Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbivu, mbichi wanaodaiwa kumuua Milembe wa GGM kujulikana leo

Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya Milembe Suleman.  Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Kesi hiyo inawakabili Dayfath Maunga, Safari Labingo, Genja Pastory, na Musa Pastory, ambao wanakabiliwa na shtaka la mauaji.

Geita. Hatima ya washtakiwa wanne wanaokabiliwa na kesi ya kumuua Milembe Suleman (43), aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Geita Gold Mine (GGM) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali itajulikana leo Jumatatu Agosti 26, 2024.

Hukumu ya kesi hiyo namba 39/ 2023 ambayo ipo chini ya Jaji Mfawidhi, Kelvin Mhina inatarajiwa kusomwa leo, saa nane mchana.

Awali, hukumu hiyo ilipangwa kutolewa Julai 19, 2024, lakini iliahirishwa hadi Agosti 23, 2024 ambayo nayo haikusomwa kutokana jaji anayeisikiliza kesi hiyo kuwa na udhuru.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Dayfath Maunga, (30), Safari Labingo (54), Genja Pastory na Musa Pastory (33) ambao wanakabiliwa na shtaka moja la kumuua Milembe.

Washtakiwa hao ambao awali walikuwa watano, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Mei 24,2023 na kesi kuanza kusikilizwa Mahakama Kuu, kanda ya Geita Aprili 8, 2024 kwa vipindi tofauti hadi Juni 28, 2024 ambapo pande zote mbili zilimaliza kutoa ushahidi.

Upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 29 na vielelezo 19 na baada ya ushahidi huo, Mahakama ilimwachia huru mshtakiwa wa tano, Cecilia Macheni baada ya kuona hana kesi ya kujibu.

Washtakiwa wanne waliobaki walijitetea wenyewe na wote kwa nyakati tofauti walidai kutohusika na mauaji hayo na kuiomba Mahakama iwaachie huru.


Ushahidi wa upande wa mashtaka

Shahidi wa pili na wa tatu katika kesi hiyo, waliieleza Mahakama namna simu za marehemu Milembe zilivyopatikana kwenye shimo la choo, baada ya mshtakiwa wa tatu, Genja Pastory kuwapeleka kwenye shimo alikozitumbukiza.

Shahidi wa tano ambaye ni mkaguzi msaidizi wa Polisi,  PF 25416 Peter Joseph aliieleza Mahakama kuwa sampuli za alama za vidole alizopewa kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi zikiwa na alama A-A1na X-X1 zikiwa na jina la Genja Pastory zililingana kitabia na uhalisia wake na kidole cha kati cha mkono wa kushoto wa mshtakiwa wa tatu.

Shahidi wa sita ambaye ni  ofisa tabibu wa Hospitali ya Mkoa wa Geita, Christopher Matola aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Milembe aliieleza Mahakama kuwa chanzo cha kifo cha Milembe kilitokana na kuvuja damu nyingi kulikosababishwa na majeraha makubwa ya kukatwa na kitu chenye ncha kali.

Shahidi wa 11 wa upande wa Jamhuri alieleza namna mshtalkiwa wa kwanza, Maunga alivyowatafuta wauaji wa kumuua Milembe na kuwalipa Sh2.6 milioni kwa kazi hiyo.

Shahidi wa 13 aliieleza Mahakama namna mshtakiwa wa tatu, Pastory alivyokiri kuumua Milembe na namna walivyofanikisha kufanya hivyo kwa kujifanya ni waganga wa kienyeji.

Kupitia maelezo ya onyo ya mshtakiwa alieleza April 25, 2023 saa tatu usiku wakiendelea kuweka dawa kwenye nyumba za Milembe alizokuwa akijenga eneo la Mwatulole. Mshtakiwa wa tatu (Genja), alimtaka Milembe aliyekuwa na tochi achuchumae, naye alitii kisha kuanza kumkatakata na jambi sehemu mbalimbali za mwili na alizidiwa akaanguka ndipo alikata tena sehemu za kichwani.

Shahidi wa 24, Ditektivu Coplo Hashimu aliieleza Mahakama namna walivyowakamata washtakiwa ambapo Mei Mosi,2023 walimkamata Maunga akiwa nyumbani kwa Milembe eneo la Usagara mkoani Mwanza.

Baada ya mahojiano, Maunga aliwaeleza ili kuwapata wauaji wanapaswa kumtafuta mtu aitwaye Safari Lubingo ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo.

Kukamatwa kwa Safari kuliwezesha kukamatwa pia kwa Musa Pastory ambaye ni mshtakiwa wanne aliyewasaidia kumpata mshtakiwa wa tatu, Genja Pastory ambaye ilidaiwa baada ya kuua alikwenda kwa mganga wa kienyeji, Cecilia Macheni kuondoa mkosi.

 Shahidi wa 26 ambaye ni mkemia kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ally Kanenda aliieleza Mahakama namna vipimo vya vinasaba vilivyofanywa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali vilivyobaini kuwa mpanguso (swab) wa damu kutoka kwenye mpini au mshikio wa

jambia lililotumika kumuua Milembe ina uhusiano na mpanguso wa vinasaba vya mate vya mshtakiwa wa tatu, Pastory.


Utetezi wa washtakiwa

Wakitoa ushahidi wao kwa kuongozwa na mawikili wao walidai kabla ya kukamatwa hawakuwahi kuonana na wala hawajawahi kuwasiliana kwa njia zozote za mawasiliano.

Dayfath Maunga, mshtakiwa wa kwanza alikiri kuishi nyumbani kwa Milembe, lakini akadai alikua akifanya kazi ya kuuza duka la vipodozi la Milembe na kumsaidia kwenye biashara zake za kukopesha fedha kwa riba.

Mshtakiwa huyo alidai tuhuma za kuhusishwa na mapenzi ya jinsia moja si za kweli na hakuwahi kufanya hivyo na kwamba hahusiki na kifo hicho, kwani hakuwa na sababu ya kufanya hivyo.

Mshtakiwa wa pili, Safari Lubingo alidai hafahamiani na mshtakiwa wa kwanza na hakuwahi kuwasiliana naye na kuhusu kuwatafuta Musa na Genja  na kupanga njama za kumuua Milembe alidai hawafahamu na hajawahi kuwasiliana nao.

Mshtakiwa wa tatu, Genja Pastor alidai hakuwaonyesha polisi liliko jambia, bali baada ya kumtoa kituoni walimchukua na gari na kumpeleka sehemu yenye nyasi nyingi na kumtaka atafute jambia na alipolipata aliulizwa kama analifahamu akadai halifahamu na kudai ushahidi uliotolewa mahakamani kuwa alichukuliwa alama za vidole sio wa kweli.

Kwa upande wa mshtakiwa wanne, Musa Pastory alidai hakuwahi kutoa maelezo polisi na wala kuwataja washtakiwa wengine popote, kwa kuwa alikuwa hawafahamu na kudai hajawahi kuhusika na mauji ya Milembe na kuiomba Mahakama imuachie huru.


Endelea kufuatilia mitandao ya mwananchi kupata kitakachoijiri mahakamani leo.