Mavunde: Enzi za Watanzania kubaki nyuma kwenye madini zimekwisha
Waziri wa Madini Antony Mavunde wakati akifungua Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCCF), jijini Mwanza. Picha na PraiseGod Mgumba
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Mavunde, kulikuwa na kilio kikubwa cha Watanzania kukosa fursa ya ushirikishwaji katika sekta ya madini ambacho Serikali imekitatua.
Mwanza. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Watanzania sasa wameongeza ushiriki wao katika sekta ya madini, wakishika nafasi mbalimbali za ajira, uongozi na utoaji wa bidhaa na huduma, hatua aliyosema ni matokeo ya utekelezaji wa sera na sheria za ushirikishwaji wa wazawa.
Akifungua jukwaa la tano la utekelezaji wa ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini (LCCF) leo Jumatano, Julai 22, 2026, jijini Mwanza, Mavunde amesema hali ilivyo sasa ni tofauti na miaka ya nyuma, Watanzania walikuwa wakinufaika kwa kiwango kidogo na rasilimali za madini.
Amesema kwa miaka mingi kulikuwa na malalamiko kwamba kampuni za madini zilitegemea bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi, hata kwa mahitaji ambayo yanaweza kupatikana nchini.
"Kilikuwa kilio cha Watanzania kwamba wanakosa fursa za kusambaza bidhaa na huduma migodini. Kulikuwa na wakati hata kuku na mayai vilikuwa vinaagizwa kutoka nje ya nchi, jambo lililoonyesha Watanzania hawakushiriki kikamilifu katika uchumi wa sekta ya madini," amesema Mavunde.
Waziri Antony Mavunde akisilikiza maelekezo kutoka kwa Meneja wa Geita Gold Mining Limited, Dominick Marandu wakati akipita katika mabanda kwenye tukio hilo. Picha na PraiseGod Mgumba
Amesema baada ya Serikali kusikia malalamiko hayo, ilifanya marekebisho ya sheria na kanuni ili kuhakikisha Watanzania wanapewa nafasi kubwa zaidi katika shughuli za sekta hiyo.
"Leo, kutokana na usimamizi mzuri wa sheria na kanuni zake, tunaanza kuona matokeo. Watanzania sasa wako mstari wa mbele katika sekta ya madini na wanashika nafasi muhimu katika makampuni mbalimbali," amesema.
Kwa mujibu wa Mavunde, zaidi ya Watanzania milioni sita wanashiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini kupitia shughuli mbalimbali, ikiwamo uchimbaji mdogo, huku ajira rasmi zikifikia 20,421.
Amesema kati ya waajiriwa hao, Watanzania ni 16,695, sawa na asilimia 96 ya wafanyakazi wote katika ajira rasmi za sekta hiyo.
Mbali na ajira, amesema ushiriki wa Watanzania katika nafasi za uongozi umeongezeka kwa kiwango kikubwa tofauti na ilivyokuwa zamani. nafasi nyingi za juu zilishikiliwa na wageni.
Katika eneo la ununuzi, Mavunde amesema migodi nchini hutumia takribani Sh5.1 trilioni kila mwaka kununua bidhaa na huduma, huku Serikali ikilenga kuhakikisha angalau asilimia 90 ya fedha hizo zinabaki nchini kupitia kampuni za Watanzania.
Amesisitiza kuwa msimamo huo haulengi kuwabagua wawekezaji wa kigeni bali kuhakikisha wananchi wananufaika zaidi na rasilimali za nchi.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Dk Janet Lekashingo akizungumza katika Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCCF) jijini Mwanza. Picha na PraiseGod Mgumba
"Isiwekwe tafsiri kwamba tunafanya ubaguzi. Tunachosisitiza ni utekelezaji wa sheria ili Watanzania wapate nafasi wanazostahili katika sekta ya madini," amesema.
Akizungumzia malalamiko ya baadhi ya wawekezaji kuhusu mabadiliko ya sheria, amesema hakuna sheria mpya iliyotungwa, bali Serikali inasimamia utekelezaji wa Sheria ya Madini ya mwaka 2017, hususan kifungu cha 133 kinachohusu ushirikishwaji wa Watanzania na uwajibikaji kwa jamii.
Amesema Serikali imebaini baadhi ya wawekezaji walikuwa wakitumia mianya ya sheria kwa kuingia ubia na Watanzania ambao hawakuwa na shughuli zinazofanana na kampuni zao ili kukidhi matakwa ya kisheria.
Kutokana na hali hiyo, amesema kanuni zimeboreshwa ili kuhakikisha ubia unafanyika kati ya kampuni zinazojihusisha na shughuli zinazofanana.
"Ikiwa kampuni inajihusisha na huduma za milipuko, basi mshirika wake wa Kitanzania lazima awe na kampuni inayofanya shughuli hizo. Huo ndiyo ushirikishwaji halisi tunaoutaka," amesema waziri huyo.
Amesema wizara itaendelea kufuatilia utekelezaji wa sheria hizo na haitasita kuchukua hatua kwa kampuni zitakazokiuka masharti ya ushirikishwaji wa wazawa.
Amesema tayari Serikali imezipa baadhi ya kampuni muda wa mwaka mmoja kuhamisha ujuzi kwa Watanzania kabla ya kusitisha shughuli ambazo zinaweza kufanywa na wazawa.
Washiriki katika Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCCF) wakisikiliza mawasilisho. Jijini Mwanza. Picha na PraiseGod Mgumba
"Wakati umefika Watanzania wawe sehemu ya maendeleo ya sekta ya madini, si kwa jina tu bali kwa vitendo. Tutasimamia hilo kwa nguvu zote," amesema.
Aidha, amewataka Watanzania wanaopewa fursa kuhakikisha wanatoa huduma zenye ubora na ushindani, akisisitiza kuwa uzawa pekee haupaswi kuwa sababu ya kupata zabuni bila kuzingatia viwango.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dk Janet Lekashingo amesema utekelezaji wa sera ya ushirikishwaji wa wazawa umeendelea kuimarika, akibainisha kuwa idadi ya kampuni zilizowasilisha mipango ya ushirikishwaji imeongezeka kutoka 51 mwaka 2018 hadi 1,312 mwaka 2025.
Naye Meneja wa Rasilimali Watu wa Geita Gold Mining Limited (GGML), Dominick Marandu amesema asilimia 98 ya wafanyakazi zaidi ya 7,000 wa mgodi huo ni Watanzania, huku asilimia 97 ya manunuzi yaliyofanyika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026 yakitoka kwa kampuni za wazawa.