MAWAIDHA: Mafunzo katika Hijra ya Mtume wa Allah
Muktasari:
- Katika sehemu hii ya pili tutaangazia Mafunzo na mazingatio yaliyomo Katika tukio la Kuhama Mtume wa Allah kutoka Makka kwenda Madina.
Katika toleo lililopita liliangazia Historia ya kuanzishwa kwa kalenda ya Kiislamu, ambapo khalifa wa pili wa Waislamu Umar ibn Al-Khattab (Allah Amridhie) na Maswahaba wenzake baada ya kushauriana walichagua tukio la Hijra (kuhama kwa Mtuma wa Alah kutoka Makka kwenda Madina) liwe mwanzo wa kalenda ya Kiislamu, na mwezi wa Muharram (Mfungonne) uwe wa kwanza katika kalenda ya Kiislamu ya Hijri.
Katika sehemu hii ya pili tutaangazia Mafunzo na mazingatio yaliyomo Katika tukio la Kuhama Mtume wa Allah kutoka Makka kwenda Madina.
Waislamu katika kila zama na kila mahali wanapasa kulikumbuka tukio hili la Hijra, kujifunza kwa kina matukio yake na kuchukua mafunzo na mawaidha yaliyomo ndani yake. Hakika katika Hijra ya Mtume kuna mawaidha kwetu.
Hii ni kwa sababu Hijra (kuhama) ya Mtume haikuwa kukimbia vita wala kukwepa mapambano. Bali ilikuwa ni kielelezo cha jihadi na kuimarisha misingi ya imani.
Hijra haikuwa kwa ajili ya kutafuta raha na mapumziko. Bali ilikuwa ni kuitikia amri ya Allah kwa lengo la kuanzisha upya maisha ya Kiislamu. Haikuwa safari ya kutafuta mahema, chakula, vinywaji. Bali ilikuwa ni kujiepusha na tamaa na manufaa ya kidunia.
Hijra ya Mtume wa Allah haikuwa kwa tamaa ya kuteka ardhi, kuwatisha watu wala kunyakua mali na utajiri wao. Lengo lake kuu lilikuwa kulinyanyua neno la Allah, kutekeleza hukumu (Sharia) ya Allah duniani, kusimamisha uadilifu baina ya watu, kuwafikishia waliodhulumiwa haki zao na kuzuia mikono ya madhalimu.
Maswahaba (Allah awaridhie), miongoni mwa Muhajirun (wahamiaji toka Makka) na Anṣar (wakazi halisi wa mji wa Madina na wenyeji wa Muhajirun), waliweza kutekeleza ahadi waliyojiwekea, nayo ni kuokomboa mji wa Makka na kuanzisha dola ya Kiislamu.
Hayo yalitokea baada ya kupatikana udugu wa kweli wa Kiimani baina ya Muhajirun na Anṣar. Udugu huo ulikuwa miongoni mwa mafanikio na ushindi makubwakwa Uislamu na Waislamu. Basi sisi leo hii tuko wapi katika udugu huu?! Yuko wapi Mwislamu anayegawana mali yake na ndugu yake Mwislamu mwenye mahitaji au aliyetaka hifadhi?!
Kutokana na nguvu ya Kiimani waliweza kuwagiwia ndugu zao hadi wake wao. Allah Mtukufu ameusifu undugu huu kwa kusema: “Na walioamini wakahama na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na waliotoa mahala pa kukaa (makazi) na wakanusuru, hao ndio Waumini wa kweli…” (8:74)
Hijra ya Mtume wa Alah ilibadilisha mkondo wa historia na ilikuwa na maana nyingi za kujitolea, usuhuba, subira, ushindi, kumtegemea Allah na udugu. Allah aliifanya kuwa njia ya kupata ushindi na heshima, kuinua bendera ya Uislamu na kuijenga dola yake. Allah Mtukufu amesema: “Msipomnusuru, basi Allah alikwishamnusuru walipomtoa wale waliokufuru….”
[9: 40]
Nafasi ya Mwanamke Katika Hijra.Katika historia ya Hijra walijitokeza watu wengi waliokuwa na mchango mkubwa. Miongoni mwao ni Aisha bint Abubakr Assidiq (Allah awaridhie) ambaye alituhifadhia simulizi ya Hijra, akaielewa vizuri na kuifikisha kwa umma. Pia alikuwapo dada yake, Asma, , ambaye alishiriki kumpelekea Mtume wa Allah na Abubakr (baba yake) maji na chakula walipokuwa pangoni wamejificha. Aidha, alivumilia maudhi katika njia ya Allah.
Wanazuoni wa Historia ya Kiislamu Ibn Is’ḥaq na Ibn Kathir wamesimulia katika Sira ya Mtume maneno ya Asma: “Mtume wa Allah na Abubakr walipohama kwenda Madina, walitujia watu kadhaa wa kabila la Kikuraishi, na miongoni mwao alikuwamo Abu Jahl ibn Hisham. Wakasimama mlangoni kwa Abubakr (baba yake). Nikawatokea, wakaniuliza: ‘Baba yako yuko wapi, ewe binti wa Abubakr?’ Nikawajibu: ‘Wallahi, sijui baba yangu yuko wapi.’ Abu Jahl akainua mkono wake, naye alikuwa mtu mwovu, akanipiga kofi shavuni mpaka hereni yangu ikaanguka. Kisha wakaondoka.”
Hili ni funzo kutoka kwa Asma (Allah Amridhie), analowafundisha wanawake wa Kiislamu kizazi baada ya kizazi: Namna ya kuzificha siri za Waislamu mbele ya maadui, na namna ya kusimama imara mbele ya nguvu za uonevu na dhuluma
Mapambano baina ya haki na batili ni ya zamani na yanaendelea; nayo ni miongoni mwa desturi za Allah. Allah amesema: “Wale waliotolewa katika nyumba zao bila ya haki, isipokuwa kwa sababu ya kusema: ‘Mola wetu ni Allah… [22: 40] Hata hivyo, mwisho wa mapambano hayo unajulikana. Allah amesema: “Allah ameandika: Bila shaka Mimi na Mitume Wangu tutashinda..”
[58: 21]
Njama na hila za maadui wa Uislamu dhidi ya Uislamu na walinganiaji wake, katika kila zama na kila mahali, ni jambo linaloendelea na kujirudia. Kwa hiyo, mlinganiaji wa Allah anapaswa kumkimbilia Mola wake, kumwamini, kumtegemea na kujua kwamba hila mbaya haiwapati isipokuwa wenyewe. Allah Mtukufu, amesema: “Na kumbuka wale waliokufuru walipokufanyia njama (ewe Muhammad) ili wakufunge, wakuue au wakutoe. Wao walifanya njama, na Allah akapanga; na Allah ndiye Mbora wa wapangaji.” [8: 30].
0712 690811