Mawaziri wataja mambo matano ziara ya Rais Samia Korea

Dk Ashatu Kijaji (Waziri wa Viwanda na Biashara)
Muktasari:
- Uwekezaji, biashara, ukuzaji wa bunifu za kiteknolojia, ushirikiano wa kimataifa na masuala ya afya ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kuwa manufaa ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Korea Kusini.
Dar es Salaam. Mawaziri watano wa sekta za biashara, uwekezaji, habari na mambo ya nje, wamesema ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Korea imekuwa na manufaa wakitaja mambo matano ukiwemo uwekezaji na biashara.
Mengine ni pamoja na ukuzaji wa bunifu za kiteknolojia, ushirikiano wa kimataifa na masuala ya afya.
Mawaziri hao wameeleza hayo leo Alhamisi Juni 6, 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati wakitoa mrejesho kwa wanahabari kuhusu mafanikio na manufaa yatakayopatikana kutokana na ziara ya Rais Samia nchini Korea iliyoanza Mei 30 hadi Juni 5, 2024.
Mawaziri hao ni pamoja na January Makamba (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Nape Nnauye (Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Ashatu Kijaji (Waziri wa Viwanda na Biashara), Dk Saada Salum Mkuya (Waziri wa Nchi, Fedha na Mipango Zanzibar) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo.
Profesa Mkumbo amesema ziara ya Rais Samia imeonyesha mwanga na nia ya wawekezaji wa Korea Kusini kuwekeza kwenye sekta za madini, mifugo na kilimo.

Amesema ziara hiyo itachagiza ukuzaji wa biashara kati ya Tanzania na Korea kwa siku za usoni tofauti na miaka iliyopita.
“Korea ni taifa ambalo kwa sasa kampuni zake zimetoka nje ya mipaka yake na kuwekeza hasa nchi za Asia, hivyo inawezekana tukawavuta wawekezaji kutoka Korea kuja kuwekeza Tanzania, wenzetu wamepiga hatua kubwa za kimaendeleo na teknolojia.”
“Pia Tanzania imejiwekea lengo la kuchakata mazao ya kilimo ili kuongeza thamani na Korea ni hodari katika maeneo haya, hivyo tunatarajia Gilead Teri (Mkurugenzi Mtendaji Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC) awavutie wawekezaji hao,” amesema Profesa Kitila.

Profesa Kitila amesema eneo jingine ni kukuza biashara kati ya Tanzania na Korea kupitia kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na madini hali itakayowezesha kukuza uwezo wa Taifa hili katika soko huru la Afrika.
Waziri Makamba amesema mwelekeo wa Serikali ya kuendelea kushirikiana na mataifa mbalimbali ili kutimiza malengo ya maendeleo ya ndani utaendelea kwa sababu kuna manufaa makubwa sana.
“Manufaa yaliyopatikana Korea ni makubwa, ziara hii inafungua ukurasa kati ya Tanzania na Korea na sifa za taifa hilo zinajulikana hasa maendeleo ya kisayansi, teknolojia na maarifa.”

“Rais Samia alikutana na viongozi wakuu wa Korea Kusini na kampuni kubwa za nchini huko zikiwemo Samsung na Hyundai. Samsung ni mnyororo wa kampuni za ujenzi, utafiti na nishati, hivyo Rais Samia alikutana na rais wa Samsung kuzungumza ushirikiano katika maeneo mbalimbali,” amesema Waziri Makamba.
Naye, Waziri Nape amesema katika ziara hiyo, walifuatana na wabunifu wa biashara changa zinazohusiana na teknolojia katika ubunifu wao ambapo walitembelea kituo kikubwa cha kusaidia bunifu zinazotokea ndani na nje ya Korea.
Waziri Nape amesema kituo hicho, kinawasaidia kuboresha, kuzitafutia masoko bunifu na kuwapa mitaji au maeneo watakayoyatumia kuziendeleza bunifu zao ili kutoa matokeo na kusaidia katika uchumi wao wa Taifa hilo.
“Tumejifunza namna wanavyokusanya vijana na kuwasaidia kufikia ndoto zao wanafanya vizuri sana, katika mazungumzo ya awali tuliomba Korea watusaidie kutupa mkopo wa ujenzi chuo kikubwa cha Tehama jijini Dodoma.
“Lakini tumejifunza namna Korea walivyotumia teknolojia ya habari kuboresha huduma mbalimbali kupitia Tehama,” amesema Waziri Nape.
Kwa upande wake, Dk Ashatu amesema Tanzania ipo tayari kuanza majadiliano na Korea kuhusu ushirikiano wa kiuchumi katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo na madini.
Dk Kijaji amesema katika majadiliano hayo, wangependa Korea iwajengee uwezo wenye viwanda na wazalishaji wa mazao ya kilimo nchini, kuhusu viwango vya ubora wa bidhaa zitakazofikia vigezo vya ili kuuzwa popote.
“Moja ya jambo kubwa ni kujifunza kwa wenzetu, wanafanyaje au walifikaje kwenye viwango walivyonavyo leo ili tukizalisha bidhaa zetu ziende Korea, Marekani na masoko yote ya mataifa yaliyoendelea.
“Jambo jingine tunalopambana uendelevu wa biashara zetu, tumekuwa na changamoto hiyo kwa sababu tunazalisha kidogokidogo, unapata soko leo unapeleka bidhaa yako kwa mara kwanza na mara ya pili imeisha, hivyo hatuna mwendelezo, sasa tunataka kuwaita wawekezaji wakubwa waje ili tunapoanza kuzalisha, tuzalishe bidhaa za kutosha.
Ujenzi hospitali Binguni
Dk Mkuya amesema kuchelewa kwa ujenzi wa Hospitali ya Binguni Mjini Unguja kumetokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha. Amesema Serikali ilikuwa inaweka fedha zake za bajeti kidogo kidogo, wakati mchakato ukiendelea wa kutafuta fedha za ujenzi za Binguni.
“Lakini tumeona sehemu tutakayopata mkopo nafuu na teknolojia ya kisasa ya sekta ya afya ni Korea, kama mnavyoona Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila imejengwa na Korea ambao ni wazuri katika teknolojia,”amesema Dk Mkuya.
Katika ziara hiyo, Serikali imepokea mkopo wa Dola za Marekani 163.6 milioni kutoka Benki ya Exim ya Korea, kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo iliyopo Zanzibar na kituo cha mafunzo ya utabibu.