Mawakili wapya 524 wapokewa, kusajiliwa

Sehemu ya Mawakili wapya wakitoa heshima kwa Jaji Mkuu (hayupo kwenye picha).
Muktasari:
- Wamo majaji, wasajili wa Mahakama Kuu, mahakimu na maofisa wengine wa Mahakama.
Dar es Salaam. Mawakili wapya wa kujitegemea 524 wamesajiliwa wakiwemo majaji, wasajili wa Mahakama Kuu, mahakimu na maofisa wengine wa Mahakama.
Pamoja na hao, wamo wahitimu wa Shule ya Sheria waliofaulu mafunzo ya sheria kwa vitendo.
Mawakili hao wapya wa kujitegemea wamekubaliwa na kupokewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, leo Alhamisi Desemba 12, 2024 katika sherehe za 71 tangu mwaka 1986. Hafla imefanyika katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Miongoni mwa mawakili wapya ni Jaji wa Mahakama Kuu, Wilfred Dyansobera; Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Eva Nkya; Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Chiganga Tengwa. Pia wamo naibu wasajili wa Mahakama Kuu.
Mahakimu ni Richard Kabate, Rhoda Ngimilangwa, Vicky Mwaikambo, Harriet Marando, Lugano Kasebere. Yumo pia Katibu wa Jaji Mkuu, Venance Mlingi.
Akizungumza kabla ya mawakili hao kupokewa, Msajili wa Mahakama, Tengwa amesema kulikuwa na waombaji 747 lakini waliokubaliwa ni 528.
Tengwa amesema waliofika mbele ya Jaji Mkuu kwa ajili ya usajili walikuwa 526, mmoja hakufika na mwingine aliwekewa pingamizi.
Amesema wote waliofika mbele ya Jaji Mkuu wamefaulu lakini waombaji wawili wameshindwa kukamilisha taratibu za Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na hivyo kufanya waliokubaliwa kubakia 524.
Tengwa amesema kati ya waliokubaliwa na kupokewa wanaume ni 296 na wanawake 228.
Amesema idadi ya mawakili waliokubaliwa na kupokewa inajumuisha mawakili 294 waliohitimu mafunzo ya uwakili kutoka Shule ya Sheria Tanzania (LST).
Tengwa amesema 214 walipata msamaha wa kutokuhudhuria Shule ya Sheria ya Tanzania (kundi linalojumuisha wasajili, na mahakimu) na 16 waliofaulu baada ya kufanyiwa usajili na Baraza la Elimu ya Sheria nchi.
"Endapo mheshimiwa Jaji Mkuu utakubali na kuidhinisha maombi ya waombaji hawa, jumla ya mawakili watakaopokewa na kuandikishwa itaongezeka kutoka mawakili 12,471 na kufikia mawakili 12,995," amesema.
Idadi hiyo ya mawakili 12,995 inahusisha wanaofanya kazi za uwakili, walioacha kazi hizo au kustaafu, walio hai na waliofariki dunia, baada na kabla ya uhuru.
Jaji Mkuu kwa mamlaka aliyopewa kisheria amewakubali na kuwapokea mawakili hao wote na kuwakabidhi vyeti vya uwakili wa kujitegemea.
"Kwa mamlaka niliyopewa na Sheria ya Mawakili Sura ya 341 Toleo la mwaka 2019, kifungu cha 8(3), ninatamka kwamba wale wote ambao majina yao yamesomwa hapa wamekubaliwa kuwa mawakili na wameorodheshwa rasmi kwenye orodha ya mawakili kuanzia leo tarehe 12, Desemba 2024," amesema Profesa Juma na kuongeza:
"Kwa mamlaka niliyopewa na Sheria ya Mawakili Sura ya 341 Toleo la mwaka 2019, kifungu cha 8(3), ninawatunuku vyeti vya uwakili wa kujitegemea, mawakili wote waliopokewa na kukubaliwa leo hii kama walivyoorodheshwa katika kitabu cha orodha ya