamudu majukumu
Katika mahojiano hayo, Mchengerwa alizungumzia jinsi anavyoimudu wizara hiyo kubwa kuliko zote alisema yeye ni mzoefu na anaimudu kwa kutumia uzoefu wake wa miaka 24 serikalini.
Aliongeza kuwa yeye ni miongoni mwa mawaziri waliofanya kazi katika mhimili yote mitatu.
“Nimewahi kufanya kazi katika mhimili wa mahakama nikiwa ofisa mwandamizi wa juu kwa miaka 13, pia Bunge kama mwenyekiti wa kamati. Msingi wa hoja ni utendaji na uchapakazi, tunaamini hoja zozote zinaamuliwa kwa kuchapa kazi.
Alisema Tamisemi ni wizara kubwa inayokusanya zaidi ya asilimia 76 ya watumishi wa umma lakini ndani yao wapo wanaofanya kazi vizuri na wengine wakawa na changamoto.
Alisema mapungufu yanayojitokeza wanayatibu na kuyafanyia kazi.
“Ndio maana nilivyoingia tumefanya kazi kubwa sana ya kukumbushana wajibu wetu, usimamizi, lakini wale tuliowapa nafasi ya kujirekebisha wakashindwa tulifanya uamuzi mgumu ikiwemo kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wanaokwenda kinyume.
“Katika sekta ya afya wapo waliosimamisha kazi, kufukuzwa na kuwawajibisha kinidhamu wengine, tumefanya kazi kubwa sana katika kipindi kifupi tangu niingie wizara hii Septemba mosi, mwaka 2024,” alisema.
Alibainisha ndani ya kipindi kifupi cha kushika nafasi hiyo, Tamisemi imefanikiwa kupunguza vifo vya mama na watoto huku suala la nidhamu kwa watumishi wa sekta ya afya likisimamiwa kikamilifu.
“Zaidi ya watumishi 35 walisimamishwa na kuchukuliwa hatua za kinidhamu katika ngazi za wakurugenzi, wakuu wa idara, hadi maofisa wa chini walioshushwa vyeo. Wengi kesi zinaendelea mahakamani,” alisema Mchengerwa.
Kuhusu uwajibikaji na utendaji kazi wa Tamisemi, Waziri huyo alisema Watanzania wenyewe ndio watakaopima jambo hilo kwa kuwa kazi kubwa imefanyika katika kuboresha huduma ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
“Watanzania wenyewe wataongea, siwezi kuzungumza moja kwa moja na kujisifia lakini mtakuwa mashahidi namna ya ambavyo tumefanikiwa kupunguza matatizo katika sekta ya afya, elimu na miundombinu,” alisema.
Barabara za Tarura
Mchengerwa alisema Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) ni miongoni mwa taasisi zinazofanya vizuri ndani ya ofisi yake, akisema imefanya kazi kubwa hasa wakati huu ambapo wamejenga mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami kuliko wakati wowote.
Hata hivyo, anasema changamoto hazikosekani hasa majanga ya asili ikiwemo mvua zinazonyesha na kusababisha mafuriko yanayoharibu barabara na kulazimika kuanza upya ujenzi wa kurekibisha miundombinu hiyo.
Juni mwaka jana, Rais Samia alifanya uteuzi wa viongozi mbalimbali akiwemo Rogatus Mativila kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Tamisemi (Miundombinu).
Kabla ya uteuzi huo, Mativila ambaye ni mhandisi kitaaluma alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).
Wakati akiapishwa, Rais Samia alimwelezea Mativila kuwa alifanya kazi nzuri akiwa Tanroads hivyo ataisimamia vyema Tarura.
Mikopo ya asilimia 10
Swali jingine aliloulizwa ni lini mikopo ya asilimia 10 iliyosimamishwa Aprili 13 mwaka jana na Serikali itaanza kutolewa, Mchengerewa alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata mikopo hiyo kwa utaratibu bora, ndio maana Serikali iliamua kuisitisha baada ya kutokea changamoto mbalimbali katika mchakato wa utoaji na urejeshaji.
Fedha za halmashauri hutolewa kwa mgawanyo wa makundi matatu ambayo ni wanawake asilimia 4 na asilimia 4 vijana huku asilimia 2 zilizobaki zikienda kuwakopesha watu wenye ulemavu, na kufanya jumla ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.
Mwaka 2023, Rais Samia alisema unadaandaliwa utatartibu mzuri wa ukopeshaji wa fedha hizo kupitia mabenki ili kuwasaidia zaidi wahitaji tofauti na utaratibu wa awali ulivyokuwa.
Katika majibu yake, Mchengerwa alisema, “dhamira ya Serikali ni kuhakikisha fedha hizi zinawafikia walengwa, lakini wengi waliochukua hawajereshi fedha hizi, unaweza ukawatafuta usiwaone, hii ni kutokana na misingi waliojiwekea huko nyuma ya namna ya kutoa fedha hizi, na kusababisha wasiokudiwa kunufaika.”
Alisema timu iliyoundwa kuratibu mchakato mpya wa utoaji wa mkopo imeshamaliza kazi yake, lakini ni mapema kueleza moduli ipi itakayotumika katika kuitoa mikopo hiyo.
Mchengewa alisema hivi karibuni majibu yatapatikana ili kuweka msingi mzuri utakaohakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa waliokusudiwa kukopesha ambao ni kina mama, vijana na watu wenye ulemavu.
“Tamisemi imeshaiwasilisha kwenye mamlaka tunasubiri maelekezo na utaratibu utakaotumika. Dhamira ya Serikali ni fedha ziende kwa walengwa waliokusudiwa,” alisema Mchengerwa.
Kuhusu kurejeshwa kwa fedha hizo, Mchengerwa alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua kwa kuwabana baadhi ya watendaji wa halmashauri na yapo maeneo likiwemo Jiji la Dar es Salaam, fedha zimeanza kurudi kwa kiwango kikubwa.
Suala la kutorejeshwa kwa fedha za mikopo hiyo limekuwa sugu na limekuwa likibainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kila mwaka.
Kwa nyakati tofauti, kabla ya Serikali kusitisha, wabunge walikuwa wakilalamikia ubadhirifu wa fedha hizo na kuitaka Serikali isitishe mikopo hiyo, kwa kuwa imetengeneza mianya ya rushwa na ufisadi kwenye halmashauri.
Mathalani, Aprili 4 mwaka jana, Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee aliuliza swali la nyongeza kwa Ofisi ya Tamisemi kuhusu upotevu mkubwa wa fedha hizo.
Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC) alisema ukaguzi wa CAG, “alibaini kulikuwa na upotevu wa zaidi ya Sh47 bilioni na mara ya pili Sh84 bilioni nazo hazijulikani, je, hawa wakurugenzi ambao ndio maofisa masuuli lini watachukuliwa hatua ili kukomesha jambo hilo.”
Naibu Waziri wa Tamisemi, Dk Festo Dugange alikiri kulikuwa na uzembe katika ufuatiliaji wa fedha hizo, ingawa kwa wakati huo akijibu swali hilo alisema kasi ya ulipaji imeongezeka. Alisema wastani wa makusanyo kwa mwaka 2018/19 ilikuwa asilimia 66 lakini mwaka 2021/22 ukusanyaji uliongezeka hadi kufikia asilimia 82.
Migogoro ya ardhi
Aakizungumzia changamoto anazokutana nazo, alisema kubwa katika maeneo mengi ni suala la ardhi, akisema katika ziara iliyofanyika hivi karibuni ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda ilizungumzwa kila alikopita.
“Lakini kwa bahati mbaya Watanzania wengi hawafahamu jukumu la ardhi, huko liliondolewa chini ya usimamizi wa Tamisemi na kupelekwa chini wizara ya ardhi,” alisema Mchengerwa.
Katika kulipatia ufumbuzi suala hilo, alisema ndani ya Serikali wanaendelea kujadili hatua nzuri ya kuliendea huku akimpongeza Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa kwa namna anavyotatua kero za ardhi katika maeneo mbalimbali.
“Kama mnavyofahamu waziri wa ardhi ni mmoja lakini watumishi hawa wapo kila eneo, ndio maana tukasema watumishi wakibaki Tamisemi itakuwa rahisi namna ya kushughulika nao hasa nidhamu zao,” alisema Mchengerwa.