Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hukumu kesi ya Milembe yaahirishwa tena

Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya Milembe Suleman.  Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Maunga na wenzake, Safari Labingo (54), Genja Deus Pastory na Musa Pastory (33) wote kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kumuua mfanyakazi wa GGM, Milembe Seleman (43).

Geita.  Mahakama Kuu Kanda ya Geita, imeshindwa kutoa hukumu ya mauaji inayomkabili Dayfath Maunga (54) na wenzake watatu baada ya Jaji Mfawidhi Kelvi Mhina wa Mahakama hiyo anayesikiliza kesi hiyo, kuwa na udhuru.

Mbali na Maunga,  washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji namba 39 ya mwaka 2023 ni pamoja na Safari Labingo (54), Genja Pastory na Musa Pastory (33).

Washitakiwa hao wanakabiliwa na shtaka moja la kumuua mfanyakazi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Geita Gold Mine (GGM), Milembe Seleman (43).

Hii ni mara ya pili hukumu ya kesi hiyo kuahirishwa, kwani hata mara ya kwanza Julai 19, 2024, hukumu hiyo iliahirishwa baada ya Jaji anayesikiliza kesi hiyo kuwa safarini kikazi.

Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 23, 2024, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Scolastika Teffe amesema kuwa kesi hiyo imeshindwa kuendelea kutokana na jaji aliyeisikiliza kuwa na udhuru hivyo maamuzi yanatarajiwa kutolewa Jumatatu Agosti 26, 2024.

Mwananchi ilifika mahakamani hapo tangu saa 2:50 asubuhi na kushuhudia ndugu wa Milembe wakiwa wamesimama kwa makundi kwenye viunga vya mahakama hiyo iliyopo mjini Geita.

Licha ya ndugu wa Milembe kuwa mahakamani, mawakili wa pande zote hawakuwepo, wala washtakiwa hawakufikishwa mahakamani.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Daifath Maunga na wenzake, Safari Labingo (54), Genja Pastory na Musa Pastory (33) wote kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kumuua mfanyakazi wa GGM, Milembe Seleman (43).

Wanadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 26, 2023 kwa kumuua kwa kumkata na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali mwilini, ikiwemo kichwani, usoni na mikononi.

Upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 29 na vielelezo 19 na baada ya ushahidi wa Jamhuri Mahakama ilimwachia huru mshtakiwa wa tano, Cecilia Macheni baada ya Mahakama kuona hana kesi ya kujibu.


Ushahidi ulivyokuwa

Katika utoaji wa ushahidi, shahidi wa pili na wa tatu wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo waliieleza Mahakama namna simu za marehemu Milembe zilivyopatikana kwenye shimo la choo baada ya mshtakiwa wa tatu Genja Pastory kuwapeleka kwenye shimo alikozitumbukiza.

Shahidi wa tano ambaye ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi,  PF 25416 Peter Joseph aliieleza Mahakama kuwa sampuli za alama za vidole alizopewa kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi zikiwa na alama A-A1na X-X1 zikiwa na jina la Genja Deus Pastory zililingana kitabia na uhalisia wake na kidole cha kati cha mkono wa kushoto wa mshtakiwa wa tatu.

Shahidi wa sita katika kesi hiyo ambaye ni ofisa tabibu wa Hospitali ya Mkoa wa Geita, Christopher Matola aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Milembe Seleman ameieleza Mhakama kuwa chanzo cha kifo cha Milembe kilitokana na kuvuja damu nyingi kulikosababishwa na majeraha makubwa ya kukatwa na kitu chenye ncha kali.

Shahidi wa 11 wa upande wa Jamhuri alieleza namna Mshtakiwa wa kwanza Dayfath Maunga (30) alivyowatafuta wauaji wa kumuua Milembe Seleman na kuwalipa kiasi cha Sh2.6 milioni kwa kazi hiyo.

Shahidi wa 13 aliieleza mahakama namna mshtakiwa wa tatu, Genja Pastory alivyokiri kuumua Milembe na namna walivyofanikisha kufanya hivyo kwa kujifanya ni waganga wa kienyeji.

Kupitia maelezo ya onyo ya mshtakiwa, alieleza kuwa Aprili 25,2023 saa tatu siku wakiendelea kuweka dawa kwenye nyumba za Milembe alizokuwa akijenga eneo la Mwatulole, mshtakiwa wa tatu (Genja) alimtaka Milembe aliyekuwa na tochi achuchumae, naye alitii.

Kisha ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo alianza kumkatakata na jambia sehemu mbalimbali za mwili na alizidiwa akaanguka ndipo alikata tena sehemu za kichwani.

Shahidi wa 24, Ditektivu Koplo Hashimu aliieleza Mahakama namna walivyowakamata washtakiwa ambapo Mei Mosi, 2023 walimkamata mshtaliwa wa kwanza Dayfath Maunga akiwa nyumbani kwa Milembe Usagara Mwanza na baada ya mahojiano aliwaambia ili kuwapata wauaji wamtafute mtu aitwae Safari Lubingo ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo.

Kukamatwa kwa Safari kuliwezesha kukamatwa pia kwa Musa Pastory ambaye ni mshtakiwa wanne aliyewasaidia kumpata mshtakiwa wa tatu Genja Pastory ambae ilidaiwa baada ya kuua alikwenda kwa mganga wa kienyeji Cecilia Macheni kuondoa mkosi.

Shahidi wa 26 ambaye ni Mkemia kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ally Kanenda aliieleza Mahakama namna vipimo vya vinasaba vilivyofanywa na ofisi yake na jinsi vilivyobaini kuwa mpanguso (swab) wa damu kutoka kwenye mpini au mshikio wa jambia lililotumika kumuua Milembe Suleman (43) ina uhusiano na mpanguso wa vinasaba vya mate vya mshtakiwa wa tatu Genja  Pastory.


Utetezi wa washtakiwa

Wakitoa utetezi wao kwa kuongozwa na mawikili wao walidai kabla ya kukamatwa hawakuwahi kuonana na wala hawajawahi kuwasiliana kwa njia zozote za mawasiliano.

Dayfath Maunga mshtakiwa wa kwanza alikiri kuishi nyumbani kwa Milembe lakini akadai alikuwa akifanya kazi ya kuuza duka la vipodozi la Milembe na kumsaidia kwenye biashara zake za kukopesha fedha kwa riba.

 Mshtakiwa huyo amedai tuhuma za kuhusishwa na mapenzi ya jinsia moja siyo za kweli na hakuwahi kufanya hivyo na kwamba hahusiki na kifo hicho na hakuwa na sababu ya kufanya hivyo.

Mshtakiwa wa pili Safari Lubingo alidai hafahamiani na mshtakiwa wa kwanza na hakuwahi kuwasiliana naye na kuhusu kuwatafuta Musa na Genja  na kupanga njama za kumuua Milembe alidai hawafahamu na hajawahi kuwasiliana nao.

Mshtakiwa wa tatu, Genja Pastor alidai hakuwaonyesha polisi liliko jambia bali baada ya kumtoa kituoni walimchukua na gari na kumpeleka sehemu yenye nyasi nyingi na kumtaka atafute jambia na alipolipata aliulizwa kama analifahamu akadai halifahamu na kudai ushahidi uliotolewa mahakamani kuwa alichukuliwa alama za vidole siyo za kweli.

Kwa upande wa mshtakiwa wa nne Musa Pastory alidai hakuwahi kutoa maelezo polisi na wala hakuwahi kuwataja washtakiwa wengine popote kwakuwa alikuwa hawafahamu na kudai hajawahi kuhusika na mauji ya Milembe na kuiomba Mahakama imuachie huru.