Mbowe kuanza ziara Marekani

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe

Muktasari:

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe anaanza ziara ya kikazi ya siku sita Marekani. Pamoja na mambo mengine atahudhuria kongamano litakalokusanya viongozi mbalimbali na mashirika kujadiliana hali ya demokrasia, utawala wa sheria na maendeleo ya kiuchumi barani Afrika

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe anatarajia kufanya ziara ya kikazi ya siku sita nchini Marekani.


Katika ziara hiyo, Mbowe anatarajiwa kukutana na viongozi mbalimbali kujadiliana hali ya demokrasia, utawala wa sheria na maendeleo ya kiuchumi barani Afrika.

Hiyo ni ziara ya kwanza kufanywa na kiongozi huyo wa juu kutoka chama cha upinzani nchini Tanzania, tangu alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Vyama vya Demokrasia Afrika (DUA), katika mkutano mkuu wa umoja huo uliofanyika Novemba 9, 2022.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumapili, Desemba 04, 2022  na Mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema kiongozi huyo anatarajiwa kuondoka leo kwenda Marekani.“Akiwa Marekani, Mbowe atahudhuria kongamano la International Democrat Union (IDU) litakalodumu kwa siku tatu, Kongamano hili litakalohudhuriwa na vyama wanachama wa IDU, viongozi wa serikali, wabunge na maseneta wanaotokana na vyama wanachama wa IDU pamoja na taasisi za kimataifa, litahitimishwa na kikao cha Baraza la Uongozi la IDU  Desemba 09, 2022,” amesema


Mrema amesema Mbowe akiwa nchini humo anategemewa kuhudhuria kongamano lingine la mkutano wa Baraza la Uongozi la IDU kama Mwenyekiti Mwenza wa Democrat Union of Africa (DUA) na mmoja wa Makamu Wenyeviti wa IDU zaidi ya nafasi yake kama kiongozi wa Chadema.


“Mbowe atafanya mfululizo wa vikao na viongozi mbalimbali duniani pamoja na taasisi na mashirika ya kimataifa kuhusiana na hali ya kisiasa nchini Tanzania kwa nafasi yake kama mwenyekiti wa Chadema. Kadhalika, atakutana na mashirika na viongozi mbali mbali kujadiliana hali ya demokrasia, utawala wa sheria na maendeleo ya kiuchumi Barani Afrika,” amesema


Mrema amebainisha ziara ya Mbowe itahitimishwa kwa kuzungumza na Watanzania waishio nchini humo kwenye mkutano utakaofanyika Desemba 10 mwaka huu jijini Washington DC.